Kumekuwa na dhana kwamba, Wabunge wa viti maalum ambao hutokana
na vyama vya siasa, hawawajibiki moja kwa moja kwa wananchi.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Dk Mary
Mwanjelwa anasema kuwa, nafasi hiyo inamweka moja kwa moja katika kuwatumikia
wananchi kama walivyo wabunge.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa kukagua miradi ya maendeleo
mkoani, amesema kuwa anawajibika kuisaidia jamii katika sekta za elimu, afya na
maendeleo ya jamii.
“Nitahakikisha najiotolewa kwa nguvu zangu zote nikishirikiana
na wananchi bila kubagua makundi ya walemavu, vijana, watoto, wajane,
wajawazito, yatima. Vilevile nitaboresha sekta ya elimu katika kuwepo kwa
madarasa ya kutosha, uhakika wa upatikanaji wa vitabu,”
Dk Mwanjelwa anasema hatajali itikadi za vyama na udini katika
kuwatumikia wananchi wa mkoa huo kwani wajibu wake kama mbunge ni kunoa makali
katika kusaidia jamii.
Anasema katika kipindi cha miaka mitatu yaani tangu mwaka 2011
hadi 2013 mfululizo amechangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya
msingi Itagano, ujenzi wa mabweni ya wasichana na vitanda 16 na kutoa misaada
mbalimbali katika kukabiliana na ukosefu wa miundombinu ya shule.
Mwanjelwa anasema kuwa mbali na kujikita katika sekta ya elimu
pia amejitoa kusomesha watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi 10 na
kugawa sare za shule kwa watoto 300 katika wilaya za Mkoa wa Mbeya ili
kuwaandalia maisha bora ya baadaye.
Anasema kuwa katika uongozi na kama kiongozi ninapaswa na
kutambua jukumu langu kwa wananchi wangu hususan kuhakikisha tunatoa mikopo
isiyokuwa na riba kwa kinamama wajane ili waweze kuanzisha miradi endelevu
katika kujikwamua kiuchumi miongoni mwao.
“Kwa kweli jamii ina changamoto kubwa ambayo kama viongozi
tunapaswa kubeba jukumu hilo kwa kuangalia pale tunapoweza katika kuhakikisha
tunaboresha huduma za kijamii katika nyanja mbalimbali nchini bila kuangalia
jinsia,”
Kwa upande wa afya, anasema kwa kipindi cha mwaka 2012 ametoa
misaada ya magodoro 300 katika hosptali za wazazi katika wilaya za mbeya
hususan katika wodi ya wazazi ya hosptali ya rufaa ya Meta kwa lengo la
kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaolazwa na kusubiri kujifungua.
“Nikiwa kama mwanamke ninapaswa kulenga maeneo yaliyo na
changamoto kubwa kwani tuliangalia katika hospitali ya Meta ambapo kulikuwa na
changamoto ya muda mrefu ya upungufu wa vitanda na magodoro hali iliyokuwa
ikipelekea wagonjwa wawili kulala kitanda kimoja,” anasema.
Mwanjelwa anaziita kuwa changamoto wanazokabiliana viongozi
katika jamii.
Kuhusu maendeleo ya jamii, anasema kuwa katika kuhakikisha
wanawake wanaachana na utegemezi ametoa mashine za kutotolea vifaranga vya kuku
katika wilaya nane za jiji la Mbeya na kuhamasisha kujiunga katika vikundi vya
ujasiriamali.
“Licha ya kutoa mashine hizo nimetoa mitaji ya kuanzishia katika
vikundi (saccos) za wanawake ili kuwajengea misingi imara ya usimamizi wa
miradi na kujiwamua kiuchumi pindi miradi hiyo inapokuwa endelevu,” anasema na
kuongeza:
“Kinamama wakiwezeshwa wanaweza hivyo ni jukumu letu kusimamia
miradi wanayoanzisha kiuchumi ili kuweza kusaidia familia zao kielimu, afya na
jamii ili waache kuwa tegemezi katika familia.”
Kuhusu elimu ya viongozi, Dk Mwanjelwa anasema ili kuhakikisha
kunakuwa na usimamizi bora wa rasilimali, ameanzisha semina kwa madiwani katika
halmashauri zote kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji kazi kwa wananchi
na kutambua na kuchanganua changamoto zinazoikabili jamii kwa kuzingatia
demokrasia, utawala bora na uwajibikaji
Chanzo Mwananchi
|
1 comment:
Kwa maelezo hayo big up kwani kazi ni nzuri sister ongeza juhudi usife moyo kwani najua Mbeya tulivyo hatuwapendi wachapakazi zaidi ya kuwapiga madongo na mwisho kuishia kwa kuwapatia madaraka watu walioshindikana na ambao wenyewe hawaoni mbele kama ilivyo sasa balaa mbeya hawataki hata Rais aje mei mosi
Post a Comment