SERIKALI imetakiwa kutoa mitaala ya
elimu kuhusu hali ya hewa katika shule za Sekondari nchini ili kukabiliana na
ongezeko la joto na mabadiliko ya tabia ya nchi katika karne zijazo.
wito huo ulitolewa na Meneja wa
Kanda ya Nyanda za juu kusini magharibi wa Mamlaka ya hali ya hewa, Ahmed Issa,
alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya sekondari Wenda walipotembelea
kituo hicho katika kuadhimisha siku ya hali ya hewa duniani.
Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo
ni mabadiliko ya hali ya hewa na vijana hivyo ni muhimu kwa Serikali kuandaa
mitaala ya elimu kuhusiana na hali ya hewa ili kuwafanya vijana waelewe njia
mbali mbali za kukabiliana na ongezeko hilo kwa miaka ya baadaye kwa kuwa ndiyo
watakaokuwepo.
“ Vijana ndiyo watakaokuwepo na kuishi
katika karne zijazo, hivyo ni bora tukajikita katika kuwaelimisha wao kwa
serikali kuandaa mitaala ya masomo wakiwa mashuleni namna ya kuendana na
mabadiliko yanayotokea” alisema meneja huyo.
Aliongeza kuwa tangu mwaka 1850 kumekuwa
na kasi ndogo ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa joto kuongezeka duniani lakini
kadiri muda unavyoozidi kusonga mbele joto linazidi kuongezeka hadi kufikia
asilimia 0.75 hadi asilimia moja na utabiri ukionyesha hali kuwa mbaya zaidi.
Alisema hadi sasa zaidi ya asilimia 60
ya ongezeko la joto duniani husababishwa na hewa mkaa angani ambapo njia kuu ya
kukabiliana na hali hiyo ni pamoja na upandaji wa miti ya asili kuendana na
eneo husika itakayochangia kunyesha kwa mvua yenye manufaa katika jamii.
Meneja huyo alisema hayo yote
yanawezekana kukabiliana nayo ikiwa ni kushirikisha vijana na kuwapa elimu
mapema na kuzingatia umuhimu wa ufuatiliaji wa taarifa zinazotolewa na mamlaka
ya hali ya hewa na jinsi ya kujihami.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment