MBUNGE wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya Dr.Mary Mwanjelwa amekanusha uvumi ulioripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuwa anatarajia kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Alisema taarifa hizo ni uzushi na uongo kwa sababu yeye ni kada wa CCM wa siku nyingi ambaye amepewa dhamana na chama hicho kugombea ubunge kupitia jumuiya ya wanawake hivyo hatarajii kuwageuka kwa sababu bado anayo dhamana ya kuendelea kuwa Mbunge.
Alisema, taarifa hizo zimenishtua sana, na hata wapiga kura wangu nao wamepata mshtuko mkubwa na wakanipigia simu ili kutaka kupata ukweli kutoka kwangu hivyo nimeona ni vizuri nitoe ufafanuzi. Alisema yeye ni mbunge wa wananchi wote mkoani hapa, hana matatizo yeyote na chama hivyo haielewi sababu za kumfanya ahame chama chake na kujiunga na CHADEMA, kwa sababu ya uteuzi wa baraza jipya la mawaziri. "Mimi ni mbunge kwa tiketi ya CCM na pia ni kada wa chama ambacho ndicho kilichonipitisha kugombea nafasi ya ubunge viti maalumu, na hatimaye nikafanikiwa kuchaguliwa sasa iwaje leo nikihame chama,"alihoji Mbunge huyo. Aliongeza habari zilizoripotiwa ni za uongo, na kuwa kamwe hawezi kuingilia uteuzi wa Rais Kikwete katika kuwateua mawaziri, kwani hayo ni mambo ambayo hayamhusu kabisa. Dk.Mary alisema yeye amekwenda Bungeni kuwawakilisha wananchi wa mkoa wa Mbeya, sikwenda Bungeni kwa sababu ya kutaka kuwa Waziri, hizo ni nafasi za uteuzi na mwenye mamlaka hiyo ni Rais Kikwete. Mbunge huyo wa viti maalum Mbeya, aliongeza hivyo ni vyema waandishi wa habari waache kuandika habari za kuchafuana, kuharibiana bali wafuate misingi na maadiri yanayolinda tasnia ya habari. Alisema iwapo mwandishi anakuwa amepata taarifa ni vyema amfuate muhusika ili kupata ukweli juu ya habari anayotaka kuiandika iwapo ina ukweli wowote ndani yake. Aliongeza kama hayo yalikuwa ni maoni ya wananchi, anashindwa kuelewa yeye anaingizwaje katika habari hiyo, kwani ana mkataba wa kuwatumikia wananchi kwa miaka mitano na amebakiza miaka mitatu. "Siwezi kuhamia CHADEMA, kwani CCM haijanifanyia kosa lolote, sikwenda Bungeni ili niteuliwe kuwa Waziri, kikubwa kwangu ni kuingia Bungeni kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi wangu wa mkoa wa Mbeya" alisema Dk.Mary. Kwa mujibu wa Mwanjelwa alisema kuwa ni kweli alizungumza na Mwandishi aliyeandika habari hizo na kwamba mwandishi huyo alikuwa akitaka kupata ufafanuzi wa uvumi ulioenea ya kwamba kuna baadhi ya wananchi wanataka kwenda kumuona ili wamshawishi akihame chama kwa sababu ya Rais hakumteua kwenye Baraza jipya la Mawaziri. "Mimi nilimjibu mwandishi huyo ya kwamba huo ni mtazamo wa wananchi lakini si wa kwangu "alisema Mwanjelwa huku akisisitiza kuwa hicho ni kipindi chake cha kwanza kuingia Bungeni sasa iwaje ashikwe na tamaa ya kutaka kushika madaraka ya juu . Hata hivyo, alisema atagombea tena nafasi hiyo kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ili wanawake wampe tena kura zao kwani anajijua bado anafaa zaidi ya kufaa, hivyo atajitokeza katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015 kutetea nafasi yake hiyo kwa tiketi ya Chama cha mapinduzi..
|
1 comment:
C C M Mbeya nawauliza huyu Mheshimiwa ameolewa?kiukweli nimempenda kanivutia mno tafadhalini jamani nimempenda
Post a Comment