Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Featured Posts

Friday, April 29, 2016

WATU WATATU WANAOSADIKIWA KUWA MAJAMBAZI WAUAWA NA JESHI LA POLISI KATIKA MAJIBIZANO YA RISASI CHUNYA MKOANI MBEYAKaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya  Butusyo Mwambelo akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya  (Hawapo pichani)katika kuzngumzia tukio la kuuawa kwa majambazi watatu wakati wakijaribu kufanya uhalifu katika duka la kuuzia  vinywaji mji mdogo wa Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akionyesha silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 na risasi 26 kwenye magazine ambayo ilikuwa ikitumika na majambazi hao katika tukio la kutaka kufanya uhalifu kwenye duka la vinywaji mali ya Hamisi mji mdogo wa Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya April 27 mwaka huu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akionyesha panga ambalo linadaiwa kutumiwa na majambazi hao .

Baadhi ya askari polisi wakifuatilia kwa makini mkutano wa kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo wakati akizungumza na waandsihi wa habari kufuatia tukio la kuuwawa kwa majambazi watatu waliotaka kufanya uhalifu katika duka la vinywaji vya jumla linalomilikiwa na Hamisi Mkazi wa Matundasi Chunya Mkoani Mbeya .
Silaha mbalimbali zilizo kamatwa katika tukio la kuuwawa kwa majambazi wilayani Chunya mkoani Mbeya Aprili 27 mwaka huu.
 
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika majibizano ya kurushiana risasi wakiwa katika majaribio ya kufanya uhalifu kwenye duka la Bia la Jumla.
 
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo, alisema tukio hilo lillitokea juzi majira ya saa mbili usiku katika kijiji cha Matundasi Wilaya ya Chunya Mkoani hapa.
 
Mwambelo alisema siku ya tukio majambazi hao walikuwa watano na walibebana kwenye pikipiki mbili ambapo majambazi watatu walipanda pikipiki moja huku wengine wawili wakiwa wamepanda nyingine.
 
Alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa ya kiinterensia na kufanikiwa kujipanga ili kukabiliana na majambazi hao ambapo katika majibizano ya risasi jambazi mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Baraka anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 35 – 38  mkazi wa Makongolosi na fundi ujenzi   aliuawa kwa kupigwa risasi tumboni na mgiuuni.
 
Alisema marehemu baada ya kukaguliwa alikutwa  na silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 ikiwa na risasi 26 kwenye magazine,na kwamba majambazi wengine wanne walifanikiwa kukimbia kuelekea Kijiji cha Matondo na ndipo askari waliendesha msako kuwatafuta.
 
Alisema baada ya majambazi kuwaona askari waliwasha pikipiki zao kwa nia ya kukimbia huku wakirusha risasi ovyo ndipo Polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi wawili na kukamata pikipiki moja yenye namba za usajili MC 761 AFS aina ya Sanlg iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao pamoja na Begi moja lenye tochi na Panga..
 
Alisema majambazi wengine wawili walifanikiwa kukimbilia kusiko julikana ambapo Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali likishirikiana na wananchi ili kuwakamata waliotoroka na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
 
Aliongeza kuwa majina ya miili ya majambazi wawili hayajafahamika ambapo alitoa wito kwa wananchi kufika katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kuwatambua ikiwa ni pamoja na kuchukua miili yao baada ya kufuata utaratibu baada ya kuwatambua kwa ajili ya kuwazika kutokana na Hospitali hiyo kukabiliana na changamoto ya Chumba cha kuhifadhia maiti.
 
Aidha Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Butusyo Mwambelo anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri ili kuzuia vitendo vya kihalifu mapema kabla ya kutokea.
 
    

Thursday, April 28, 2016

MKUU WA MKOA WA MBEYA AMOS MAKALLA AZINDUA MRADI WA UIMARISHAJI WA MIFUMO YA SEKTA ZA UMMA(PS3)

Mkurugenzi wa Mradi wa PS3 Dk. Emmanuel Malangalila akitoa taarifa ya Mradi huo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi iliyofanyika katika ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya.

Mratibu wa Mradi wa PS3 Beatha Swai akieleza malengo na matarajio ya mradi huokwa Halmashauri za Mkoa wa Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma uliozinduliwa kimkoa jijini Mbeya

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) Shanon Young akitoa neno katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa PS3 ambao umedhaminiwa na Serikali ya Marekani

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja (aliyesimama) akitoa utambulisho wa wageni katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa PS3


Wakuu wa Idara na viongozi mbali mbali wakifuatilia shughuli za uzinduzi wa Mradi katika ukumbiwa Tughimbe Mafiati jijini Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya  Mbeya, Nyerembe Munasa akitoa neno la shukrani baada ya hotuba ya mgeni rasmi

Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja

Viongozi wakiagana

Washiriki wakiwa kwenye ukumbi wa Mikutano
 
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema uimarishwaji wa mifumo ya sekta za Umma nchini utasaidia kuondoa tatizo sugu la watumishi hewa endapo utekelezaji wake utafanyika vizuri.
 
Makalla aliyasema hayo  alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mradi wa Uimarishaji mifumo ya Sekta za Umma mkoani Mbeya uliofadhiliwa na shirika la Msaada la Marekani (USAID) katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya.
 
Mkuu huyo wa Mkoa alisema Mradi huo umekuja katika kipindi muafaka ambacho serikali ya awamu ya tano inajitahidi kuhakikisha inahimiza na kurekebisha iliyokuwepo katika Sekta za Umma ili kurahisisha utoaji huduma bora kwa wananchi.
 
Alisema Mradi huo utasaidia kuweka mfumo mzuri ambao utaondoa kabisa tatizo la watumishi hewa katika taasisi za umma na kuboresha mfumo wa utendaji kwa watumishi kutimiza wajibu wao kwa kiwango chenye ubora na wakati unaostahili.
 
Awali akisoma taarifa katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mradi, Dk. Emmanuel Malangalila alisema mradi huo utahakikisha mifumo iliyopo katika ngazi ya Halmashauri inaimarishwa kupitia kitita cha afua zilizoundwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi wa Tanzania.
 
Dk. Malangalila alisema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2015 hadi 2020 ambapo mafanikio yanategemewa kutokea kwenye sekta ya Utawala bora na ushirikishwaji wa raia ambapo Rasilimali za taifa zitatumika kwa uwazi, kuwawezesha ushiriki wa wananchi katika kupanga, kufuatilia na kutoa matokeo katika kila sekta.
 
Alisema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwenye maeneo yenye uhitaji zaidi, kuimarisha mfumo wa ajira pamoja na kudumu kwa watumishi katika ajira serikalini.
 
Aliongeza kuwa mradi huo pia utasaidia ongezeko la pato la ndani kwa ajili ya huduma za umma, kuongezeka kwa ufanisi katika matumizi ya fedha za umma pamoja na kuongeza uwiano kati ya kiasi cha fedha kilichotumika na mali iliyonunuliwa jambo ambalo litapunguza hati chafu na zenye mashaka kwenye halmashauri.
 
Dk. Malangalila alisema kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji taarifa iliyopo nchini pamoja na matumizi ya takwimu kwa wadau utasaidia kutokuwa na takwimu za kutengenezwa ambapo pia Mradi huo utasaidia katika tafiti tendaji zitakazosaidia mradi kujua changamoto na mikakati  ya kuzishughulikia changamoto hizo.
 
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo kutoka Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi, Beatha Swai alisema Mradi huo unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania Bara ambayo ni Iringa, Dodoma, Kagera, Kigoma,Lindi, Mara,Mbeya, Morogoro, Mtwara,Mwanza, Njombe, Rukwa na Shinyanga.
 
Alisema uzinduzi wa mradi huo umeshafanyika katika Mikoa ya Iringa, Shinyanga, Dodoma na Morogoro huku Mikoa ya Mtwara, Mwanza na Mbeya ikizindua kwa pamoja ambapo alisema mategemeo ya Wizara ni kuwa mradi huo utasaidia kuwajengea uwezo watumishi wa Halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yao.
 

Wednesday, April 27, 2016

MAKALLA ATEMA CHECHE KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI WAKIWEMO MADIWANI

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya na viongozi wa Jiji la Mbeya wakikagua Soko la Kimataifa la Mwanjelwa ambalo halitumiki kutokana na wafanyabiashara kuhofia ukubwa wa kodi

Baadhi ya Wafanyabiashara wakilalamikia Chumba kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya Dampo kudaiwa kupangishwa kwa Mfanyabiashara kinyume na matumizi yaliyokusudiwa

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya wakipita mbele ya Vizimba vya wafanyabiashara wadogo ambavyo pia havitumiki kutokana na kodi kuwa kubwa

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akikagua Soko la Mwanjelwa

MKUU wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla amewaagiza Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuisimamia Halmashauri ili isonge mbele katika shughuli za maendeleo.
Agizo hilo alilitoa  katika ziara yake ya kujitambulisha alipokuwa akiongeza na madiwani, watumishi wa halmashauri, viongozi wa mila na viongozi wa dini katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Makalla alisema Madiwani wanayonafasi ya kuisimamia Halmashauri kwa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kama inavyotakiwa, pamoja na kusimamia asilimia kumi za mapato kwenda kwenye mikopo ya vikundi  vya Vijana na akina mama.
“Kazi ya madiwani sio kususia vikao na kudai posho, nyie majukumu yenu ni kuisimamia halmashauri kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa na zile asilimia kumi zinatengwa na kuwafikia walengwa, kwanza itakuongezea kura kwenye uchaguzi ujao” alisema Mkuu wa Mkoa.
Makalla alisema Madiwani hawapaswi kupokea posho za vikao kama kikao kitakuwa kimevunjika lengo likiwa ni kubana matumizi na kuokoa fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Aidha aliwanyoshea vidole Watendaji wa Kata na vijiji pamoja na viongozi wote kuanzia ngazi ya kijiji kuhakikisha wanasoma mapato na matumizi kwa wananchi ya fedha walizochangia.
“Wasiosoma mapato na matumizi siku zao zinahesabika, haiwezekani mradi mmoja haujakamilika mnawachangisha wananchi michango mingine hapo lazima kuna ufisadi ambao  mbele yake utasababisha migogoro katika jamii” alisisitiza Makalla.
Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza kuwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni marufuku mawakala kutumika kukusanya ushuru ndani ya halmashauri bali kazi hiyo inapaswa kufanywa na watumishi wenyewe.
“Ni marufuku mawakala kutumika kukusanya mapato kwanzia mwaka wa fedha ujao kwani wanasababisha kero kwa wananchi pia wao wanapata faida kubwa kuliko halmashauri, watumishi wako wengi wengine wanakaa maofisini bure tu hivyo watakaa kwenye mageti kukusanya ushuru kwa kutumia mashine ya kielekroniki” aliagiza Makalla.
Wakati huo huo Makalla aliagiza Watumishi wote katika Mkoa wa Mbeya kurudi kwenye vituo vyao vya kazi kwa ajili ya kuhakikiwa upya ambapo alitoa kuanzia tarehe 20 hadi 24 Aprili 2016 kuwa muda wa kusafiri na kwamba zoezi litaanza Aprili 25 hadi 29,mwaka huu.
Alisema amelazimika kurudia zoezi la kuhakiki baada ya kubainika kuongezeka kwa watumishi hewa katika Halmashauri ya Jiji na Wilaya ya Mbeya ambapo Halmashauri ya Wilaya imeongezeka kutoka watumishi 9 hadi 13 huku Jiji wakiongezeka kutoka 14 hadi 23.
Alisema ili kufanikisha zoezi hilo ameunda kikosi cha watu 14 ambapo mtumishi atapaswa kuonekana kwa sura akiwa na barua ya kazi, kitambulisho na slipu ya Mshahara wa mwisho wa mwezi.

Thursday, April 21, 2016

WAJANJA WAANZA KUJIMEGEA UWANJA WA NDEGE WA ZAMANI MBEYA

Muonekano wa Ofisi za Uwanja wa  ndege wa Zamani wa Mbeya unaodaiwa kuvamiwa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Airport,  Enock Mwampagama akifafanua jambo  kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu uvamizi wa Uwanja wa ndege

Baadhi ya Waandishi wa habari wakipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Airport

Baadhi ya Waandishi wakiangalia mawe (bikons) zilizowekwa katika mashamba ambayo wananchi wamepimiwa ndani ya Uwanja wa Ndege

Moja ya Jiwe likionesha kiwanja kilichopimwa

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Pambogo wakicheza kwenye uwanja wa Ndege ambapo wanalia kukosa eneo la kuchezea licha ya watu kugawana maeneo

Njia ya kurukia ndege ambayo sasa imegeuka uwanja wa kujifunzia kuendeshea magari
 
MUDA mfupi kupita baada ya Serikali kujenga na kuzindua Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe uliopo Wilaya ya Mbeya Mkoani Hapa, Baadhi ya Wananchi wameanza kujipimia na kugawana uliokuwa Uwanja wa ndege wa zamani uliopo Iyela jijini Mbeya kwa matumizi binafsi.
 
 
Idadi ya viwanja vinavyodaiwa kuuzwa ni kati ya 60 hadi 70 ambapo jopo la wanahabari wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania  (TAJATI) walitembelea na kukuta mawe yaliyopimwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi.
 
 
Imeelezwa kuwa viwanja hivyo vyenye thamani ya kuanzia sh mil 20 hadi sh mil 50 kila kimoja vimegawiwa kwa wananchi huku ikielezwa kuwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Mwanguku kuwa ndiye anayemiliki eneo hilo kabla ya kuanzishwa kwa uwanja huo zaidi ya miaka 50 iliyopita.
 
 
Uwanja huo wenye urefu unaokadiriwa km 2.7 uliopo Iyela jijini Mbeya umedaiwa kuuzwa kwa wananchi wa eneo hilo huku kukiwa na madai kuwa baadhi ya Watumishi wa Halmsahauri ya Jiji la Mbeya wanahusika na uuzwaji wa eneo la uwanja huo.
 
 
 
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka TAJATI, Mwenyekiti wa Mtaa wa Airport,  Enock Mwampagama alikiri kuona uwanja huo umevamiwa huku kukiwa na baadhi ya viwanja vilivyopimwa na baadhi ya watu wakiendelea kulima eneo hilo.
 
 
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Pambogo ambako uwanja huo umepakana na mtaa huo Esia Edward, alisema  mara baada ya kuona eneo hilo linavamiwa alitoa taarifa ya uvamizi huo serikalini ambako hakupata mrejesho juu ya uvamizi huo.
 
Mwenyekiti wa mtaa wa Block T Adrian Majembe, alisema  ameona uvamizi mkubwa ukiendelea eneo hilo na kuwa hata hivyo yeye kama Mwenyekiti wa mtaa unaopakana na uwanja huo hakushirikishwa kwa lolote na kuwa amesikia eneo hilo la viwanja lilikuwa ni la familia ya mtu aliyetambulika kwa jina la Mwanguku ambaye inadaiwa eneo hilo ni mali ya familia hiyo.
 
 
Alisema wakazi wa eneo hilo walidai kuwa eneo hilo wamegaiwa na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipokuja Jijini Mbeya.
 
 
Alisema hata yeye alisikia watu wakisema wananchi wamegawiwa viwanja na wameruhusiwa kujenga eneo hilo na Waziri Lukuvi, Majembe ambaye aliwahi kuwa  Meya wa Manispaa ya Mbeya kati ya mwaka 1994-2000.
 
 
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iyela Henry Shipela alisema mara alipopata taarifa za uvamizi wa eneo hilo alifuatilia na kukuta watu wakiwa wanalima na kuwa baada ya kuulizia baadhi ya watu akaambiwa kuwa ni familia ya watumishi wa uwanja wa ndege na kuwa hata hivyo atafuatilia kujua sababu zaidi juu ya uvamizi wa uwanja huo.
 
 
Akizungumzia suala la uvamizi wa uwanja huo Meneja wa Uwanja wa Kimataifa wa Songwe, Hamis Amir, alisema  amesikia suala la uvamizi wa uwanja ndege wa Iyela ambao ulikuwa ukitumika awali kabla ya kuanzishwa kwa uwanja wa Songwe mwaka 2012 lakini hata hivyo hajui vyema mipaka ya uwanja huo.
 
 
Mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya Jiji anayeelezwa alihusika katika upimaji huo aliyetambulika kwa jina la Ben Mponzi alisema kuwa uwanja huo ulipimwa na Ofisa Mpima Ardhi wa Jiji la Mbeya Athuman Maugo ambaye naye alidai kuwa eneo hilo lilipimwa kwa idhini ya serikali na si Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
 
 
Kwa upande wake  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Dkt Samwel Lazaro, alisema  Halmashauri ya Jiji la Mbeya haihusiki na jambo lolote kuhusu uwanja wa ndege wa Airport.
 
 
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja alisema Serikali ya Mkoa imeandika barua serikali kuu ili kuomba kibali cha kubadili matumizi ya uwanja huo ikiwa ni kutumia katika sekta ya uwekezaji.
 

Wednesday, April 20, 2016

WATOA MSAADA WA MILIONI 1.7 KUJENGA CHOO CHA WALIMU

 
Diwani wa Kata ya Isapulano Wilaya ya Makete Alphonce Mbilinyi akizungumza neno baada ya kupokea msaada wa fedha wa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu katika Shule ya Msingi Ivilikinge.

Afisa Mtendaji akipokea Msaada kutoka kwa kiongozi wa Mwapima Forum ndugu Tito Tweve

Baadhi ya viongozi wa Mwapima forum wakikabidhi mfuko wa saruji kwa viongozi wa Kijiji na Kamati ya Shule ya Ivilikinge kwa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu


Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Ivilikinge, Ibrahim Fungo, akipokea kipande cha Malumalu kwa ajili ya kujengea Choo cha Walimu shuleni kwake

Mwalimu Mkuu akipokea Peni kwa ajili ya matumizi ya walimu

Baadhi ya viongozi wakikabidhiana vifaa mbali mbali kwa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu

Tito Tweve akizungumza na wananchi wa Ivilikinge kuhusu kuguswa na hatimaye kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa Choo cha Walimu

Wanachama wa Mwapima forum wakiangalia mazingira ya Choo cha walimu wa Shule ya Msingi Ivilikinge ambacho kimechakaa na hakifai kwa matumizi ya binadamu

Wanafunzi wakitoa burudaniMazingira na hali halisi ya Choo cha Walimu

Choo cha Wanafunzi ni bora na cha kisasa tofauti na choo cha Walimu

VIJANA nchini wameshauriwa kuwa na utamaduni wa kukumbuka asili yao kwa kurudi kushiriki katika shughuli za maendeleo katika maeneo waliyotoka badala ya kuwaachia wazazi pekee licha ya umri wao kuwa mkubwa.

Wito huo ulitolewa na Baadhi ya Vijana waishio nje ya Kijiji cha Ivilikinge Kata ya Isapulano Wilaya ya Makete mkoani Njombe waliounda umoja wao unaojulikana kwa jina la Mwapima Forum wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi wa vyoo vya walimu katika Shule ya Msingi Ivilikinge.

Akisoma taarifa kwa niaba ya wenzake, Mratibu wa Mwapima Forum, Award Mpandila alisema umekuwa utamaduni kwa vijana kutoka katika maeneo waliyozaliwa na kukulia na kuelekea sehemu nyingine kutafuta maisha lakini pindi wanapofanikiwa hujisahau na kushindwa kurudi kuchangia shughuli za maendeleo.

Alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya Vijana wapatao 60 waliosoma shule ya Msingi Ivilikinge kutoka maeneo mbali mbali ya Ndani na Nje ya Nchi walijikusanya kupitia mitandao ya kijamii kwa lengo la kufahamiana na kupeana taarifa za kijijini kwao kuona kama kuna changamoto ambazo wanaweza kusaidia kuzitatua.

Mpandila alisema umoja huo ambao ulianzishwa Disemba 21, mwaka jana baadhi ya wanachama wake walibaini kuwepo kwa Changamoto ya Choo cha Walimu katika Shule hiyo huku Wanafunzi wakitumia vyoo vya kisasa vilivyojengwa kwa msaada wa watu wa Marekani(USAID).

Alisema umoja huo uliamua kuchangishana ili kutatua tatizo la Choo kwani Walimu walikuwa wakitumia Choo kilichochakaa na wakati mwingine walilazimika kufuata huduma hiyo majumbani mwao.

Alisema katika makusanyo hayo zaidi ya shilingi Milioni 1,763,700 zilikusanywa ambazo zitaweza kumudu gharama za ujenzi wa Choo kimoja chenye matundu mawili hadi kukamilika kutokana na mahitaji muhimu kununuliwa na kukabidhi kwa serikali ya Kijiji na Kamati ya Shule kwa ajili ya usimamizi.

Akisoma risala ya Shule katika hafla hiyo, Mwalimu Atuwene Fungo alisema Walimu walikuwa wakitumia kwa hofu kubwa choo chao kutokana na kuchakaa kwani kilijengwa muda mrefu bila kuwa na miundombinu ya kudumu ambapo kilijengwa Mwaka 1976 wakati shule hiyo ikianzishwa.

Alisema msaada uliotolewa na vijana hao utasaidia Walimu kuokoa muda wa kufuata huduma ya choo mbali na mazingira ya shule hivyo itarahisha wao katika ufundishaji kutokana na mwalimu kuwepo muda wa kutosha katika mazingira ya shule.

Alisema changamoto zingine ni upungufu wa Walimu, uchakavu wa miundombinu, madawati, upungufu wa Walimu na vifaa vya kufundishia jambo ambalo Vijana waishio nje ya Kijiji hicho waliahidi kutatua baadhi kama Madawati na vifaa vya kufundishia pamoja na ujenziwa madarasa mapya.

Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Isapulano ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Alphonce Mbilinyi, licha ya kuwapongeza vijana hao kwa juhudi walizoonesha za kukumbuka nyumbani kwao kwa kuwasaidia walimu aliahidi kusimamia ujenzi wa Choo hicho na kuhakikisha kinakamilika ndani ya siku kumi na nne.

“Sina maneno mengi ya kuongea nimeguswa na jambo la hawa vijana nawapongeza sana ni mfano wa kuigwa na watu wengine mkumbuke kuja kutusaidia wazee wenu, nawaahidi ujenzi wa hiki choo utaanza haraka sana na ndani ya wiki mbili utakuwa umekamilika, Hapa kazi tu” alisema Diwani Mbilinyi.

Nao baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Ivilikinge, Emelite Sanga,Luthi Msigwa,Ezron Tweve na Cosmas Luvanda walisema wanafarijika kuona watoto wao wanakumbuka nyumbani na kusaidia shughuli za maendeleo leo kwa jambo hilo litawapunguzia mlundikano wa michango mbali mbali katika Kijiji chao.