Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Sunday, March 9, 2014

Mamlaka ya hali ya Hewa kanda ya kusini yapongezwa

Wachungaji na baadhi ya waombolezaji wakiwa katika ibada ya kumsindikiza Pacha wa pili (Anania)aliyefariki dunia kati ya mapacha wanne waliozaliwa na Aida Nakawala mkazi wa Kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya

Msafara wa kuelekea katika makaburi ya kijiji tayari kwa mazishi ya Pacha wa Pili kati ya mapacha wanne aliyefariki kwa ugonjwa wa Nimonia

Mchungaji wa kanisa la Africa Mission Church akiendelea na ibada ya mazishi makaburini tayari kwa safari ya mwisho ya mtoto Anania

Mwili wa Marehemu ukishushwa kaburini

Katikati ni Meneja wa Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za juu kusini, Ahmed Issah pamoja na wafanyakazi wake wakiwa makaburini kumsindikiza marehemu ambapo pia Mamlaka hiyo ndiyo iliyosafirisha mwili wa marehemu kutoka Hospitali ya Wazazi Meta walikokuwa wakipatiwa matibabu.

Meneja wa Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za juu kusini, Ahmed Issah, (wa kwanza kushoto)akisaidia kufukia kaburi la marehemu pia Mamlaka hiyo ndiyo iliyosafirisha mwili  wa marehemu kutoka Hospitali ya Wazazi Meta walikokuwa wakipatiwa matibabu.

Baba wa Marehemu Weston akiwa amekaa kwa unyonge huku akifuatilia mazishi ya mwanae


 Meneja wa Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za juu kusini, Ahmed Issah akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mamlaka ya hali ya hewa kutokana na kuguswa na msiba huo
  Shomi Mtaki ambaye ni mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo kutoka Wilaya za Momba na Mbozi akizungumza jambo kwa niaba ya waandishi wa habari ambapo alisema jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kufunga na kuomba kwa ajili ya maisha yao kutokana na kufanya kazi katika mazingira magumu.

  Shomi Mtaki akitoa rambi rambi yake kwa familia ya marehemu
Haya ni makaburi mawili waliyozikwa mapacha wawili Alinikumbu ( wa kwanza kuzaliwa) na Anania( wa tatu kuzaliwa) waliofariki dunia kwa siku tofauti kutokana na ugonjwa wa Nimonia uliosababishwa na hali ya Maisha duni ya kijijini kwao Chiwanda yanayowakabili wakazi wa huko.




WANANCHI na wakazi wa kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya wametoa Pongezi kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye makao makuu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe(SIA) uliopo Mkoani Mbeya  kwa kufanikisha mazishi ya Mtoto mmoja kati ya mapacha wawili waliofariki dunia kwa ugonjwa wa Nimonia.


Pongezi hizo zimetokana na mamlaka hiyo kujitolea kusafirisha Mwili wa Marehemu kutoka Hospitali ya Wazazi Meta walikokuwa wakipatiwa matibabu hadi Kijijini Kwao Chiwanda Wilayani Momba.


Mbali na usafiri huo pia msafara wa kuelekea kijijini kwa mazishi pia uliongozwa na Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda, Ahmed Issah akiongozana na wafanyakazi watatu.


Akizungumza kwa niaba ya familia Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mpumpi katika kijiji cha Chiwanda,Winston Mtali alisema ni heshima kubwa iliyooneshwa na meneja huyo kwa kuthamini msiba wa mtoto mdogo na kujitolea kugharamia usafiri na shughuli zote kwa ujumla.


Alisema mara nyingi shughuli za misiba kama hiyo huratibiwa na wananchi kwa ushirikiano na serikali ya kijiji lakini katika mazishi ya Mapacha hao hali imekuwa tofauti kutokana na uwepo wa misaada kutoka kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda ya Nyanda za juu kusini.


Aliongeza kuwa viongozi wote wanapaswa kuonesha moyo wa kujitoa kwa watu wa hali ya chini kama alivyofanya Meneja huyo pamoja na wafanyakazi wake kwa kuamua kutoa usafiri na kushuhudia mazishi.


Kwa upande wake Meneja huyo, Ahmed Issah alisema anayepaswa kushukuriwa zaidi ni vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikitoa taarifa za mara kwa mara zinazohusiana na watoto hao tangu kuzaliwa hadi sasa na hawakuweza kukata tama.


Alisema hata watu wanaotoa misaada ni kutokana na kupata taarifa zenye uhakika kutoka kwa waandishi wa habari ambazo zimesaidia watu wengi kujua hususani wanaoishi nchi za nje.


Alisema hivi sasa watu hawahangaiki  upataji wa taarifa juu ya jambo lolote isipokuwa kwa kuingia katika mtandao wa Mbeya yetu Blog ambako hupata kila tukio linapotokea kwa uhakika zaidi.

Akishukuru kwa niaba ya Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mazishi ya mtoto huyo,  Shomi Mtaki ambaye ni mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo kutoka Wilaya za Momba na Mbozi alisema jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kufunga na kuomba kwa ajili ya maisha yao kutokana na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Na Mbeya yetu

No comments: