SHEKH Yassin Bambala wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya amevuliwa wadhifa huo kwa kosa la kuhamasisha waumini wa dini ya Kiislam kususia zoezi la Sensa ya watu na makazi litakalo anza usiku wa kuamkia Agosti 26,2012 kote nchini Tanzania.
Tamko hilo la kumvua wadhifa huo limetolewa na Katibu wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Mbeya Shekh Juma Kila katika ofisi ya Bakwata iliyopo eneo la Sokomatola Jijini Mbeya mara baada ya kukamilika kwa maamuzi ya baraza hilo.
Katibu huyo alisema hatua hiyo imetokana na Sheikh Bambala kushiriki na kuhudhuria vikao vya baadhi ya waislamu wanaopinga zoezi la Sensa kufanyika kwa kuwataka waislamu wasijitokeze kuhesabiwa.
Alisema baraza hilo limebaini kuwa wapo baadhi ya viongozi wenzao ambao walikuwa wakionekana kufanya kampeni za chini chini kuungana na taasisi nyingine kuwataka waislam wasishiriki Sensa ya mwaka huu.
Alisema kitendo hicho kinapingana na msimamo wa BAKWATA na kiongozi mkuu wa Waislamu (Mufti), kuhusu kuhakikisha waislamu wanashiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Killa alisema wahusika hawa wamekiuka maagizo ya pamoja ya waislamu kwani awali masheikh wa ngazi za wilaya na wale wa mikoa nchini, waliitwa na Mufti mjini Dodoma kwenye kikao cha Tume ya dini na kupeana msimamo wa pamoja kuhusiana na zoezi la Sensa na wakakubali kurudi kwenye maeneo kuwahamasisha waislamu wenzao juu ya umuhimu wa Sensa.
Aliongeza kuwa wamebaini kuwa baadhi ya Masheikh, akiwemo Sheikh Bambala baada ya kurudi kutoka Dodoma, wameanza kufanya kazi tofauti na makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa.
Katibu huyo wa BAKWATA mkoa, alisema kufuatia hali hiyo wameanza kuchukua hatua kali kwa viongozi waliodhihirika na ushahidi kupatikana kuwa wamekuwa wakienda kinyume na maagizo ya Tume ya Dini hiyo. Hata hivyo alisema nia ya kumvua madaraka kiongozi huyo ni kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi wa dini hiyo ya Kiislamu anayeamua kwa matakwa yake kupingana na misimamo ya Baraza pamoja na ile ya serikali.
Aidha aliwasihi wananchi kujitokeza katika zoezi hilo na kuwapuuza baadhi ya watu wanaopita kuhamasisha ili kususia zoezi hilo.
Kwa hisani ya Gordon Kalulunga na Venance Matinya
|
No comments:
Post a Comment