Ndugu wa marehemu Frank Shoka aliyetuhumiwa kwa wizi wa kuku mwili wake ukisubiriwa kuja kuchukuliwa napolisi |
WAKATI jeshi la polisi Mkoani Mbeya
likijitahidi kutoa elimu kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria
mkononi, bado hali imezidi kushamiri baada watu wawili kuuawa kwa tuhuma
za wizi wa mifugo.
Matukio hayo ywmetokea katika Wilaya za
Kyela na Mbeya vijiji yakiwemo ya wizi wa kuku na ng’ombe jambo lililopelekea
wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaua bila kuwafikisha kwenye vyombo
vya dola.
Katika Tukio la kwanza lililotokea
katika kitongoji cha Katusi kijiji cha Mjere wilaya ya Mbeya vijijini wananchi
wamemuua Frank William Shoka(30) kwa tuhuma za wizi wa kuku watatu mali ya
Dismas Rashid(41)mkazi wa kijiji hicho.
Akizungumzia tukio hilo, Dismas Rashidi
aliyeibiwa kuku hao alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 20,mwaka huu na
kuongeza kuwa marehemu alivunja banda la kuku majira ya usiku wa manane na
kuchukua kuku watatu wakati yeye akiwa amekwenda kumuuguza mwanae katika kituo
cha Afya Mjere ambako aliandikiwa sindano za masaa.
Alisema Baada ya kurudi nyumbani na
kukuta kuku wake hawapo alianza kufuatilia na kumkuta marehemu akiwa na kuku
hao katika kituo cha mabasi akitaka kuwasafirisha kwenda Mbeya,alipoulizwa juu
ya kuku hao alikosa majibu wakati huo ikiwa ni saa kumi na moja alfajiri.
Alisema mtuhumiwa huyo baada ya
kushindwa kutolea maelezo juu ya kuku hao wananchi walianza kumpiga kwa kutumia
fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyomfanya kupoteza maisha
papo hapo mita chache kabla ya kufikishwa katika ofisi ya kijiji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mjere, Mussa
Tenson Mgula amesema alipata taarifa za tukio hilo kwa wananchi na alipofika
alikuta mtuhumiwa ameshauawa hivyo alitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji
hicho Evarist Benny ambaye alitoa taarifa kituo cha polisi Mbalizi majira
ya saa mbili asubuhi ambapo Polisi walifika majira ya saa nane mchana na
kuuchukua mwili wa marehemu.
Aidha Baada mwili wa marehemu
kufanyiwa uchunguzi na Daktari mwili ulikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa
taratibu za maziko,hata hivyo wakati wa tukio hilo mke wa marehemu
aliyefahamika kwa jina la Mary Julius[30]alikuwa hayupo nyumbani akidai kuwa
walikuwa wametengana.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa
ya kawaida wakati polisi wakisubiriwa mmoja kati ya kuku walioibwa alitaga yai
moja na kuwaaacha wananchi katika hali ya mshangao.
Katika tukio la pili lililotokea kijiji
cha Lupembe kata ya Katumba Songwe tarafa ya Unyakyusa wilaya ya Kyela Godfrey
Mwakapalila mkazi wa kijiji cha Mpunguti aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali
za mwili wake na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi.
Chanzo cha mauaji hayo ni wizi wa
ng’ombe mali ya Moto Mwakiange(36) mkulima na mkazi wa kijiji cha Muungano
tukio lililotokea majira ya saa mbili asubuhi octoba,19 mwaka huu.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la polisi
linamshikilia Moto Mwakiange kwa mahojiano zaidi wakati upelelezi
ukiendelea wa kuwabaini watu waliohusika na mauaji,aidha mwili wa
marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Diwani
Athumani amethibitisha kutokea kwa matukio yote hayo na kutoa wito kwa wananchi
kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkoani na atahakikisha wale wote
waliohusika na mauaji wanakamatwa ili kujibu tuhuma za mauaji.
Picha na Ezekia Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment