SHIRIKA la Nishati na umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Mbeya
limewataka wateja wake wilayani Ileje waliotapeliwa na Mhasibu wa shirika hilo
Emmanuel Ntahemuka kutoa taarifa Polisi kisha kumshitaki.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Tanesco mkoa wa Mbeya John
Bandiye alipokuwa akizungumza na wateja wa shirika hilo na waandishi wa habari
waliofika katika ofisi za Tanesco wilaya ya Ileje wakati zoezi la kukata umeme
na kukusanya mapato ya shirika hilo likiendelea.
Bandiye alisema hayo baada ya wateja kulalamikia utaratibu wa
shirika hilo kukata umeme bila taarifa kwa madai kuwa wateja hao wanadaiwa
madeni mengi huku wao wakiwa wamelipa na kupewa stakabadhi ambazo zinadaiwa
kuwa ni za kugushi.
Meneja huyo alisema kuwa lengo la shirika lake si kukata umeme
bali ni kukusanya mapato na kwamba tayari baadhi ya wateja kuelimishwa na
kupewa ufafanuzi wameanza kulipa kwa makubaliano maalum kutokana na madeni yao
kuwa makubwa.
‘’Lengo la Shirika siyo kukata umeme bali ni kukusanya mapato
yake ambayo hayajalipwa kwa muda mrefu na malipo mliyokuwa mnalipa hayakuwa
yanaingia kwenye mtandao wa Shirika na ndiyo maana hata mihuri ya stakabadhi
siyo ya mashine mhasibu mliyekuwa mnampatia fedha mpaka sasa tumemsimamisha
kazi kwa ajili ya uchunuzi na anayetaka kumshitaki ni ruksa na sisi
tutawasaidia ili akamatwe na Polisi’’ Alisema Bandiye.
Alisema Ntahemuka amesimamishwa kazi kwa ajili ya uchunguzi na
hatua zingine zitachukuliwa dhidi yake pamoja na wenzake.
Mbali na hayo ameomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wateja
wote na kwamba kuanzia sasa wateja wenye shida wafike katika ofisi hiyo au
wapige simu yake ya kiganjani ambayo aliitaja kuwa ni 0754 214499.
Jumla ya wateja 989 wa Tanesco wapo wilaya ya Ileje ambayo ni
wilayailiyopo pembezoni mwa Tanzania mpakani na nchi ya Malawi.
Kwahisani ya Gordon Kalulunga, Ileje
|
No comments:
Post a Comment