MKULIMA AKIWEKA MBOLEA KATIKA SHAMBA DARASA
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbeya imetoa msaada kwa wananchi walioathirika na mvua zilizonyesha na kuharibu mazao katika kijiji cha Nsambya kata ya Iwindi iliyopo katika halmashauri hiyo mkoani hapa.
Msaada huo ulitolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo Evance Balama akiongozana na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Juliana Malange pamoja na mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini (CCM) Lackson Mwanjali na mwenyekiti wa halmashauri hiyo Andason Kabenga.
Wananchi wa kijiji hicho walipata hasara baada ya mvua kubwa kunyesha na kuharibu jumla ya ekari 248 za mazao mashambani kufuatia mvua iliyonyesha Februari 5 mwaka huu.
Akikabidhi msaada huo Mkuu wa wilaya ya Mbeya Evance Balama alisema kutokana na hasara iliyotokana na mvua hiyo ambayo iliharibu mazao ambayo ni mahindi ekari 122, maharage ekari 96, kahawa ekari 17.5,migomba ekari 10 na nyanya ekari 2 ambazo jumla yake ni ekari 248,
Alisema wilaya haita weza kufidia hasara yote hiyo isipokuwa waliona ni vema wakatoa mbegu za maharage ambazo zinaweza kustawi kwa kipindi hiki tofauti na mazao mengine ambayo msimu wake umeshapita.
Aidha halmashauri hiyo ilitoa mbegu za maharage zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tano ambazo zitagawiwa kwa wakazi 369 walioathirika na mvua hizo ambapo kila mtu atapata debe mbili za mbegu sawa na kilo 40.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo hilo Mchungaji Lackson Mwanjali alitoa msaada wa mbolea ya kupandia yenye jumla ya shilingi milioni moja ambayo pia kila mwananchi atapata kilo 10 za mbolea hiyo.
Afisa mazao wa wilaya hiyo Maselina Mlelwa aliwaasa wakulima hao kutouza mbegu hiyo kwa kuwa ilikuwa imekwa dawa ya kuulia wadudu hivyo haifai kuliwa wala kufanyiwa biashara ya aina yoyote.
“kile kidogo tulichokipata tukitumie kwa njia za kitaalamu kwa njia bora za kilimo kwa kutumia wataalamu hawa tulionao lakini hizi mbegu hazifai kuliwa kwa kuwa zimewekwa sumu lakini mkitumia vibaya mtakuwa mnafanya vibaya na kusababisha njaa baadaye,” alisema afisa huyo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanakijiji Mwenyekiti wa kijiji hicho Rashidi Mwanyiru aliwashukuru sana viongozi wa halmashauri kwa msaada huo na kusisitiza kuwa hicho kidogo walichokipata watatumia vizuri kwa kile walichoelekezwa na wataalamu wa kilimo na mazao.
Aliongeza kuwa anawaomba wahisani wengine kuonesha mfano kama walivyo fanya viongozi wa halmashauri hiyo kwa kutoa msaada kwa wathirika wengine wanapopata
matatizo na siyo kuisubuli serikali pekee.
Na Venance Matinya wa Kacometa
No comments:
Post a Comment