WATANZANIA wametakiwa kuwa makini na
kutofautisha shughuli za waganga wa jadi, waganga wa tiba asili na waganga wa
kienyeji zinazopotosha jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi
karibuni Mratibu wa Chama cha Watabibu wa Dawa Asili Tanzania (ATME) Mkoa wa
Mbeya,Boniventura Mwalongo, alisema baadhi ya watu hutumia majina wa waganga
kufanya uhalifu tofauti na matakwa ya watanzania.
Alisema baadhi ya matendo kama biashara
haramu ya viungo vya binadamu na mauaji ya Albino, Vikongwe, upigaji nondo,
utoaji utajirisho, fedha za majini, kuunganisha watu na freemason, rambaramba,
kuzuza na kuruka na ungo siyo sehemu ya shughuli za tiba asili.
Alisema tiba asili inatambuliwa kwa
mujibu wa sheria namba 23 ya mwaka 2002, hivyo waganga wa kienyeji wanatumia
utapeli kuwarubuni wananchi kwa kuigiza kama matabibu wa tiba asili.
Alisema Watabibu wa tiba asili Mkoa wa
Mbeya wanatoa wito kwa taasisi zinazojihusisha na tiba asili kutojitambulisha
kama waganga wa tiba asili na badala yake wajitambulishe kama watabibu wa tiba
asili.
Alisema utambulisho wa mganga wa tiba
asili unatumika vibaya na baadhi ya madui wa tiba asili na kupelekea wananchi
kuelewa na kuwatambua kama Waganga wa jadi, waganga wa tiba asili na waganga wa
kienyeji kama wamoja ambapo wanatofautiana kwa matendo na ueledi wao pamoja na
sifa na ujuzi wao.
Mratibu huyo aliongeza kuwa ni wakati wa
Watatibu wa Tiba asili kote nchini kusajiliwa kwa mujibu wa sheria ili
kuwakomesha na kukemea kwa nguvu wanaowahujumu kwa kujihusisha na vitendo vya
ushirikina na mambo yanayoipotosha jamii.
Alisema kila mtabibu anapaswa kuwa
mlinzi wa maadili ya taaluma yake kwa mujibu wa sera, sheria kanuni na miongozo
iliyopo.
Aidha alitoa wito kwa Vyombo vya Dola
kuwafungulia milango ya ushirikiano ili kukabiliana na vitendo vya kidhalimu
vinavyoihusisha tiba asili ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza
kutokana na matumizi mabaya ya taaluma ya tiba asili.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa
unalengo la kulaani vitendo vya kinyama na kikatili vinavyokiuka sheria za nchi
vinavyofanywa na waganga wa kienyeji kama ilivyotokea Mkoani Mwanza Oktoba 28
Mwaka huu kwa Waganga wawili wa Kienyeji na mkulima mmoja kukamatwa wakiwa na
kuingo cha binadamu wakitaka kukiuza kwa shilingi milioni moja.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment