na Gordon Kalulunga, Mbeya
WAKATI serikali ikitafakari jinsi ya kurudisha nyumba zake zilizouzwa kwa watu binafsi nchini, nyumba yake nyingine imeuzwa jijini Mbeya kwa mfanyabiashara maarufu, Tanzania Daima limedokezwa.
Nyumba hiyo iliyoko eneo la Mafiati yenye namba 162 block S, licha ya Wakala wa Majengo mkoa wa Mbeya kuzuia kuuzwa, kampuni ya udalali ya J.A. Kandonga Court Broker $ Public Auctioners, ilikaidi na kuiuza.
Nakala ya barua ya wakala wa majengo mkoa wa Mbeya ya Julai 4 mwaka huu yenye kumbu kumbu namba MID/TBA/MBY/GH 162 'B'/8, iliyopelekwa kwa dalali huyo, ilisema kuwa inasikitika na tangazo la dalali huyo kuhusu kukusudia kuiuza nyumba hiyo kutokana na amri ya mahakama.
Barua hiyo ambayo imesainiwa na kaimu wa wakala huyo mkoa wa Mbeya, Jafari Kiyoga, imesema kuwa kwa taratibu za kiserikali nyumba hiyo isingepaswa kuuzwa kutokana na mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za serikali ambapo sheria inaruhusu nyumba hizo kuuzwa baada ya miaka 25 tangu kutolewa kwa hati miliki.
“Ofisi ya wakala wa majengo inasikitika kumtaarifu dalali huyo kuwa tangazo lake ni kinyume na mkataba wa mauziano ya nyumba kati ya serikali na mtumishi husika,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Ilisisitiza kuwa kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na 10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka 25 kuanzia tarehe ya hati miliki.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka kwenye mamlaka mbalimbali vilisema kuwa nyumba hiyo imeuzwa kwa sh milioni 250 kwa mfanyabishara maarufu mkazi wa Dar es Salaam ambaye ni mzaliwa wa mkoa wa Mbeya.
Mtumishi aliyekuwa ameuziwa nyumba hiyo awali na serikali, Simboleo Gibson Kileo, alipotafutwa kuthibitisha kuwa nyumba hiyo imeuzwa alikiri kuuzwa kwa nyumba hiyo kinyume cha sheria.
Alisema nyumba hiyo aliinunua mwaka 2002 na kumalizia malipo 2005 na kisha kupatiwa hati miliki mwaka 2007, lakini akadai kushangazwa na dalali huyo kufika eneo la nyumba na kuwakwepa watu waliokuwepo kwa ajili ya kuinunua nyumba hiyo.
Dalali aliondoka na kurejea baadaye na kuwatangazia watu kuwa nyumba hiyo tayari ilikuwa imenunuliwa kwa sh milioni 250 huku wengine wakiwa tayari kuinunua kwa milioni 400.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment