Katika maisha ya kila
siku ya binadamu suala la ulinzi na usalama wa mali na maisha ni muhimu sana.
Binadamu huishi kwa kutegemeana basi ndivyo ilivyo hata katika suala la ulinzi
wa mali na maisha yetu. Unaweza kujiuliza je,ni nani mwenye jukumu la
ulinzi?je,ni mimi au wewe? Au ni sisi sote.
Basi katika miaka ya hivi
karibuni Jeshi la Polisi Nchini limeendeleza dhana ya ulinzi shirikishi na
ulinzi jirani kwa lengo la kushirikisha jamii kwa karibu zaidi katika suala
zima la ulinzi na usalama. Zana hii imekuwa ikitoa fursa kwa jamii na wadau
mbalimbali kutoa taarifa za kuzuia uharifu hali inayofanikisha kudhibiti
vitendo hivyo.
Ni wazi kabisa kuwa kila
mmoja wetu ana jukumu la kushiriki katika ulinzi.Ushirikishwaji huu wa wananchi
katika kuzuia na kudhibiti vitendo vya uharifu ni mpana zaidi, kwani vitendo
vya uvunjifu wa amani na utovu wa nidhamu si vya kuvumilika katika jamii. Kila
mmoja wetu anapaswa kujua nini cha kufanya pale anapoona vitendo ambavyo si vya
kiungwana vikitendeka.
Katika siku za hivi
karibuni hususani katika mechi za
ligi kuu Tanzania bara kumekuwa kukitokea vitendo ambavyo si vya kiungwana wala
kinidhamu katika mchezo wa mpira wa miguu. Vurugu mbalimbali kutoka mashabiki
wa timu zinazoshiriki ligi kuu zimevuka mipaka kwani imefikia hatua hata ya
kurushiana mawe.Katika mechi ya hivi karibuni kati ya Mbeya City dhidi ya Yanga
mechi iliyofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine kulitokea vitendo visivyo
vya kiungwana katika medani ya michezo.
Ikumbukwe kuwa suala la
ulinzi katika sehemu mbalimbali ni jukumu letu sote. Kila mmoja wetu awe mlinzi
wa mwenzake katika kuhakikisha amani na utulivu vinachukua nafasi yake katika
michezo ili kwa ujumla wananchi wapate burudani.
Vurugu na vitendo visivyo
vya kimichezo vina athari kubwa si tu kwa timu bali hata kwa mashabiki na
wananchi wa mkoa husika kwani inapotokea timu kufungiwa kutofanya michezo yake
katika uwanja wa nyumbani ni athari hata katika shughuli za kiuchumi pamoja na
kuua mapato ya mlangoni. Pia vurugu kama hizi ni athari pia katika shughuli za
uwekezaji na kuzuia upatikanaji wa fursa ya ajira kwa wananchi.
Yapo mapendekezo
mbalimbali ya wananchi juu ya suala hili la kudhibiti vurugu katika michezo.
Itambulike kuwa ni suala la kila mwananchi kwani kama kila mmoja wetu ataona umuhimu
wa kutoa taarifa pale anapotilia mashaka mtu/watu kwa vyombo vya ulinzi na
usalama, basi suala hili tunao uwezo wa kulidhibiti na kulimaliza kabisa.Kila
mwananchi atoe ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufanikisha kudhibiti na
kutokomeza vitendo vya vurugu uwanjani na katika michezo kwa ujumla.
Pengine kwa sasa ni muda
muafaka kwa uongozi wa timu pamoja na shirikisho la soka nchini ni kuliangalia
suala hili kwa kina zaidi ili kujiepusha na madhara makubwa zaidi. Kuwepo na adhabu
kali zaidi kwa timu itakayo shindwa kuwadhibiti mashabiki wake dhidi ya vitendo
visivyo vya kimichezo.
Ni imani yangu kuwa kila
mwanamichezo na wadau wote wa michezo watashiriki kikamilifu kuzuia na kutoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi pale waonapo dalili za vurugu kutoka kwa mtu au kikundi cha watu kikipanga njama za
uvunjifu wa amani katika michezo hasa mechi za ligi kuu zinazoendelea.
Kamanda wa Polisi mkoa wa
Mbeya Kamishina msaidizi, DIWANI ATHUMANI anawakumbusha mashabiki na wadau wote
wa michezo kuwa “michezo ni uchumi, michezo ni burudani, michezo ni
upendo/amani na kila mmoja wetu aone kuwa ana kila sababu ya kutekeleza hili”
Imetolewa na:
[DIWANI ATHUMANI – ACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA
MBEYA.
|
No comments:
Post a Comment