ZAIDI ya Shilingi Bilioni 2.3
zinahitajika kwa ajili ya kurudisha miundombinu ya barabara za Halmashauri ya
Wilaya ya Kyela baada ya kuharibiwa vibaya na mafuriko yaliyoikumba Wilaya hiyo
hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya
Kyela, Magreth Ester Malenga, alipokuwa akitoa tathmini ya athari zilizotokana
na mafuriko wakati akipokea msaada wa vitu mbali mbali kutoka Benki ya NMB
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Malenga alisema miundombinu ya barabara
katika kuvifikia vijiji ni mibaya na haipitiki kabisa hali inayosababisha
baadhi ya waathirika wa mafuriko kutofikiwa kwa wakati hivyo ili iweze kurudi
katika hali yake ya kawaida zinahitajika kiasi hicho cha Shilingi Bilioni 2.3
kwa barabara za Halmashauri pekee.
Alisema katika mafuriko hayo hadi sasa
Watu 7 wamepoteza maisha huku mwili mmoja ukiwa haujapatikana kutokana na
kusombwa na maji na kaya 3983 ndizo zilizokumbwa na athari ya mafuriko hayo.
Aliongeza kuwa kati ya kaya hizo ni kaya
235 zenye wakazi 1080 ndizo zilizoathirika kwa kiasi kikubwa sana ingawa
zimepata misaada mbali mbali kutoka Serikalini, Mashirika binafsi na watu mbali
mbali.
Alisema msaada zaidi unahitajika kwa
ajili ya kuzifikia kaya zingine 2040 ambazo bado hazipatiwa msaada wowote wa
chakula na mahitaji ya kawaida kutokana na miundombinu kuwa mibovu ya kuwafikia
walipo.
Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza kuwa tangu
kutokea kwa maafa hayo Serikali imetoa Tani 6 za Mahindi pamoja na fedha za
kusagia na kununulia maharage kwa ajili ya waathirika huku mwananchi mmoja
mmoja akijitokeza kuchangia alichonacho pamoja na mashirika.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini, Lucresia Makiriye, alisema benki yao imeguswa sana na
maafa yaliyotokea hivyo wameamua kutoa msaada kwa waathirika ili waweze kuishi
kama Watanzania wengine.
Alisema NMB imetoa vitu vya thamani ya
Shilingi Milioni 10 pamoja na kusafirisha hadi wilayani Kyela ambavyo
vitazinufaisha kaya zaidi ya 320 zilizopatwa na majanga ya mafuriko hayo.
Alivitaja vitu hivyo kuwa ni pamoja na
Mchele kilo 3200 ambao utagawiwa kwa kilo kumi kwa kila kaya, Maharage kilo
1600 kila kaya kilo 5 na mafuta ya kupikia Katoni 54 ambapo kila kaya
itapata Lita tatu.
Akishukuru kwa ajili ya msaada huo Mkuu
wa Wilaya ya Kyela, Magreth Malenga alisema hivi sasa hakuna mwananchi
atakayekuwa na shida ya chakula na kwamba atahakikisha walengwa wanafikishiwa
kama ilivyokusudiwa.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment