Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, January 15, 2015

WAKULIMA MBARALI KUWEZESHWA KWA NJIA YA MASHAMBA DARASA.

Afisa kilimo Mazao Wilaya ya Mbarali, Geophrey Mwamengo(mwenye kofia) akipima shamba kwa ajili ya kupandikiza mpunga katika kilimo cha aina ya Shadidi kwenye Skimu ya Ipatagwa.

Bwanashamba wa Kata ya Mahongole wilaya ya Mbarali, Fredy Amir, akimpa maelekezo mkulima jinsi ya kusawazisha shamba la mpunga kabla ya kupandikiza.

Bibi Shamba wa Kijiji cha Ilaji, Hawa Magota,akiandaa kamba yenye vipimo kwa ajili ya kutumia wakulima wakati wa kupandikiza mpunga.
Wakulima wakiandaa shamba darasa tayari kwa kupandikiza mpunga.

Wakulima wakiendelea kupandikiza mpunga katika shamba darasa ambalo litakuwa mfano juu ya kuandaa kilimo shadidi.



WAKULIMA wa Mpunga  Wilayani  Mbarali wametakiwa kujiunga na vikundi ili wawezeshwe na kupewa elimu ya uzalishaji wa mpunga kupitia mashamba darasa.

Imeelezwa kuwa pia Halmashauri hiyo imejipanga  kuimarisha mashamba darasa kwa ajili ya kufundishia wakulima wa kilimo cha mpunga ili kuongeza uzalishaji.

Hayo yalibainishwa  na Afisa Kilimo Mazao wa Wilaya ya Mbarali, Geophrey Mwamengo, wakati wa zoezi la kupandikiza Mpunga katika shamba darasa lililopo kwenye Skimu ya Umwagiliaji ya Ipatagwa wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya.

Mwamengo alisema Halmashauri imebaini ongezeko la uzalishaji wa Mkulima mmoja mmoja baada ya kutoka na teknolojia sahihi  katika mashamba darasa hali iliyopelekea kuongeza nguvu katika kuboresha mashamba darasa katika Wilaya hiyo.

Alisema uzalishaji wa mpunga katika mashamba ya kawaida kwa Wilaya ya Mbarali msimu wa mwaka 2013/2014 ilikuwa ni wastani wa Tani 4.5  kwa hekta ili hali uzalishaji wa vikundi katika Mashamba darasa yalikuwa Tani 10 kwa Hekta na kuongeza kuwa hadi sasa kuna mashamba darasa 19.

Aliongeza kuwa baadhi ya wakulima wakitoka kwenye mashamba darasa na kila mtu kujilimia Shamba lake mavuno huongezeka mara mbili zaidi ambapo katika msimu wa mwaka 2013/2014 pato la mkulima binafsi lilikuwa ni Tani 15 kwa Hekta.

Afisa huyo alisema kutokana na hali Halmashauri imejipanga kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, ushirika na umoja wa wakulima wanaotumia maji na  kuboresha matumizi ya zana bora za kilimo.

Kwa upande wake Bwana Shamba wa Kata ya Mahongole, Fredy Amir, alisema matokeo ya mashamba darasa ni mazuri kutokana na hali za wakulima kubadilika kiuchumi ambapo asilimia kubwa wanamiliki vyombo vya usafiri pamoja na kujenga nyumba nzuri.

Alisema hivi sasa wamejikita zaidi katika kuwahamasisha Wakulima kuendesha kilimo Shadidi kutokana na kilimo hicho kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha mvua kuwa chache hivyo kutoa hofu kwa wakulima.

Alisema kilimo hicho hakitumii maji mengi hivyo huchangia kupunguza migogoro ya maji katika jamii kwa ujumla kwa kuwa aina hiyo ya kilimo huhitaji maji machache ambapo baada ya wakulima kupewa elimu husaidiana kupunguziana maji mashambani.

Naye Bwana Shamba kutoka Ofisi za Umwagiliaji Kanda ya Mbeya(PHRD), Talibo, ambao ndiyo wafadhili wa Mashamba darasa hayo alisema kama Ofisi  husaidia kuwahamasisha wakulima kili,mo Shadidi kutokana na kutumia maji machache.

Alisema Ofisi ya umwagiliaji huvisaidia vikundi kupitia mashamba darasa kwa kuwapatia mahitaji yote muhimu yanayohitajika wakati wa kuandaa shamba hadi mavuno ambapo baada ya kuvuna mazao hubaki kwenye kikundi.

Aliyataja baadhi ya mahitaji kuwa ni pamoja na mbegu za kupanda, mbolea za kupandia, mbolea za kukuzua, dawa za kuulia wadudu na mashine za kutumia wakati wa palizi.

Mwisho.
Na Mbeya yetu



1 comment:

Anonymous said...

Ni vema sana kwa wakulima kupata elimu ya upandaji mpunga. Lakini afya ni ya muhimu. Angalia akina mama hao hawana boots kiasi kwamba wataathiri afya zao jamani. Watoe na elimu ya afya ya kujikinga na vijidudu miguuni na mikononi wanapofanya kazi sehemu zenye maji kama hapo.