KATIKA utekelezaji wa miradi ya
maendeleo kwa mwaka wa Fedha wa 2012/2013, Mkoa wa Mbeya umeshindwa kukidhi
mahitaji kutokana na kukabiliana na changamoto mbali mbali ikiwemo
ucheleweshaji wa fedha kutoka Hazina.
Hayo yalibainishwa katika Kikao cha
Ushauri cha Mkoa wa Mbeya (RCC) kilichofanyika hivi karibuni`katika ukumbi wa
Mikutano wa Mkapa uliopo Sokomatola Jijini hapa na kuongozwa na Mwenyekiti wake
ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro.
Awali akifungua Mkutano huo Kandoro
alisema lengo na madhumuni ya kikao hicho ni kujadili bajeti ya Mkoa kwa mwaka
wa fedha 2012/2013 na Mwaka wa fedha 2013/ 2014 sambamba na kuangalia utekelezaji
wake na changamoto zilizojitokeza katika ukamilishaji wa miradi kwa kila
Halmashauri.
Kandoro alisema Licha ya bajeti
kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 236 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 hadi
shilingi Bilioni 277.5 kwa mwaka wa fedha 2013/2014 bado changamoto kubwa ni
ubora wa kazi zinazofanywa na kusimamiwa na Halmashauri kutoridhisha
kulingana na viwango vya fedha wanazotengewa.
Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni
hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali kuendelea kujirudia kila mwaka hali inayoashiria
Halmashauri kutokuwa makini na suala la matumizi sahihi ya fedha zinazotokana
na kodi za wananchi kwa kuzitumia tofauti na malengo na muda unaokuwa
umepangwa.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa
utekelezaji wa miradi mwaka uliopita umeshindwa kufikia malengo kutokana na
Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuendelea kuwa tegemezi katika bajeti zake
kwa asilimia 95 ambapo Halmashauri zinaweza kujitegemea kwa asilimia tano
pekee.
Alisema jambo la kutegemea ruzuku kutoka
Serikalini siyo jambo la kufurahia hivyo kila Halmashauri ihakikishe inasimamia
sheria ndogo zilizotungwa zinazohusu ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuepuka
kuwa wategemezi kwa kiwango kikubwa kama kilichopo kwa sasa ndani ya
Halmashauri za Mkoa wa Mbeya.
Mbali na hilo Kandoro aliagiza Viongozi
wa Halmashauri kuwa karibu na wananchi kwa kuwashirikisha katika kazi za
maendeleo ili kurudisha moyo wa uchangiaji na kupenda kujitolea kwa ajili ya
maendeleo ya Mkoa wa Mbeya na nchi kwa ujumla hali ambayo itasaidia kusukuma
ukusanyaji wa mapato.
Aidha akisoma taarifa ya utekelezaji kwa
mwaka uliopita Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja ambaye pia ni
katibu wa kikao hicho alisema changamoto zilizojitokeza ni pamoja na kuchelewa
kutolewa kwa fedha za maendeleo na wakati mwingine kutolewa kidogo kidogo hali
hiyo mhusababisha kuchelewa kuanza kutekeleza kwa baadhi ya miradi husika.
Aliongeza kuwa kutokuwa na majengo bora
ya ofisi na nyumba za viongozi kwa wilaya mpya kama vile Halmashauri ya Wilaya
ya Momba na Busokelo zilizoanzishwa mapema mwaka huu na hivyo kutokuwa na
miundombinu inayojitosheleza.
Alisema kuwepo kwa matumizi makubwa ya
mafuta kwa ajili ya mapokezi na ziara za viongozi wa kitaifa , Wizara na
washirika wa maendeleo wanapotembelea Mkoa na Wilaya na kuongezeka kwa gharama
za usimamizi kutokana na kuongezeka kwa Halmashauri na Wilaya.
Mtunguja alisema changamoto nyingine ni
uhaba wa vifaa muhimu vya ujenzi wa barabara katika Halmashauri na gharama
kubwa za stahili za uhamisho na ajira mpya kwa watumishi wapya ndani ya taasisi
za Serikali.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment