Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, November 16, 2011

Makala Maalum ya Mkoa wa Mbeya: Jiji la MBEYA, Watu na Jiografia ya Uchumi.


Napenda kuanza kwa kuzingatia  mizania ama tafakari ya kijiografia zaidi ili wote wapate kunielewa kwa haraka, wengi wapenda maendeleo ya Jiji la MBEYA watanielewa  kwa umakini wangu katika nyanja hii ya Jiografia ya Uchumi ili kutambua lulu/dhahabu/ubora/umuhimu wa  jiji la Mbeya ndani Tanzania ambalo mungu kwa makusudi yake ameamua liwe hapo na si kwingine, lakini kimantiki nazama kwa kina kulizungumzia jiji la Mbeya katika medani ya Jiografia ya Uchumi na fursa za kimaendeleo katika  Jiji na Mbeya  kama Mkoa kwa ujumla wake. Mwendo wa kifua mbele macho zaidi ya mita mia moja yaani bila ya shaka yoyote ndio mwendo wa watu wake, hii ni kijivunia kila mtu Tanzania na Duniani kote anatambua kuwa Mbeya ni mkoa Imara, thabiti na makini katika Nyanda za juu kusini mwa Tanzania, nikiwa na maana ni mkoa  kiungo katika Uchumi na hata medani za kimaendeleo katika eneo hili la nyanda za juu kusini, ukilinganisha na majirani zetu ndani ya Tanzania yaani Rukwa, Iringa, na Ruvuma na hata kwa nchi zinazopakana na Tanzania yaani Malawi, na Zambia bado unakuta Jiji hili la kusini magharibi mwa Tanzania linachangamoto kubwa zaidi za kiushawishi katika kukua na kushamiri kwa jiografia ya  uchumi na huu ni ukweli usiohitaji utafiti wa kisayansi.

Ukweli usiopingika  Mbeya ni Jiji pekee  ndani ya Tanzania linalopakana na lenye mahusiano kiuchumi  ya moja kwa moja na nchi mbili [Zambia, Malawi] au tatu [DRC] kwa watu wake usafiri kwa njia ya barabara ili kufanya biashara  hasa kununua kutoka kwetu MBEYA. Fursa hii katika Jiografia ya Uchumi  utaanza kuelewa kuwa mahali lilipo JIJI la MBY ni kitivo cha maendeleo ya uhakika kwa Serikali ya Jiji, wana MBY, Wafanyabiashara yoyote ile, Asasi za elimu kuanzia Sekondari hadi Vyuo Vikuu, ukweli ni kwamba Dunia ya leo ukiwa na uhakika wa soko wewe ndio mfalme. Jiji la Mbeya linategemewa kwa takribani  asilimia 35 ya maisha ya Wakazi wa Kongo upande wa Mashariki - DRC  kiuchumi na biashara, Kaskazini mwa Malawi wanategemea zaidi uimara wa biashara ndani Jiji la Mbeya bila ya kusahau Zambia Kaskazini, na sema haya kwa ukweli usiopingika biashara za TUNDUMA na KASUMURU misingi ya kuimarika kwake ni Jiji la MBEYA. Changamoto yetu ni ukosefu wa takwimu sahihi za shughuli za uhamiaji, biashara za ndani na zile zinazovuka mipaka katika eneo hili ndio maana haya ninayoeleza hayako bayana, sio tu kwa wafanyabiashara na wakazi ili watambue fursa zilipo kwenye jiji la! Bali hata Serikali ya Jiji, Wanasiasa hawalijui hili au kutotilia mkazo nafasi hii hili kujenga Uchumi.

Mbeya na dunia ya leo, wote tunafahamu England ndio mwanzilishi wa maendeleo ya tekinolojia na ustarabu wa kijamii na kusambaa barani Ulaya kote, ni wazungu hao hao walianzisha na kuijenga Marekani[USA] kama sehemu yao yakushamiri kimaendeleo ya uchumi. Baada ya Vita ya Pili ya Dunia Marekani ilisaidia Japan na Ulaya kuboresha uchumi wake katika mpango makini uliojulikana kama [Marshal Plan]. Dunia ya leo tunazungumzia maendeleo ya kasi katika nchi kama China, Afrika ya Kusini,Korea ya Kusini, Brazil na India, wengi wataanza kusema yaani huyu bwana anataka kufananisha MBY na huko kwenye hizo nchi ukweli sio hivyo kabisa bali ni kuonesha nafasi ya MBY kijiografia na maendeleo ya Dunia kiuchumi [ The Global Shift of Capitalist Economy]. Nasema haya kwa sababu ‘South Africa’ ni nchi pekee yenye uchumi imara na thabiti Afrika na imezizidi hata baadhi ya nchi za Ulaya kama Portugal, Greece, Turkey hata Poland, lakini kwa Tanzania nchi hiyo ndio mwekezaji namba moja,  kwa Jiji la MBY ndio jiji pekee kijiografia unaanza kuligusa kama unakuja Tanzania  kwa barabara toka Durban, hivyo itambulike kwa ukaribu huu kunafursa kubwa tena kubwa zaidi kujenga mahusiano na ushawishi wa kiuchumi baina yetu na wawekezaji wa South Africa, kuanzia mwaka 2005 tumeshudia ukiondoa  Benki zetu tatu jijini MBY tulizozizoea yaani kwa majina na utendaji [ NMB,NBC,CRDB], sasa idadi ya banki za kigeni mbazo zote misingi yake ni Afrika ya Kusini hapa Jijini Mby imeongezeka kwa kasi ya mwanga wa radi, nakupa kazi wewe mwenyewe unayesoma waraka huu anza kuhesabu tena anza na ile ambayo  mimi binafsi nilishiriki kuhakikisha inakuja MBY tena inajengwa kwenye eneo makini kabwe stendi- Barclaybank,mkabara na ‘TUCTA ECONOMIC SITE’. 

Hali ya hewa ya MBY, kwa kuwa jiji la MBY liko nyanda za juu kusini ambapo hari ya hewa binafsi napenda iitwe tamu yaani nzuri kifani kwa mtu yoyete anayependa afya yake ataipenda, ni hali inayovutia mtu awaye yoyote kujisikia kuwekeza na kuishi. Mtakumbuka Jiji la Mbeya kulikuwa na Wageni wengi toka nchi za Scandnavia katika miaka ya 1990 wengine waliishi Veta  na wenginge BLOCK T, kwenye nyumba sasa tunaziita za TANROADS hii ni kutokana na mradi mkubwa wa nchi za Scandinavia baada ya wao binafsi kukubali hari ya hewa  na kuona ni mahala pa zuri kwa kuishi, na walianza kufanya mengi makubwa kupitia miradi yao ya maendeleo. Wengi mtakuwa mashahidi na wala sijambo geni Jijini Mbeya kuona dereva mwanamke anaendesha gari  la taasisi kubwa hata Serikali,  hari hii ilitokana na mradi huo ambao ulipanga kufanya mengi makubwa kwa jiji la MBY, huu ulikuwa mpango kabambe na mzuri sana lakini ulififishwa na hari ya  kutokea mara kwa mara wimbi la ujambazi na ubakaji wa wageni hasa Wazungu kwa wakati huo inasikitisha na imeiweka MBY kwenye ramani mbaya sana na nchi za Scandinavia kama wadau wa maendeleo, ni vigumu kwa sasa kuona nchi za Scandinavia zinasaidia MBY katika mipango ya maendeleo, lakini bado tuna nafasi ya kushirikiana nao kwa mtazamo na mahusiano mapya ili tujenge MBY mpya. Nasema haya kwa kuwa tupo kwenye dunia mpya kabisa, WaMBY Wapya na Jiji Jipya mambo ya historia na mambo ya kale yamepita, yale maisha ya kumsifu mtu kuwa mbabe  kwa uwezo wake wa kufanya ujambazi, uhalifu, na uharamia wanao athirika ni jamii ya wana JIJI la MBY, ninapata imani kubwa kuona kila kijana MBY anajishughulisha kibiashara najua uwezo wa kununua  kwa wakazi ni mdogo kutokana na vipato vyetu,  tuangalie jinsi tutakavyoweza kushirikiana na wageni ili tunyanyue uchumi na kujenga jamii yenye uchumi imara, kwa kuwa kwenye uchumi imara jinai haina nafasi na kwenye jinai hakuna uchumi utakaojengwa.

Miundo Mbinu kama changamoto ya kimaendeleo, leo nafurahi kushiriki kwenye hii blog ‘MBEYA YETU’ kwa kuwa maendeleo ya mawasiliano sasa ndio ajenda kuu ya kukuza uchumi wa Dunia, swala la kupata taharifa kupitia mitandao ndio dunia ya leo: magazeti yamepitwa na wakati hata nchi zilizoendelea magazeti yanagawawiwa bure kwenye kampeni kwa kuwa sio biashara tena, mambo yote ni blog nasema ongereni tena na tena. Hili kukuza uchumi wa jiji la MBY lazima haya yatekelezeke kwa haraka zaidi, Uwanja wa ndege Songwe utawezesha Wafanyabiashara kuanzisha fursa mpya na kugeuza  mfumo wa kibiashara na  kuthibitisha kuwa Jiji MBY ni kitivo cha jiografia ya uchumi kwa Mikoa ya nyanda za juu kusini na  nchi jirani zetu, Napenda kupongeza Benk zote kwa namna moja au nyingine zilizoamua kuweka na kudumisha miundo mbinu yao Jijini MBY. Ni vema kuzitumia kwani hakuna Uwekezaji kibiashara bila benki kama chombo cha kushamirisha uchumi, Pili upimaji wa Viwanja na ujenzi wa miundombinu ni shabaha ya kujenga jiji la kisasa kwani ukweli usiopingika Jiji MBY linaathiriwa na ujenzi holela hii ni hatari sana sana sana kwani ndio chanzo cha matatizo yote ya kijamii, uchumi na kisiasa. Kwa kuzingatia hata mgogoro ulioitwa wa Machinga na Jiji  kiini chake ni kuyumba kwenye eneo hili la miundombinu ya jiji, nakumbuka ilikuwa changamoto kubwa kupata kibali cha Kujenga ‘TUCTA ECONOMIC SITE’ ambayo mnaiita Kitega Uchumi cha OTTU  pale Kabwe stand, nafahamu ugumu tulioupata kufanya kazi hile hasa kibali cha ujenzi  na harakati za uvamizi wa eneo hilo toka kwa watu bianafsi wenye ubinafsi wa nafsi na wasio makini kwa maendeleo ya JIJI la MBY, nasema haya mimi ni sehemu wanzilishi na utekelezaji wa  Wazo hilo mwaka 2007 nikiwa Mwalimu wa Sheria za Kazi pale Chuo cha Wafanyakazi [Tanzania Labour College] zamani chuo cha OTTU, wewe unayesoma  waraka huu utaona sasa ajira zilizopatikana pale,uwekezaji uliofanyika pale kweli panastahili heshima na pongezi kwa wote walishiliki, jengo linavutia na kupamba Jiji la Mbeya hili ni swala la shauku kwa kila mmoja wetu kutambua  maendeleo ya uchumi na kijamii ni swala la kimiundo mbinu na si vinginevyo.

Kwa kuhitimisha napenda sema yafuatayo kwa wana jiji la MBY, dunia imebadilika sana na hili ni kutokana kukua kwa kasi kwa mfumo wa ubebari katika nchi zinazokuwa kwa kasi ya ajabu sana kama China na Afrika ya Kusini kwa Afrika, hivyo tutarajie wageni wengi kushiriki nasi katika uchumi. Hii ni changamoto kwa vijana wa MBY, Serikali ya Mkoa, Jiji, Wanasiasa  na Wafanyabiashara wote kwa ujumla tuweke shime ya kulijenga jiji la MBY kimiundo mbinu, sehemu za makazi, barabara zenye nafasi, maeneo maalumu ya biashara  sio kila kwenye barabara tutafanya biashara lazima tubadilike na kukubali kuwa ni jiji pekee linaloweza kupanga ni muundo gani wa shughuli za kibiashara na zifanyike wapi? Ukweli  tunahitaji soko huru na sio holela, najua wapo watu wenye nia mbaya wanapenda holela ili wanufaike na mfumo holela, hatuwezi kwenda hivyo kama tumelikubali  na tuna nia njema kwa JIJI MBY na vizazi vijavyo. Basi bado tunayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya Kiuchumi jijini MBY kwa kuruhusu sheria na taratibu kuchukua nafasi yake si vinginevyo, kwa kuwa haki inakuwa tamu badala ya wajibu kutimizwa, lazima tufahamu Tanzania ndio nchi pekee inayoangaliwa kiuchumi wa maendeleo toka kwa makampuni makubwa hata mataifa makubwa mfano katika kutekeleza haya ni nchi pekee Rais wa USA kulala siku nne nje ya White House kwa lengo la kustadi muundo wa kuboresha mazingira ya kiuchumi Tanzania, hivyo badala ya kuandamana kwa mapambano ya mabomu ni vema tuandamane kutafuta maendeleo kwa kuchangisha fedha za ujenzi wa masoko, miundo mbinu ya maji na kuanzisha SACCOS. Ukweli ni amani pekee iliyo na nguvu  katika jiografia ya uchumi, Shime Serikali Kuu, shime Jiji, shime wanasiasa, shime vijana, shime wadau wa maendeleo Jumuiya ya Ulaya, Shime USA, Shime nchi za Scandinavia,Shime Japan, Shime China, ShimeKorea ya Kusini na Shime Africa ya kusini njooni tujenge jiji la MBY kwa kuwa ni sehemu muhimu kwa maendeleo ya uchumi na maisha ya watu wote kuishi.

                                          Imeandikwa na 

Edwin, Mwakyembe.

No comments: