HALMASHAURI ya Busokelo Wilaya ya Rungwe
Mkoani Mbeya imeanza kutekeleza kwa vitendo miradi iliyozinduliwa na mbio za
mwenge wa uhuru uliomaliza mbio zake Oktoba 14, Mwaka huu nchi nzima.
Katika mbio za mwenge katika Halmashauri
ya Busokelo ilitolewa mizinga ya nyuki 60 kwa vikundi 6 yenye thamani ya
shilingi Milinoni 2.7 ambapo kila kikundi kilipatiwa mizinga 10 tayari kwa
ufugaji wa nyuki.
Kutokana na vikundi hivyo kukabidhiwa
mradi huo wa ufugaji nyuki Halmashauri iliandaa mafunzo ya siku tatu kwa wenye
viti na makatibu wa vikundi 8 pamoja na mafundi seremala kwa ajili ya kupatiwa
mafunzo namna ya ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa inayochangia uhifadhi wa
mazingira.
Msimamizi wa mafunzo hayo, Anamary
Joseph ambaye ni afisa mazingira wa Halmashauri ya Busokelo alisema kupitia
mafunzo hayo yatasaidia kuhamasisha wananchi kuacha kufuga nyuki kienyeji jambo
ambalo huchangia kuharibu mazingira kutokana na njia wanayotumia wakati wa
kuvuna.
Alisema ufugaji wa nyuki kwa njia za
kienyeji huharibu mazingira kwa sababu wanapovuna hulazimika kuchoma moto ili
nyuki waweze kukimbia na wao kuvuna kirahisi lakini hali hiyo huchangia kuchoma
moto misitu na pia mazao yanayovunwa kuhosa ubora na kiwango ambacho
kitamkomboa mkulima.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya
katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kijiji cha Lufilyo
Busokelo Wilayani Rungwe, Mwenyekiti wa Halmashauri Meshack Mwakipunga alisema
wameamua kuwajumuisha mafundi seremala katika mafunzo hayo ili mizinga iwe
inatengenezwa jirani na wananchi na kwa gharama nafuu.
Alisema mazingira ya busokelo yanaruhusu
ufugaji wa nyuki hivyo wananchi wakihamasishwa pia itasaidia kuongeza vipato
vyao kupitia mazao ya kilimo ambayo yatasaidiwa na nyuki kufanya uchavushaji
wakati wakijitafutia chakula.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispin Meela alisema ni vema vikundi vilivyopewa
mafunzo vikasimamiwa ili matunda yaonekane na iwe fundisho kwa wengine ambao
hgawataki kujiunga na vikundi.
Alisema uchumi wa mtanzania unatokana na
juhudi za mtu binafsi kupitia vikundi ambapo kupitia vikundi ni rahisi Serikali
kuvisaidia kama ilivyofanya kwa kuwapa mizinga ya nyiki ambapo mradi huo hauna
gharama yoyote ambayo kikundi kitapaswa kugharamia wakati wa kuendesha miradi
hiyo.
Alisema Nyuki hawana gharama yoyote
ambapo wakishawekewa mizinga huingia wenyewe na kuanza kutoa asali jambo ambalo
mfugaji atatakiwa kuanza kuvuna na kuuza asali ambayo itakuwa imevunwa kwa
kufuata taratibu za kitalaamu.
“ mnajua hawa nyuki hawana gharama
zozote ambazo kikundi kitapaswa kugharamia kwa sababu nyuki hawaugui kwamba
watatakiwa kupatiwa chanjo, hawali pumba, hawahitaji kuletewa maji bali
huyafuata popote yalipo na wala hawataki pembejeo kutoka serikalini hivyo
changamkieni fursa hiii.” Alisema Mkuu wa Wilaya.
Aliongeza kuwa ili kudhibiti uharibifu
wa mazingira na kujenga mazingira rafiki kwa ufugaji wa nyuki ni vema wanaofuga
nyuki kienyeji wakadhibitiwa kwa kuwa ndiyo wanaochoma mazingira hivyo
Halmashauri iwadhibiti kupitia kanuni za vijiji na vitongoji kwa kuwaondoa
kabisa misituni.
Mafunzo hayo yatolewa na wataalamu
wawili kutoka kampuni ya National Beekeeping Supplies kutoka Mkoani Dodoma
mafunzo ambayo yaliyofanyika kwa siku tatu ambapo wamefundishwa namna ya
uvunaji na ufungaji kwa kuzingatia mahitaji ya soko la kimataifa.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment