Katika warsha iliyohudhuriwa na waandishi wa mkoa huo kwa siku tatu iliyofanyika katika ukumbi wa Mtenda Sunset Centre, wawezeshaji wa warsha hiyo Beda Msimbe na David Mbulumi, walitoa ufafanuzi kuhusu changamoto na Mtanziko wa maadili ya Uandishi wa Habari ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha waandishi kubaini habari zinazokiuka maadili kwenye Magazeti.
Mwezeshaji Beda Msimbe alisema kuwa kumetokea mmomonyoko wa maadili na kupoteza uzalendo kwa baadhi ya Wahariri na waandishi wao jambo ambalo linasababishwa na sababu mbalimbali ambazo aliwaachia washiriki kuzitaja ambapo baadhi ya waandishi walisema kuwa baadhi ya wahariri wamekuwa wakiwaomba rushwa waandishi wao huku hawawalipi malipo ya habari zao.
Msimbe alifundisha dhana na Misingi ya DEFIR pamoja na madhumuni yake ambapo alikumbusha wajibu na changamoto zilizoainishwa kwenye azimio hilo kwa Wamiliki wa vyombo vya habari, Wahariri, waandishi, Dola, watoa matangazo, wafadhili, wanasiasa, Mabalozi na wadau wengine wa habari.
Sanjari na hayo wawezeshaji hao walisema kuwa ni muhimu waandishi wa habari wakawa na uzalendo badala ya kuandika habari za kuwatumikia watu wachache na kuuacha umma wa watanzania ambao ndiyo unawategemea kupata habari za uhakika ambazo hazijatiwa chumvi.
Katika warsha hiyo waandishi walioshiriki walijifunza tofauti ya uandishi wa Udaku na unaowajibika kwa jamii, uandishi wa Habari kitaaluma dhidi ya uandishi wa Media jamii mfano mitandao ya kijamii ambayo mingine haimilikiwi na watu wenye taaluma ya Habari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoani Mbeya Christopher Nyenyembe, alisema kuwa warsha hiyo ni chachu mpya kwa waandishi wa habari ambao ni kioo cha jamii ambapo kutokana na warsha hiyo anaamini kuwa waandishi wamejifunza na kuelewa vema makosa ambayo walikuwa wakiyafanya awali na kutoitendea haki jamii kwenye habari zao.
No comments:
Post a Comment