Imeelezwa kuwa sababu za kudorora
kwa ujenzi wa hosteli za wanafunzi katika shule za sekondari Mkoani
Mbeya, ni wananchi kukata tamaa ya kuchangia shughuli za maendeleo kutokana na
kutosomewa taarifa za mapato na matumizi.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo
la Mbarali, Bw.Modestus Dickson Kilufi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri wa
Mkoa(RCC) kilichofanyika jijini mbeya.
Bw. Kilufi alitoa kauli hiyo baada
ya taarifa ya elimu ya mkoa wa Mbeya iliyowasilishwa ndani ya kikao hicho
na Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda, kuonyesha kuwa shule ya
sekondari ya Madibira yenye kidato cha tano na sita iko hatarini kufungwa
kutokana kukosa hosteli, hali inayosababisha wanafunzi kulala madarasani.
Alisema kuwa suala la wananchi kususia
kujitoa katika kuchangia maendeleo hususani ujenzi wa hosteli kwa ajili ya
wanafunzi Mkoani hapo unatokana na utendaji na usimamizi mbovu wa
viongozi wanaohusika kwa kutowasomea mapato na matumizi huku kukiwa hakuna
jambo lolote linaloendelea baada ya kutoa michango yao.
Akitolea Mfano wa Shule ya
Sekondari ya Rujewa Mbunge huyo alisema kuwa wananchi walijitoa kimasomaso
kuchangia ujenzi wa madarasa ya kidato cha tano na sita muda mrefu lakini
tangu wachangie michango hiyo hadi hakuna linaloendelea hadi sasa
jambo ambalo alidai kuwa linachangia wananchi hao kukata tama ya
kuchangia.
“Naomba ieleweke wazi kwamba
wananchi siyo kusema kuwa hawataki kuchangia maendeleo ya ujenzi wa
Hostel, tatizo lililopo ni kwamba wananchi wamekuwa wakichanga michango yao
lakini wamekuwa hawasomewi mapato na matumizi huku kukiwa hakuna ujenzi wowote
unaokuwa ukiendelea” alisema na kuongeza.
“Wananchi wapo tayari kuchangia
maendeleo hayo lakini sumu iliyopo ni hiyo ya kutosomewa mapato ya
matumizi ya michango yao, na kwamba hata kama wananchi hao ni wajinga kiasi
gani kwa hilo hawata kuwa tayari kuendelea kujitoa kwa nguvu zao huku wasijue
fedha zao zinakwenda wapi”alisema Mbunge huyo.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa
Viti Maalum (CCM), Bi.Hilda Ngoye alihoji uhalali wa kufunguliwa kwa shule hiyo
ya Madibira wilayani Mbarali, wakati sera ya taifa ya elimu inaelekeza kuwa
shule yenye kidato cha tano na sita ili ifunguliwe kigezo cha kwanza ni
kuwepo kwa hosteli kwa wanafunzi wote.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia
ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw.Abbas Kandoro alionyesha kushtushwa na hoja hiyo na
kuhoji kazi za kamati za maendeleo ya kata, pamoja na kuagiza wakuu wote wa
wilaya Mkoani hapo kufuatilia na kuhakikisha taarifa za mapato na
matumizi zinasomwa katika kila kijiji na yeye (Kandoro), kupewa nakala za
taarifa hizo.
Na Esther Macha, Mbeya
|
No comments:
Post a Comment