WAKATI asasi na taasisi mbali mbali
zikiwemo TGNP, TAMWA na WRP zikipinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, hali
hiyo imeonekana kutopewa mwitikio na baadhi ya familia.
Kutopewa kwa kipaumbele na kushindwa
kuwachukulia hatua wanaofanya vitendo hivyo kumetokana na Familia moja
jijini Mbeya kutaka kumaliza kifamilia suala la ubakaji lililotokea hivi
karibuni.
Tukio hilo lilitokea Machi 13 mwaka huu
majira ya saa 11 jioni katika Mtaa wa Mapambano Kata ya Iyela wakati mtoto wa
kike alipotumwa dukani na Mama yake Mzazi na kukumbwa na tukio hilo.
Mtuhumiwa wa tukio hilo ambaye ni
mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Iyela Jijini Mbeya Patrick Ndelwa(18)
anatuhumiwa kumbaka Mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka nane(jina
limehifadhiwa) shule ya Msingi Mapambano Jijini Mbeya.
Hatua ya kufikia wazazi wa pande zote
mbili kutaka kumalizana kifamilia imetokea baada ya Jeshi la Polisi kushindwa
kufungua jalada la tukio hilo tangu Machi 14, mwaka huu
lilipolipotiwa.
Aidha jalada la tukio hilo lilifunguliwa
Machi 24 mwaka huu huku Polisi wakitaka yafanyike mazungumzo katika pande hizo
mbili na kushindwa kuwachukulia hatua waliotenda makosa kama hayo.
Uchunguzi umebaini kufanyika kikao Machi
26,mwaka huu eneo la Mapambano Iyela kilichowakutanisha pande hizo mbili kwa
nia ya kulimaliza nyumbani suala hilo huku upande wa mtuhumiwa ukidai kuwa
aliyetenda kosa hilo ni yatima.
Aidha imebainika kuwepo kwa mkakati wa kumhamisha
mwathirika wa tukio hilo kumpeleka Jijini Dar es Salaam kwa nia ya kupoteza
ushahidi na Jalada kutopelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali ili kukwamisha
taratibu za kumfikisha mtuhumiwa Mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mama Mzazi wa mwathirika wa tukio
hilo,Salome Msigwa alisema aligundua kubakwa kwa mwanae alipoanza kumuogesha
Machi 13 mwaka huu majira ya saa kumi na mbili jioni na alipomuuliza alijibiwa
kuwa aliyembaka ni Patrick Ndelwa ambapo alimtendea unyama huo katika
kichochoro karibu ya nyumba yao.
Alisema baada ya kugundua tatizo la
mtoto, alitoa taarifa kituo cha Polisi ambapo mtuhumiwa alikamatwa na mtoto
kupelekwa kupimwa Hospitali ya Rufaa na kupewa Matibabu huku akitakiwa
kufuatilia vipimo vingine Machi 28.
Baadhi ya wadau wamelalamikia kuongezeka
kwa vitendo ya ukatili dhidi ya watoto na kwamba vimekuwa vikiongezeka Jijini
Mbeya sehemu kubwa imekuwa ikichangiwa na Dawati la Kijinsia la Jeshi la Polisi
kutokana na kugeuka Mahakama kuyamaliza matatizo kwa kupatanisha pande
zinazotuhumiana.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amekiri kupokea tatizo hilo kwamba jeshi lake linafanyia uchunguzi swala hilo likikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment