BABA MZAZI ANAYETUHUMIWA KWA WIZI WA MTOTO
Jeshi la
Polisi linamshikilia Salehe Issah Mwangosi(29) Mkazi wa Tankini Kasumulu Kata
ya Itope Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya kwa tuhuma za wizi wa mtoto jinsi ya
kiume mwenye umri wa siku sita.
Imedaiwa
kutenda kosa hilo dhidi ya mzazi mwenzake aliyefahamika kwa jina la Mboka
Mwakikagile(21)mkazi wa Kitongoji cha Sama A Kijiji cha Ibanda Kata ya Itope
Jumapili April 6 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi kwa kushirikiana na
mwanamke mmoja ambaye hajafahamika jina mara moja aliyejifanya ni mama yake
mkubwa wa mtuhumiwa.
Mipango hiyo
iliyoanza kuandaliwa na mtuhumiwa siku tatu baada ya mtoto kuzaliwa kwa kutumia
simu ya kiganjani ya mtuhumiwa yenye namba 0767356222 na mzazi wa mtoto kwa
namba 0757006839 ambapo siku ya tukio Salehe alimwambia kuwa mama yake mkubwa
angekwenda kumjulia hali mtoto aliyezaliwa.
Baada ya
Salehe kuwasiliana na mzazi mwenzake walikubaliana Mama yake mkubwa angekwenda
Jumapili Aprili 6 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi ambapo mwanamke huyo
alifika nyumbani kwa Mboka(Mzazi wa mtoto)ambapo aliwakuta wazazi wake akiwemo
Mzee Lupalo Elija Mwakikagile(90) na mkewe Nelly Kyusa(49) ambao walimpokea.
Mwanamke
huyo alifikanyumbani kwa Mwakikagile akiwa ameshika mkoba wenye nguo za mtoto
mchanga,sabuni na mahitaji mengine ambapo alijieleza kuwa yeye ni afisa wa
Mamlaka ya mapato na Mama mkubwa wa Salehe hivyo amekuja kwa ajili ya kumjulia
hali na kumpa pole Mboka kwa kujifungua.
Mama huyo
baada ya kumwangalia Mtoto alidai ana matatizo ya macho hivyo waende naye
Zahanati ya Njisi Kasumulu kwa ajili ya matibabu ambapo walipakizana kwenye
pikipiki na kufika huko Zahanati na kumkuta Daktari ambaye alimtaka mzazi
kununua Daftari ya matibabu kwa kuwa kadi ya kliniki hutolewa mwezi mmoja tangu
kuzaliwa kwa mtoto.
Ndipo Mboka
alikwenda Dukani umbali wa mita 500 kwa ajili ya kununua daftari akimwacha
mwanamke huyo akiwa amembeba mtoto na aliporejea hakumkuta mwanamke huyo wa
mtoto na hata aliposubiri kwa muda alimuuliza Salehe kupitia simu ya Daktari
ambapo Salehe alisema asiwe na shaka mama huyo atamleta mtoto.
Mboka aliamua
kutoa taarifa Polisi Kasumulu kwa ajili ya kuibiwa mtoto lakini alishangaa
kumkuta Salehe Polisi naye akitoa taarifa juu ya kupotea kwa mtoto hali
inayoonesha kulikuwa na njama kwani yeye ndiye alikuwa akifanya mawasiliano na
mwanamke huyo na yeye ndiye aliyesema kuwa atakuja nyumbani kumwangalia.
Hata hivyo
uchunguzi umebaini kuwa mwanake aliyedaiwa kuiba mtoto huyo alisajili upya
namba ya simu badala ya awali kwa kutumia leseni yake ya udereva huku ikionesha
kuwa amezaliwa April 24 mwaka 1986 na mara kadhaa alijitambulisha kama Afisa wa
mamlaka ya mapato na wakati mwingine akijifanya Muuguzi.
Kwa upande
wake ndugu wa mtuhumiwa akiwemo Baba mdogo aitwaye Assah Mwangosi(49)wamesema
kuwa hawaelewi lolote kuhusiana na tukio hilo na kuwa hawakuwa na taarifa za
kijana wao kuzaa nje ya ndoa kwani
Salehe ana mkewe aitwaye Falesy Sanderson(29) aliyemuoa mwaka 2006 alipokuwa
akifanya biashara wilaya ya Karonga nchi jirani ya Malawi.
Ndugu
wamedai Salehe anamiliki pikipiki mbili zenye namba za usajili T640 CHA na T 796 BKG ambazo huzitumia
kwa ajili ya kubeba abiria maarufu kama bodaboda eneo la Kasumulu na
inasadikiwa moja ya pikipiki kutumika kuiba mtoto.
Kwa upande
wa Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba bado wanamshikilia Salehe kwa
mahojiano na wanafanya juhudi za kumtafuta mtoto na kutoa wito kwa mwenye
taarifa za mtoto huyo atoe Polisi na mtuhumiwa aweze kukamatwa.
Na Ezekiel Kamanga Mbeya yetu |
No comments:
Post a Comment