Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, October 13, 2015

SERIKALI YAJIPANGA KUDHIBITI MAGONJWA YA NIMONIA NA KUHARA KWA WATOTO

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, akitoa hotuba ya ufunguzi wa Warsha kwa Maafisa afya kuhusiana na Ugonjwa wa Nimonia na Kuhara kwa watoto wadogo.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini,wizara ya afya na ustawi wa jamii, Nsachris Mwamwaja akitoa taarifa ya Serikali kuhusiana na udhibiti wa magonjwa ya kuhara na Nimonia kwa watoto

Mganga mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina akitoa taarifa ya hali ya magonjwa ya kuhara na Nimonia kwa watoto katika Mkoa wa Mbeya

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Groly Mbwile akizungumza jambo kwa niaba ya madaktari.

Baadhi ya washiriki wa Warsha wakifuatilia kwa makini mada zinazotolewa

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Washiriki wa Warsha wakipata maelezo namna ya kuwatibu wagonjwa wa kuhara na Nimonia

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya pamoja na washiriki wa Warsha wakipata maelekezo na hatua za kufuata kabla ya kumhudumia mgonjwa wa Kuhara

Washiriki wa Warsha wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya
 

SERIKALI imesema Tanzania imefanikiwa na kufikia kwa kiwango kikubwa malengo ya milenia ya kupunguza vifo kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
 
Aidha imeelezwa kuwa kupungua kwa vifo hivyo ni kutokana na kugunduliwa kwa magonjwa sababishi ambayo ni Kuhara na Nimoni hivyo kuwekewa mpango mkakati wa kuondokana na magonjwa hayo.
 
Hayo yalibainishwa  na mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini,wizara ya afya na ustawi wa jamii Nsachris Mwamwaja katika Warsha kuhusu mkakati wa kuimarisha kinga ya kuharisha na Nimonia kwa Waganga Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mbeya iliyofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
 
Mwamwaja alisema lengo la serikali ni kuona magonjwa hayo hayaendelei kuwa tishio kwa jamii nchini  kwa kutoa elimu kwa akina Mama kuzingatia usafi wakati wa kunyonyosha watoto.
 
Alisema vifo vya watoto vinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa iwapo kila mtoto mwenye nimonia atapewa dawa ya Amoxicilian na kila mtoto anayeharisha atapewa dawa ya ORS na Zinki.
 
Awali akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema Watoto 76 walifariki dunia mkoani Mbeya mwaka 2014 kutokana na magonjwa ya Nimonia na kuhara.
 
Kandoro alisema magonjwa hayo huchangia kwa kiasi kikubwa katika jumla ya wagonjwa wanaohudhuria kwenye vituo vya huduma ya afya ikiwa ni kwa wale waliolazwa na kwa wanaopata huduma nje mkoani hapa.
 
Alisema mwaka 2014 jumla ya watoto 262,452 walihudhuria katika vituo mbalimbali vya tiba,kati yao watoto 42,532  sawa na asilimia 16 waliugua ugonjwa wa kuharisha na watoto 3,644 sawa na asilimia nane walilazwa na kati ya watoto waliolazwa  33 sawa na asilimia moja walifariki.
 
Alisema kwa upande wa Nimonia  idadi ya watoto waliougua mwaka 2014 ilikuwa 55,842  kati yao waliolazwa walikuwa 2,647 sawa na asilimia 4.7 na vifo vilikuwa 43 sawa na asilimia mbili.
 
Akizungumzia utekelezaji wa shughuli za chanjo kwaajili ya kuzuia nimonia na kuhara iliyozinguliwa na serikali mwaka 2013,Kandoro alisema mwaka 2014 mkoa ulitarajia kuchanja watoto wapatao 112,508 kwa chanjo ya nimonia na walichanjwa 106,700 sawa na asilimia 95 na kwa Kuharisha walichanjwa watoto 112,571 sawa na asilimia 100.
 
Alisema  uhamasishaji wa Tiba na kinga ya magonjwa hayo,Kandoro aliwataka viongozi katika kuanzia ngazi ya mkoa,wilaya na halmashauri kushirikiana kwa karibu na jamii ili kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo kama si kuvimaliza kabisa.
 
Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya Dk.Seif Muhina alisema kwa sasa mwamko wa wakazi wa mkoa huo katika kushiriki masuala ya chanjo ni mkubwa hivyo kuthibitisha kuwepo na uhakika wa hamasa ya kinga ya magonjwa hayo kufanikiwa.
 

No comments: