Licha ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka waislamu nchini kushiriki zoezi la Sensa ya watu makazi, hali hiyo imeonekana kuwa tatizo kwa kijiji cha Ruiwa Kata ya Ruiwa Wilayani Mbarali ambapo watu wasita wanaosadikiwa kuwa ni waislamu wenye msimamo mkali kugoma kuhesabiwa kwa madai kuwa serikali imepuuza madai yao.
Imeelezwa kuwa waislamu hao walishaeleza serikali kuwa hawako tayari kuhesabiswa lakini bado serikali imeshindwa kutekeleza matakwa yao na hivyo kukataa kuhesabiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusiana na madai hayo , Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa Bw. Jordan Masweve alisema kuwa kwa kata zoezi la sense toka limeanza imekuwa ni tatizo kubwa sana kutokana na watu hao kuonyesha msimamo wao wa kutotaka kuhesabiwa.
“Wao wanadai kuwa hawapo tayari kuhesabiwa hata iweje msimamo wao ni mmoja hata wafanywe nini lakini suala ni kutokubali kuhesabiwa tu kwa madai serikali imeepuza madai yao toka mwanzo ya kutotaka kuhesabiwa”alisema.
Bw. Masweve alisema tukio hilo limetokea Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 8.30 mchana katika kijiji cha Ruiwa wakati makarani wa sense walipofika katika makazi wa wananchi hao wakiongozwa na Mtendaji wa kijiji kwa lengo la kuwataka wakubali kuhesabiwa lakini waligoma.
Alisema hata hivyo zilifanyika jitiha za kuwasihi kushiriki zoezi hilo lakini hawakutaka kukubali ndipo mgambo wa kijiji walipowakamata na kuwapeleka kwenye ofisi ya Kata.
Bw. Masweve aliwataja waislamu waliokamatwa kuwa ni Ally Mwangoto,Subeti Juma, Abinala, Pembe ,Ally Suleiman pamoja na Nawab Suleiman licha ya kufikishwa katika ofisi ya kata bado waliendelea kuwa na msimamo wao kuwa hawako tayari kuhesabiwa na kudai kuwa vyovyote itakavyokuwea wapo tayari hata kuchinjwa au kufungwa jela lakini si kuhesabiwa.
Hata hivyo alisema kuwa waislamu hao walidai kuwa hata Mkuu wa Wilaya akifika hapo hawako tayari kuhesabiwa msimamo wao ni mmoja tu .
“Bado tupo nao hapa ofisini tukisubiri Mkuu wa Wilaya ya Mbarali ,na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbarali ili waje kuwachukua watu hawa”alisema.
Aidha aliongeza kuwa kabla ya zoezi hilo kuanza kulikuwa na mikutano ya hadhara ambayo ulikuwa unaendeshwa na viongozi wa kiislamu kutoka Jijini Mbeya walikuwa wakihamasisha waislamu wenzao kuwa ambao hawatakuwa tayari kushiriki zoezi hilo kukimbilia misikitini ambako watawapelekea chakula mpaka zoezi hilo litakapokuwa limekamilika.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea kijiji cha Ruiwa Mkuu wa Wilaya Mbarali Bw. Gulamu Hussen Kiffu alisema amepata taarifa za tukio hilo lakini bado hajafika huko lakini yupo njiani kuelekea huko ili aweze kujua undani wa tukio hilo.
“Kwasasa nipo kwenye gari naelekea Ruiwa kwa ajili ya tukio hilo mara baada ya kufika na kuangalia tukio lilivyo nitatoa taarifa kamili na hatua zipi ambazo tutakuwa tumechukua”alisema.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Bw.Athuman Diwani alisema bado hajapata taarifa hizo na kudai kuwa taarifa zote za matokeo atatotoa mara baada ya zoezi la sense kumalizika. |
1 comment:
Kweli ujinga ni sawa na zigo la kuni. Ukigoma sensa kwani usipohesabiwa inakuwaje utafaidika nini?
Post a Comment