HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, kupitia Baraza la Madiwani limewafukuza kazi watendaji sita, wakiwemo watumishi watatu wa Idara ya Uhasibu kwa tuhuma za kujipatia fedha isiyo halali kiasi cha shilingi milioni 35,328,314. Watumishi waliokabiliwa na tuhuma hiyo ni Sarah Kibona Mhasibu mwandamizi,Tito Robart Mwakisole Mhasibu daraja la kwanza pamoja na Petro Ulamso Yohana ambaye ni mlinzi. Akitoa tamko la kuwafukuza kazi , Meya wa Jiji la Mbeya Athanasi Kapunga, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani mara baada ya kukaaa kama Kamati ya kuwajadili watumishi hao, Baraza limependekeza kufukuzwa kazi kwa watumishi hao. Alisema, Sara Kibona pamoja na Tito Robert wanakabiliwa na shitaka (kanuni 42) kujipatia fedha isiyo halali (wizi)kiasi cha shilingi milioni 35,328,314.94 na shitaka la pili (kanuni ya 42) kushindwa kutimiza wajibu au kutekeleza maelekezo aliyopewa na mwajiri wake wa kazi na hivyo kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha. Alisema, watuhumiwa wote wanadaiwa kutumia fursa ya cheo chao kwa kushirikiana na mtumishi wa Benki ya NMB kuiba fedha za mishahara ya watumishi wasiostahili kulipwa kwa kuingiza mishahara hiyo kwenye akaunti za watu mbalimbali pamoja na za kwao wenyewe. Aidha, Meya huyo alisema kuhusu mlinzi Petro Ulamso yeye akaunti yake inadaiwa kutumiwa na wahasibu hao kwa kuingiziwa fedha shilingi milioni 3,875,350 ambazo ni mali ya mwajiri. Pia mlinzi huyo anakabiliwa na shitaka la pili la kushindwa kutimiza wajibu akiwa kama mlinzi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya na kushindwa kutoa taarifa ya kuingizwa kwa kiasi hicho cha fedha isivyo halali kwa mwajiri ili zirejeshwe serikalini. Baraza hili limependekeza kufukuzwa kazi kwa mthamini ardhi daraja la kwanza Joseph Ndaki kwa tuhuma za kughushi taarifa za uthamini wa ardhi ili kuidanganya serikali kwa kusudio la kujipatia manufaa binafsi kutokana na fedha ya zaidi ambayo ingelipwa kama fidia ya eneo la Ikuti na Inyala kwa ardhi na mali ambazo hazipo.
pia mtumishi huyo anadaiwa kushindwa kutimiza wajibu akiwa mtumishi wa umma, kuharibu taswira ya utumishi wa umma mbele ya jamii na kufanya vitendo vinavyodhalilisha utumishi wa umma ukishirikiana na wananchi wasio waadilifu kughushi taarifa na pia kudhalilisha mamlaka ya halmashauri ya jiji la Mbeya. Alisema, Ndaki alikuza eneo la uthamini pasipo uhalali na kwamba hekta 72 ndizo alipaswa kuzifanyia kazi lakini yeye aliingiza hekta 190 kwa maslahi yake mwenyewe na hivyo baraza limependekeza afukuzwe kazi.
|
No comments:
Post a Comment