Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, January 16, 2015

UKARABATI WA BARABARA YA IGANZO – KABWE WAZUA KIZUNGUMKUTI.

Sehemu ya barabara inavyoonekana kabla ya kuanza kujaziwa vifusi vya mawe juu yake.

Gari la Wachina likiendelea kumwaga kifusi barabarani.

Pamoja na ukarabati kuendelea lakini usafirishaji wa abiria kwa njia ya Pikipiki ya Matairi matatu(Bajaji) haukusimama.

Katapila la Wachina likiendelea kusawazisha vifusi katika barabara hiyo

Baadhi ya Wakazi wa Isanga wakishangaa hatua za ujenzi huo.


Katapila likiendelea kusawazisha vifusi vya mawe juu ya barabara ya Lami.

Baadhi ya magari yakiendelea kupita huku barabara ikikarabatiwa kutokana na kutoweka alama yoyote kuonesha kama kuna ujenzi unaendelea.


Mmoja wa viongozi wa Kampuni ya CCCC inayojenga barabara ya Mbeya Lwanjiro akisimamia Magari na mitambo iliyoazimwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Bajaji ikiwa imenasa katikati ya Kifusi cha mawe yaliyomwagwa katika barabara ya Lami yenye mashimo.



 picha na Mbeya yetu.

UKARABATI wa Barabara ya Lami iliyochimbika inayotoka Iganzo kuelekea Kabwe jijini Mbeya umezua maswali mengi kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na hatua zinazofanywa.



Baadhi  ya Wakazi  hao wamelalamikia kitendo cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya kukarabati barabara hiyo iliyochoka lami yake kwa kujaza vifusi vya mawe juu yake pasipo kutindua ile ya awali.



Ukarabati wa barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya Kilomita moja ulianza jana majira ya asubuhi ambapo Mkandarasi wa barabara hiyo hakujulikana mara moja licha ya magari na mitambo ya Mkandarasi wa Kampuni ya CCCC inayojenga barabara ya Mbeya – Lwanjiro kutumika katika ujenzi huo.



Kwa mujibu wa wakazi hao walisema kitendo cha Halmashauri ya Jiji kumwaga vifusi juu ya lami iliyochoka ni kufuja fedha za walipa kodi kutokana na vifusi hivyo kuwa na uwezekano wa kusombwa na maji katika kipindi hiki ambacho Mkoa wa Mbeya unamvua kubwa.



Wakazi hao waliongeza kuwa kawaida kunakuwa na vibao vinavyoonesha Mkandarasi wa barabara pamoja na Mkandarasi mshauri lakini vitu hivyo havijawekwa huku ikionekana magari maitambo ya wachina kukodiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya likilazimika kujaza mafuta katika mitambo hiyo.



Hata hivyo mmoja wa Mafundi wa Kampuni ya CCCC ambaye hakutaka jina lake kuandikwa alisema ukarabati wa barabara kwa muda mfupi kuna hatua ambazo zinapaswa kufuatwa wakati ujenzi mkubwa unasubiriwa ili barabara iweze kudumu kwa kipindi Fulani.



Fundi huyo alizitaja hatua hizo kuwa ni kutindua lami ya awali kasha kumwaga udongo wa chini(Sir base) kasha anafuata kumwaga kokoto(stone base) kasha anamalizia na Lami laini ambayo inaweza kudumu kwa miaka mitano wakati uongozi ukijipanga kutafuta fedha za kufumua barabara na kuijenga upya.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Musa Zungiza, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuwafafanulia wananchi juu ya malalamiko hayo lakini simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa jambo lililolazimu kutafutwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya miundombinu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Sheikh Dormohamed Issa.



Mwenyekiti huyo alisema hana taarifa kuhusu kuanza kwa ukarabati barabarani jambo alilosema kilichokuwa kikisubiriwa ni upatikanaji wa fedha na kuahidi kulifanyia kazi kwa kumtafuta Injinia wa Jiji la Mbeya ili kujiridhisha na hatua hizo.



Sheikh Issa aliongeza kuwa pamoja na ukarabati kuendelea lakini hakuna watakachokuwa wamekifanya endapo hawatatindua lami za zamani kwani vifusi hivyo vitaweza kusombwa na maji kutokana na  mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa.



Mwisho. 
Na Mbeya yetu

1 comment:

Anonymous said...

Kwa kweli hata mie nisiyejua ujenzi wa barabara naona hapa wamechemsha kabisa. Utajengaje nyumba bila msingi? huku ni kushindwa kazi kwa wawekezaji wa nje. Mbona hata wawekezaji wa ndani wasingefanya hilo. Lo! aibu sana sana hata kwa nchi majirani wakiona hili Mbeya!!!!!Magufuli kaona hili kweli!!!