Habari na Ester Macha, Chunya.
Zao la Tumbaku ni zao ambalo limekuwa likiwakomboa wananchi na hivyo kupunguza ukali wa maisha waliyonayo hasa maeneo ya vijijini ambako wananchi wake wamekuwa na maisha magumu,licha ya kuwakomboa wananchi pia hata serikali imekuwa ikiongeza mapato yake kupitia halmashauri zake za wilaya zinazolima zao hilo.Kilimo hicho cha Tumbaku kimekuwa kiingizia serikali dola za kimarekani 614.8 kutokana na ushuru unaotolewa baada ya mauzo ya zao hilo kwa wakulima.
Kwa kutambua hilo serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vyama vya ushirika ambavyo vimeundwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima vinaboreshwa na hata kusaidia ili viweze kupata mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha lengo likiwa ni kumsaidia mkulima ili aboreshe kilimo cha tumbaku.
Vile vile hata ukiangalia katika halmashauri za Wilaya nchini ambazo zinalima tumbaku katika mapato yao ya halmashauri asilimia kubwa wamekuwa wakipata mapato makubwa kutokana na kilimo cha zao hilo na ndio kimekuwa mkombozi kwao.
Hata hivyo kilimo hicho kwa muda mrefu kimekuwa mkombozi kwa wakulima na hivyo kumwondolea umasikini na hata halmashauri za Wilaya nchini ambazo mikoa yake inalima Tumbaku zimekuwa zinaongeza kipato kutokana na uuzaji wa Tumbaku ambapo kwa miaka miwili mfululizo zaidi ya sh.Bil.26 zimepatikana.
Hivi karibuni Chama kikuu Cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Wilayani Chunya (CHUTCU LTD) kilifanya mkutano mkuu wa kawaida na kuhudhuliwa na wanachama wa vyama vya ushirika vya Msingi 21(AMCOS) ambavyo vinalima zao la Tumbaku kupitia wanachama wake wa vyama vya ushirika vyenye wakulima zaidi ya 8,057.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi. Mariamu Mtunguja anasema kuwa mkutano huo uwe na manufaa na ambao utalenga kujadili na kujenga ushirikiano na kukuza zao la tumbaku ambalo ni kichocheo cha maendeleo kwa wakulima.
Bi. Mtunguja anasema kuwa ili vyama vya ushirika viweze kuwa imara hakuna budi viongozi wanaopata madaraka kuhakikisha kuwa wanatatua matatizo ya wakulima ambao wamekuwa na matatizo mbalimbali katika kilimo cha Tumbaku hususani maeneo ya vijijini.
"Ndugu zangu viongozi hakikisheni mnafanya kazi vizuri ili kuondoa maswali kwa wakulima wenu kuwa mlipokuwa madarakani mlifanya nini, badala ya kiongozi kuhoji ushirika umemfanyia nini alipokuwa madarakani "alifafanua kiongozi huyo.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo aliwataka wanaushirika kuwa mfano mzuri wa kuigwa na wengine kwa kuondoa migogoro iliyopo ndani ya ushirika badala yake wafanikishe maendeleo mazuri kwa wakulima waliowachagua na kwamba hiyo itawafanya waliowachagua wawe na imani na uongozi uliopo madarakani.
Akizungumzia kuhusu takwimu za uzalishaji wa zao hilo Kiwilaya Bi.Mtunguja anasema kuwa mekuwa ukipanda kutoka tani 5,361 kwa msimu wa mwaka 2008/2009 hadi tani tani 7,540 kwa msimu wa mwaka 2009/2010 ikiwa ni ongozeko la zaidi ya asilimia 28.9 huku msimu wa mwaka 2010/2011 kukiwa na tani 12,570 zilizalishwa ambayo ni sawa na ongozeko la asilimia 40.21.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo anasema kuwa kuongozeka kwa uzalishaji huo kumechangiwa na wanaushirika kuanza kujitegemea na hivyo kurudisha tija kwa wakulima kutokana na bei ya pembejeo inayotolewa bila faida ambazo zilikuwa zinawekwa na makampuni wakati wao wakiwa wanafanya biashara ya tumbaku
Aidha anaongeza kuwa bei nzuri ya Tumbaku iliyotolewa kwa msimu wa mwaka 2008/2009/2010 ambayo ilitokana na utaratibu wa wakulima kupitia vyombo vyao vya ushirika kuagiza na kusambaza pembejeo kumejenga imani kubwa na makampuni kuamini kuwa wanaushirika wanaweza wakiamua kwa umoja wao.
Anasema kuwa pia mfumo huo unaweza kupunguza kasi ya ongozeko la gharama za kilimo cha tumbaku hasa pembejeo za kilimo ambazo zimekuwa shida kwa wakulima.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo anasema kuwa kutokana na kuthamini wakulima wake serikali itaendelea kuunga mkono kwa kuvidhamini vyama vya ushirika kupata mikopo kutoka katika mabenki mbalimbali ili waweze kuboresha kilimo cha tumbaku.
Kuhusu kudangwanywa wakulima Bi. Mtunguja aliwataka wakulima kuacha kudanganywa na watu wasiopenda maendeleo ya ushirika kwa kuwaambia pembejeo zinatolewa na wanaushirika kwa bei kubwa na hazijakidhi
viwango na kusema kuwa yote ni kutaka kuwakatisha tamaa ili warudi kwenye shida walizokimbia.
Aidha Bi. Mtunguja anasema kuwa licha ya kuwa na ongozeko hilo la uzalishaji wa tumbaku la zaidi ya asimilia 100 bado bei ya tumbaku ilishuka kutoka wastani wa USD 2.34 kwa kilo katika msimu wa mwaka 2010/2011 hadi kufikia wastani wa dola 1.4 kwa tumbaku ya mvuke katika msimu wa kilimo uliopita.
Anasema kuwa hata baada ya mahitaji kuongozeka kimataifa tumbaku ilihitajika tena kwa wingi na ndio maana msimu ujao wa mauzo bei ya msingi ya Tumbaku ya mvuke imepanda kufikia dola za kimarekani 1.82 kwa kilo na bado kuna makampuni yamelata mahitaji mengine.
Aidha Katibu Tawala huyo amewataka wakulima wa tumbaku kulima mazao mbadala kutokana na zao hilo kuendelea kupigwa vita na wanaharakati mbalimbali duniani.
Anasema kuwa licha ya kuwa zao hilo bado linaendelea kupigwa vita lakini ni vema wakulima pia wakajikita zaidi na mazao mengine ambayo yanakubali katika maeneo hayo ambayo nayo yatakuwa mkombozi kwa mkulima.
Bi. Mtunguja anasema kuwa kauli hiyo hailengi kukataza kilimo cha zao hilo bali kuanza kuchukua tahadhari mapema kwakuwa hakuna ajuaye nini yatakuwa matokeo ya hoja zinazojadiliwa na kupiganiwa na wanaharakati wanaopinga uvutaji wa sigara.
Aliyataja mazao yanayoweza kupewa nafasi na kuleta manufaa makubwa kwa wakulima kuwa ni pamoja na ufuta unaostawi katika ardhi ya wilaya ya Chunya, karanga pamoja na alizeti.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHUTCU Wilaya ya Chunya Bw. Sebastian Mogela amekiri ushirika kuendelea yategemea makampuni ni kuchelewa kupiga hatua kimaendeleo akisema yapo kwaajili ya kufanya biashara yapate faida na si kutoa misaada kwa wakulima.
Bw.Mogela amesisitiza kuwa za umuhimu wa chama kikuu hicho kuwa na maofisa ugani wake ili waweze kusimamia kwa karibu kilimo hicho na kuleta manufaa zaidi kwa wakulima badala ya kuendelea kutumia wataalamu wa makampuni yanayonunua tumbaku.
Anasema kuwa hiyo itasaidia wakulima kupatiwa ushauri kupitia maafisa wao kuliko kutumia makampuni binafsi anayonunua tumbaku.
Hata hivyo kwa kutambua umuhimu wa zao la tumbaku bodi ya Tumbaku nchini hivi karibuni ilifanya mkutano wake maalamu ambao lengo lake kuu ilikuwa ni kujadili kupandisha kiwango cha uzalishaji kutoka tani 50,000 mwaka 2009 hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka 2010 jambo ambalo lilifikiwa kwa kuzalisha tani 126 sawa na asilimia 103.
Akizungumza katika huo maalamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Vita Kawawa anasema kuwa pia lengo kubwa ya mkutano huo pia ni kuangalia changamoto za zao hilo na na mafanikio
Anasema halmashauri za Wilaya nchini pia zinaongeza kipato kutokana na uuzaji wa Tumbaku ambapo kwa miaka miwili mfululizo zaidi ya shilingi bilioni 26 zimepatikana.
Pia Bw. Kawawa anasema kuwa mkutano huo uelekeze nguvu zake kuwakomboa wananchi wa Mkoa huo jinsi ya kufaidika kwa kupata ajira kutokana na kiwanda cha kusindika Tumbaku ambacho mpaka sasa kimekaa bila kufanya kazi zaidi ya miaka 10.
Hata hivyo Meneja Mkuu wa CHUTCU Wilayani Chunya Bw.. Bakari Kassia ametaja mikoa ambayo inalima tumbaku kuwa ni Mbeya, Shinyanga, Ruvuma, Iringa,Tabora, Rukwa mkoa wa katavi,Singida na Kigoma.
Anasema kuwa katika mikoa hiyo nane ndo imekuwa ikizalisha tumbaku kwa wingi na kwamba kwa Mkoa wa Mbeya ni Wilaya ya Chunya ambayo inalima kwa Tarafa tatu ambazo ni Kiwanja, Kwimba na Kipembawe.
Hata hivyo anasema kumekuwepo na changamoto mbali mbali katika halmashauri ya wilaya ya Chunya kushindwa kuwahimiza wananchi kuhusu kilimo cha tumbaku wakati ndo kinaongoza kuwapatia mapato, kingine ni maafisa ushirika kushindwa kuhimiza wananchi kutokana na halmashauri kushindwa kuwapatia mahitaji muhimu ili waweze kuwahimiza wananchi.
No comments:
Post a Comment