ILI kukabiliana na wimbi la
uhalifu na wizi wa mali za watu, Makampuni binafsi ya sekta ya ulinzi
yameagizwa kuajiri wafanyakazi waliopitia mafunzo ya mgambo ili kukabiliana na
wahalifu katika maeneo yao ya kazi.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya
ya Rungwe, Crispin Meela alipokuwa akifunga mafunzo ya Mgambo hatua ya kwanza
yaliyomalizika hivi karibuni katika uwanja wa shule ya Sekondari Meta
Wilaya ya Mbeya na katika Viwanja vya Kijiji cha Isange Halmashauri ya Busokelo
Wilaya ya Rungwe Mkoani hapa.
Meela alisema Serikali ilitoa maagizo
kwa wenye makampuni ya ulinzi kuhakikisha inaajiri wafanyakazi waliopitia
mafunzo ya magambo ili iwe rahisi kupambana na vibaka na wahalifu ambapo katika
mafunzo hayo hujifunza hata mbinu za kujihami ikiwa ni pamoja na kutumia
silaha.
Alisema walinzi ambao hawajapitia
mafunzo ya mgambo ndiyo wanaoshirikiana na wahalifu kutokana na kutokula kiapo
wakati wa mafunzo hivyo kutokujua uadilifu na uzalendo kwa mali za umma na
watanzania kwa ujumla kwa kutoa siri za mali wanazolinda.
Aliongeza kuwa baada ya kufungwa kwa
mafunzo hayo hatatakiwa kuwepo mlinzi wa aina yoyote katika taasisi ya umma
ambaye hakupitia mafunzo ya mgambo, ambapo ikibainika mwenye kampuni pamoja na
mfanyakazi wake watachukuliwa hatua kali iliwa ni pamoja na kuifungia kampuni
hiyo.
Kwa mujibu wa msoma risala katika
mafunzo yaliyomalizika Mbeya mjini, Vicent Nkalla, alisema jumla ya
walioandikishwa walikuwa 500 lakini walioanza mafunzo ni 185 na waliohitimu ni
112 pekee, ambapo wanawake walikuwa 27 na wanaume 85.
Alisema sababu ya kukimbia mafunzo hayo
ni kutokana na utovu wa nidhamu miongoni mwa waliokwepa, wengine walikuwa na
magonjwa mbali mbali na wengine kutokujua umuhimu wa mafunzo ya mgambo kwa
vijana.
Alisema katika mafunzo hayo waliweza kujifunza
jinsi ya kushirikiana, kutumia silaha, kujilinda porini, mbinu za kivita na
ukakamavu pamoja na mafunzo mbali mbali ya zimamoto. Uhamiaji. Takukuru na
huduma ya kwanza katika jamii.
Mafunzo hayo yalianza Julai 15 hadi
Novemba 14 mwaka huu, mafunzo ambayo yalikuwa yakitolewa na askari wa
Jeshi la Ulinzi (JWTZ) kwa ushirikiano na kamati ya ulinzi na usalama ya
Wilaya.
Kwa upande wa mafunzo yaliyomalizika
Wilayani Rungwe, Jumla ya walioandikishwa 466 lakini waliofanikiwa kuhitimu ni
87 ambapo wanawake ni watatu na wanaume 84 ambapo sababu ya utoro imeelezwa
kuwa ni utovu wa nidhamu.
Kutyokana na mahudhurio kutokuwa mazuri
katika maeneo yote Mkuu wa Wilaya ameagiza kila Halmashauri kupitia Madiwani
kutunga sheria ndogo ambazo zitawabana wale wote wanajiandikisha kuhudhuria
mafunzo lakini hukacha pasipo kuwa na sababu ya msingi.
Alisema suala la mafunzo ya mgambo lipo
kisheria hivyo kitendo cha kijana kukubali kuandikishwa lakini siku ya kwanza
ya mafunzo anakimbia inabidi abanwe kupitia sheria ndogo zitakazokuwa
zimetungwa kupitia Halmashauri zao ambapo sheria hizo zitatawanywa hadi katika
ngazi za vijiji na vitongoji.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment