Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, October 14, 2015

MBEYA PRESS FC YAAMBULIA KICHAPO KUTOKA KWA LUTETE FC

Timu ya Kijiji cha Lutete Kata ya Kisondela ikiwa tayari kuwakabili wageni wao ambao ni timu ya Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya

Mwandishi mkongwe na Mwenyekiti mstaafu wa MBPC, Jonas Mwasumbi  akitoa mawaidha kabla ya kuanza kwa mtanange baina ya Wanahabari na wanakijiji wa Lutete

Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mbeya Press Club, Joachim Nyambo(kushoto) akiwaongoza wachezaji wenzie kupasha misuli joto kabla ya kukabiliana na wenyeji wao timu ya Lutete

Wachezaji wa Mbeya Press wakibadilishana mawazo

Baadhi ya Wachezaji tegemeo wa Mbeya Press wakipasha misuli joto tayari kwa ajili ya mtanange na wanakijiji.


WANACHAMA wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya walijikuta wakionja machungu ya ziara yao katika Kata ya Kisondela Wilaya ya Rungwe mkoani hapa baada ya kuambulia kipigo katika mechi ya kirafiki.

Wanachama hao wa Mbeya Press walicheza mechi ya kirafiki na timu ya Kata ya Kisondela ambayo ilishinda kwa magoli matatu kwa nunge katika mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki katika kiwanja cha shule ya Msingi Lutete.


Katika mchezo huo MBPC FC iliweza kutawala mchezo katika dakika 45 zote za kwanza japo haikuweza kutamba katika lango la wapinzani wao kwa kufunga hata goli moja lakini hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imethubutu kutikisa nyavu za mpinzani wake.

Kipindi cha pili kilianza kwa MBPC kuonesha uhai katika dakika kumi za kwanza lakini baada ya hapo mabadiliko ya wachezaji kadhaa yaliyofanywa na timu ya wenyeji yaliionesha kudhoofisha kwa kiasi kikubwa upnde wa kiungo wa timu ya wanahabari na  hapo ndipo hali ya mchezo ilibadilika na wanahabari kuwa katika wakati mgumu.

Timu ya kata ya Kisondela ilianza kujipatia goli la kwanza kunako dakika ya lililofungwa na  Thadeo Leonard,huku goli la pili likapatikana dakika ya 72 na la tatu dakika ya 80 ya mchezo magoli ambayo yalifungwa na Raha Noah.

Akizungumzia kufungwa kwa timu ya MBPC FC mwenyekiti wa kamati ya michezo na burudani,Joachim Nyambo alisema zipo sababu nyingi zilizopelekea timu yake kupata matokeo hayo ikiwemo uchovu na pia baadhi ya wachezaji tegemeo kutokuwepo kwenye msafara huo.

“Sote tunatambua wachezaji wameingia uwanjani wakiwa na uchovu wa safari ya kutoka jijini Mbeya mpaka hapa kijijini Lutete.Tulihitaji kupata muda kwaajili ya mapumziko lakini tumefika leo na kucheza mechi.Ilikuwa vigumu kutoka na ushindi”

“Lakini pia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya msiba wa mwanahabari mwenzetu Jane Lawa baadhi ya wanahabari wameshindwa kujumuika nasi katika msafara huu kwakuwa wamelazimika kubaki kwa ajili ya kuupokea mwili wa marehemu unaosafirishwa kutoka jijini Dar es salaam hadi jijini Mbeya.Kati ya wanahabari waliobaki jijini wamo pia wachezaji ambao kimsingi ni tegemeo kwenye timu yetu.Ndiyo sababu utaona hapa uwanjani tumekosa hata mchezaji mmoja wa akiba” alisisitiza Nyambo.

Kwa upande wao wakazi wa kata ya Kisondelo waliipongeza timu ya MBPC FC wakisema walitarajia ingekuwa timu rahisi kuifungwa kwakuwa wachezaji wake ni watu wenye majukumu mengi lakini walionesha upinzani wa kutosha kwenye mchezo huo.

Mmoja wa wakazi hao Jonas Mwasumbi ambaye pia ni mwanahabari mkongwe alisema ujio wa timu ya wanahabari imeleta chachu kimichezo kwenye kata hiyo kwakuwa jamii ya eneo hilo sasa inatambua kuwa wanahabari hawaishii kuandika na kutangaza habari za michezo bali pia wanao uwezo wa kushiriki kwa vitendo.


No comments: