Add caption
MKUU wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
amelitaka Jeshi la Polisi kujifunza mbinu mbali mbali za kukabiliana na
majambazi kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo katika jamii na kuhatarisha
usalama wa raia.
Aidha aliwataka Wananchi kutoa
ushirikiano kwa jeshi la Polisi na Vyombo vya ulinzi ili kudumisha amani na
utulivu kwa kushiriki kutoa taarifa za uhalifu pamoja na ulinzi shirikishi kwa
kutii sheria bila shuruti.
Kandoro alitoa kauli hiyo alipotembelea mazoezi ya Askari wa Kutuliza ghasia(FFU) mkoani hapa katika
viwanja vyao mazoezi yenye lengo la kudumisha nidhamu, ukakamavu na utayari wa
kukabiliana na adui kwa Askari wa Jeshi la Polisi.
Alisema jeshi la Polisi pekee haliwezi
kudumisha hali ya amani na utulivu kwa Watanzania bila kupata ushirikiano
kutoka kwao kwa kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwepo kwa hali ya hatari ama
uhalifu katika maeneo yao.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi
linatakiwa kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya utii wa sheria bila
shuruti pamoja na ulinzi shirikishi jambo litakalosaidia kupunguza vurugu
zisizokuwa na msingi katika jamii.
Alisema pia wananchi hawapaswi
kulazimisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa katika kukabiliana nao kutokana
na kushindwa kutii amri zinazotolewa na kukatazwa jambo bali watumie njia ya
mazungumzo wanapokuwa na madai na siyo kukimbilia kufunga barabara na kuchoma
moto.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema utaratibu wa kufanya mazoezi kwa askari wa
kupambana na kutuliza ghasia hufanyika mara mbili kwa wiki ikiwa na lengo la
kuangalia hali ya nidhamu, ukakamavi na utayari wa Askari katika kupambana na
uhalifu.
Katika mazoezi hayo Askari waliweza
kumuonesha Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Mkoa
mbinu mbali mbali za kukabiliana na maadui ikiwa ni pamoja na kudhibiti vurugu
kwa kutumia mbinu mbali mbali, kukabiliana na majambazi wenye silaha
pamoja na mbinu za kivita.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment