Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, April 24, 2013

Mary Mwanjelwa: Kuwa Mbunge wa viti maalumu siyo kubweteka




Kumekuwa na dhana kwamba, Wabunge wa viti maalum ambao hutokana na vyama vya siasa, hawawajibiki moja kwa moja kwa wananchi.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Dk Mary Mwanjelwa anasema kuwa, nafasi hiyo inamweka moja kwa moja katika kuwatumikia wananchi kama walivyo wabunge.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa kukagua miradi ya maendeleo mkoani, amesema kuwa anawajibika kuisaidia jamii katika sekta za elimu, afya na maendeleo ya jamii.

“Nitahakikisha najiotolewa kwa nguvu zangu zote nikishirikiana na wananchi bila kubagua makundi ya walemavu, vijana, watoto, wajane, wajawazito, yatima. Vilevile nitaboresha sekta ya elimu katika kuwepo kwa madarasa ya kutosha, uhakika wa upatikanaji wa vitabu,”
Dk Mwanjelwa anasema hatajali itikadi za vyama na udini katika kuwatumikia wananchi wa mkoa huo kwani wajibu wake kama mbunge ni kunoa makali katika kusaidia jamii.

Anasema katika kipindi cha miaka mitatu yaani tangu mwaka 2011 hadi 2013 mfululizo amechangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Itagano, ujenzi wa mabweni ya wasichana na vitanda 16 na kutoa misaada mbalimbali katika kukabiliana na ukosefu wa miundombinu ya shule.

Mwanjelwa anasema kuwa mbali na kujikita katika sekta ya elimu pia amejitoa kusomesha watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi 10 na kugawa sare za shule kwa watoto 300 katika wilaya za Mkoa wa Mbeya ili kuwaandalia maisha bora ya baadaye.

Anasema kuwa katika uongozi na kama kiongozi ninapaswa na kutambua jukumu langu kwa wananchi wangu hususan kuhakikisha tunatoa mikopo isiyokuwa na riba kwa kinamama wajane ili waweze kuanzisha miradi endelevu katika kujikwamua kiuchumi miongoni mwao.

“Kwa kweli jamii ina changamoto kubwa ambayo kama viongozi tunapaswa kubeba jukumu hilo kwa kuangalia pale tunapoweza katika kuhakikisha tunaboresha huduma za kijamii katika nyanja mbalimbali nchini bila kuangalia jinsia,”
Kwa upande wa afya, anasema kwa kipindi cha mwaka 2012 ametoa misaada ya magodoro 300 katika hosptali za wazazi katika wilaya za mbeya hususan katika wodi ya wazazi ya hosptali ya rufaa ya Meta kwa lengo la kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaolazwa na kusubiri kujifungua.

“Nikiwa kama mwanamke ninapaswa kulenga maeneo yaliyo na changamoto kubwa kwani tuliangalia katika hospitali ya Meta ambapo kulikuwa na changamoto ya muda mrefu ya upungufu wa vitanda na magodoro hali iliyokuwa ikipelekea wagonjwa wawili kulala kitanda kimoja,” anasema.

Mwanjelwa anaziita kuwa changamoto wanazokabiliana viongozi katika jamii.
Kuhusu maendeleo ya jamii, anasema kuwa katika kuhakikisha wanawake wanaachana na utegemezi ametoa mashine za kutotolea vifaranga vya kuku katika wilaya nane za jiji la Mbeya na kuhamasisha kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali.

“Licha ya kutoa mashine hizo nimetoa mitaji ya kuanzishia katika vikundi (saccos) za wanawake ili kuwajengea misingi imara ya usimamizi wa miradi na kujiwamua kiuchumi pindi miradi hiyo inapokuwa endelevu,” anasema na kuongeza:

“Kinamama wakiwezeshwa wanaweza hivyo ni jukumu letu kusimamia miradi wanayoanzisha kiuchumi ili kuweza kusaidia familia zao kielimu, afya na jamii ili waache kuwa tegemezi katika familia.”

Kuhusu elimu ya viongozi, Dk Mwanjelwa anasema ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi bora wa rasilimali, ameanzisha semina kwa madiwani katika halmashauri zote kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji kazi kwa wananchi na kutambua na kuchanganua changamoto zinazoikabili jamii kwa kuzingatia demokrasia, utawala bora na uwajibikaji

Chanzo Mwananchi

1 comment:

MASHAKA S.MBUGI said...

Kwa maelezo hayo big up kwani kazi ni nzuri sister ongeza juhudi usife moyo kwani najua Mbeya tulivyo hatuwapendi wachapakazi zaidi ya kuwapiga madongo na mwisho kuishia kwa kuwapatia madaraka watu walioshindikana na ambao wenyewe hawaoni mbele kama ilivyo sasa balaa mbeya hawataki hata Rais aje mei mosi