Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi
MVUA zinazoendelea kunyesha sehemu mbali
mbali hapa nchini zimesababisha madhara katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja
na kusababisha vifo.
Mvua zilizonyesha Machi 30, Mwaka
huu Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya zilisababisha kifo cha mtoto wa miaka
minne baada ya kusombwa na maji ya mto uliojaa wakati akijaribu kuvuka akiwa na
dada yake.
Marehemu alifahamika kwa jina la Vailet
Mwansopo(4) na dada yake aliyenusurika kutokana na maji hayo ni
Neva Mwansopo(6) waliosombwa na maji ya mto Hasano uliopo kitongoji
cha Namalama kijiji cha Mpona Kata ya Totowe Wilayani hapa.
Watoto hao walikutwa na janga hilo
walipokuwa wametoka nyumbani kwao Mpona kwenda kitongoji cha Hazolombo
kinachotenganishwa na mto huo walikotumwa na Mama yao kwenda kumwita Baba yao
mzazi Daimon Mwansopo ambaye anaishi na mke mwingine huko.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa Tukio hilo,
ambao ni Noel Mwazembe na Mlawa Mhamali walisema kuwa walisikia sauti ya kuomba
msaada kwa mtoto Neva ndipo walipokimbilia eneo hilo na kuambiwa kuwa maji yalipomzidi
nguvu aliamua kumwachia mdogo wake naye kufanya juhudi za kujiokoa ndipo
walipofanikiwa kumwokoa Neva kisha kuanza kumfuatilia nduguye.
Walisema baada ya kufuatilia waliukuta
mwili wa marehemu mita mia mbili kutoka eneo la tukio ukiwa umenasa kwenye
mizizi ya miti kando kando ya mto huo ndipo walipouchukua kisha kutoa taarifa
kwa Mtendaji wa kijiji cha Malangali Yaledi Mwanguku.
Walisema Mtendaji huyo alitoa
taarifa kituo cha Polisi Galula pamoja na Daktari ambapo waliufanyia
uchunguzi mwili wa marehemu na kuwabidhi ndugu kwa ajili ya mazishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed
Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wazazi kuwa
waangalifu na watoto ili kuepusha vifo visivyo vya lazima.
Aliongeza kuwa Mvua zinazonyesha
wilayani Chunya zimesababisha madhara makubwa ikiwemo uharibifu wa mazao na
kuwataka wananchi kuwa waangarifu kwa kutozurura ovyo kutokana na mito mingi
kujaa maji.
Mwisho.
|
No comments:
Post a Comment