SAKATA la Wafanyabiashara kufunga maduka
yao wakigomea Mashine za kielektroniki za kutolea Stakabadhi zilizopendekezwa
na Serikali maarufu kwa jina la EFDs limezidi kushika kasi baada ya
wafanyabiashara ya Wilaya ya Kyela na Soko la Sido Jijini Mbeya nao kufunga
biashara zao.
Zoezi la wafanyabiashara hao kufunga
maduka hayo lilianza juzi na jana katika Wilaya ya Kyela na Jiji la Mbeya ikiwa
ni muda mfupi baada ya Polisi kulazimika kutumia Mabomu ya machozi kuwatuliza
wafanyabiashara wa Soko la Mwanjelwa walipogomea mashine hizo Mwishoni mwa
mwaka jana.
Hata hivyo baadhi ya Wafanyabiashara
wamesema wao wanachogomea ni bei za Mashine hizo kuwa ni kubwa na haziendani na
mitaji ya biashara zao ambapo waliitaka Serikali ama kupunguza bei hizo ambazo
wanalazimishwa kununua kwa shilingi Laki saba hadi Laki nane au kuwakopesha ili
wawakate kwenye kodi humo humo.
Walisema suala la mashine hizo
linaonekana kama ni miradi ya watu wachache hali inayowayumbisha
wafanyabiashara na kuwanyika haki yao ya msingi ingawa wanatambua umuhimu wa
kulipa kodi kwa maendeleo ya Nchi lakini siyo kwa kuwalazimisha kununua kwa bei
kubwa.
Aidha walisema ni vema TRA wakatumia
mashine hizo kama ilivyo Idara za Maji na Tanesco wanapomfungia mteja wake Mita
inakuwa bado ni mali ya Shirika hivyo na wao wangezigawa bure kwa
Wafanyabiashara ili waendelee kukusanya ushuru na siyo kuwalazimisha kuwauzia
kitu ambacho hawana faida nacho.
Hata hivyo zoezi hilo la kufunga maduka
limeonekana kuwa na athari kubwa kutokana na baadhi ya Wafanyabiashara wadogo
wasiostahili kuwa na mashine hizo kulazimishwa kufunga maduka yao na
wafanyabiashara wakubwa wanaogomea hali inayowaathiri na wao.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment