Add caption
KANISA la Moravian Jimbo la Kusini
Magharibi limeendesha ibada maalumu ya kuliombea kanisa hilo kutokana na vurugu
zinazoendelea zikiwemo kufunga ofisi kuu za Jimbo kwa makufuli na minyororo na
baadhi ya wachungaji na wakristo Julai 15, mwaka huu.
Awali kabla ya kuanza kwa ibada na
mkutano wachungaji hao walifanya maombi maalumu na kukemea katika maeneo
yaliyokuwa yameguswa zikiwemo ofisi za Askofu, Lango la kuingilia pamoja na
Geti kuu.
Ibada hiyo iliyofanyika jana katika
Kanisa kuu la Jimbo hilo lililopo Jakaranda jijini Mbeya iliyoongozwa na
Mchungaji Amos Mwampamba na kuhudhuriwa na wachungaji wa Kanisa hilo zaidi ya
100 ilienda sambamba na tamko la kulaani vitendo hivyo.
Akisoma tamko mbele ya wachungaji na
waumini kwa niaba ya Wachungaji wa Jimbo, Mchungaji Watson Mwashambwa, alisema
kitendo kilichofanywa na wachungaji hao ni kinyume cha utaratibu wa kanisa pia
ni matakwa yao binafsi na sio mawazo ya waumini na wachungaji wote.
Alisema kitendo cha waumini wakiongozwa
na Mchungaji wa Usharika wa Bethlehemu Edward Chilale kufunga ofisi za jimbo
kwa lengo la kumshinikiza Askofu Alinikisa Cheyo ni kutokana na Askofu kuwaonya
mara kwa mara kwa vitendo vyao kinyume na kanisa.
Alisema baada ya kuonekana Askofu
anawafuatilia sana wakaamua kumuundia zengwe wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jimbo
Mchungaji Nosigwe Buya la kutaka ajiuzulu wadhfa wake.
Hata hivyo Wachungaji hao wameitaka
Serikali kutoingilia masuala ya Kanisa kwa madai kuwa wanashinikiza kufanya
maamuzi kinyume cha katiba na nje ya vikao halali.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya
kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mbeya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya Norman Sigalla wakitaka Kanisa hilo kumaliza mgogoro kwa kuitisha mkutano
wa Sinodi haraka iwezekanavyo na kumrudisha mwenyekiti madarakani.
Kutokana na kauli hiyo Kanisa hilo
limetoa msimamo wa kuendelea kumsimamisha Mwenyekiti wake Nosigwe Buya hadi
mwaka 2016 itakapoitishwa Sinodi kwa mujibu wa katiba na kwamba kusimamishwa
kwa Mwenyekiti ni kwa mujibu wa Ibara ya 11(2) ya kazi ya Halmashauri kuu xxvi.
Walisema kitendo cha Kamati ya Ulinzi na
usalama ya Wilaya cha kuwaita baadhi ya waumini na kuwakutanisha na Halmashauri
kuu kwenye kikao cha usuluhishi ni kuidharau Halmashauri na kupuuza
mamlaka yake kikatiba.
Aidha ibada hiyo ambayo ilikuwa na
mkutano ndani yake ni muendelezo wa mgogoro unaofurukuta ndani ya Kanisa hilo
Jimbo la Kusini Magharibi unaotokana na kugawanyika kwa wachungaji na waumini
kuwa katika pande mbili.
Katika mgogoro huo wapo waumini na
baadhi ya wachungaji wanaoshinikiza Askofu Alinikisa Cheyo kujiuzulu na
kurudishwa madarakani kwa Mwenyekiti Nosigwe Buya huku kundi lingine likiunga
mkono kusimamishwa kwa Mwenyekiti na Askofu kuendelea kuwa madarakani.
Hata hivyo uchunguzi wa Mbeya yetu umebaini kuwa katika ibada hiyo wachungaji waliohuduria niwa upande
unaomuunga mkono Askofu Alinikisa Cheyo hali iliyopelekea kutoa matamko ya
kukilaani kikundi kinachomuunga mkono Mwenyekiti na kusisitiza kuondolewa
madarakani.
Mwisho.
|
No comments:
Post a Comment