Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, July 10, 2012

‘Vijana hawaielewi sera yao’


na Angelica Sullusi, Mbeya
SERA ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana, haitekelezwi ipasavyo na viongozi serikalini kutokana na baadhi yao kutoielewa vyema.
Katibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Amani ‘The Foundation of Life’ ya mkoani Mbeya, Philimon Mwansasu, alisema hayo mwishoni mwa wiki wilayani Kyela wakati akizungumza kwenye mdahalo wa Jukwaa la Vijana.
Mwansasu alisema kuwa kwa mujibu wa Sera ya Vijana ya mwaka 1995 na mabadiliko yake ya mwaka 2007, viongozi wa serikali wanapaswa kuanzisha umoja wa vijana kwenye maeneo yao na kuwasimamia.
Alisema kuwa sera hiyo inawaelekeza wakuu wa mikoa kuwa ndio wenyeviti wa vijana wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwa wenyekiti wa umoja wa vijana wa wilaya, madiwani kuwa wenyeviti wa vijana kwenye kata zao na kwenye vijiji.
“Hii migomo iliyopo, maandamano na vurugu zinazofanywa na vijana katika maeneo mbalimbali nchini zinaweza kuepukika tu kama viongozi wa serikali watatekeleza kwa vitendo sera ya taifa ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007,” alisema Mwansasu.
Alisema kuwa Sera ya Maendeleo ya Vijana inaelekeza kuwa kila halmashauri nchini itenge asilimia kumi ya pato lake kwa ajili ya maendeleo ya vijana, lakini katika halmashauri nyingi fedha hizo hawapewi vijana na badala yake huelekezwa kwenye mambo mengine.
Mwansasu alisema kuwa kama vijana wataungana na kuunda chombo chao, watakuwa na sauti ya kuziomba fedha hizo na kuzitumia kwenye vikundi vyao kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Vijana wapatao 80 waliunda Jukwaa la Vijana la Wilaya ya Kyela na kuchanga sh 400,000 kwa ajili ya kuwawezesha wawakilishi wao kwenda jijini Dar es Salaam kusajili jukwa hilo.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments: