Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki-Chadema,Mheshimiwa Tundu Lissu, akitangaza kwamba wananchi wake hawatachangia michango yoyote ikiwemo ya maendeleo ya jimbo hilo.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro mkoa wa Arusha-CCM ,Mheshimiwa Ole Sendeka akitoa nasaha zake dhidi ya hoja ya Tundu Lissu kukataza wananchi kuchangia maendeleo yao.
Diwani wa kata ya Msange Singida Kaskazini Elia Digha, akichangia hoja ya Tundu ya kukataza wananchi kuchangia maendeleo yao.
Diwani wa kata ya Dung’unyi jimbo la Singida Mashariki Buno Natalias,akikosoa sera ya mbunge Tundu ya kukataza wananchi wasichangie maendeleo yao.
Mbunge Tundu Lissu,akifuatilia kwa makini makombora yaliyokuwa yakirushwa kwake kwa kitendo chake cha kuzuia wananchi kuchangia maendeleo yao.
---
Habari hii na Nathaniel Limu
MBUNGE wa jimbo la jimbo la Singida mashariki-Chadema ,Mheshimiwa Tundu Lissu,ameendelea kuwasha moto baada ya kuagiza tena,kwamba hakuna michango ya aina yo yote itakayochangwa jimboni kwake na kiongozi au mtendaji atakayethubutu kuchangisha, kitakachompata,asije akalaumu mtu.
Moto huo ameukoleza tena mwishoni mwa wiki hii wakati akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida vijijini.Akionekana kujiamini ,Tundu alisimama na kusema“Mwenyekiti,naomba nirudie tena na tena,kwamba wananchi wa jimbo langu hawatachangia mchango wo wote na atakayethubutu kuchangisha,atakiona cha moto”.
Akifafanua zaidi, amesema sababu kuu ya kutoa katazo hilo, ni kwamba hakuna po pote iwe kijijini,kata,halmashauri ya wilaya au hata serikali kuu yenyewe kunakoainisha sheria ya kumlazimisha mwananchi kutoa michango ukiwemo wa maendeleo.
Wakati akiendele kutoa ufafanuzi wake huo,madiwani na hasa wa CCM ambao wako 263 dhidi ya sita wa CHADEMA,zaidi ya robo tatu mikono yao ilikuwa juu ikiomba nafasi ya kujibu mapigo huku baadhi wakitamka “mwenyekiti kwa taarifa”.
Waliochangia kukosoa sera ya Tundu Lissu ya kupiga wananchi kuchangishwa michango,ni pamoja na diwani wa CCM kata ya Dung’unyi jimbo la Singida mashariki,Buno Natalis.Alianza kwa kusema “mwenyekiti,huyu diwani mwenzangu Tundu Lissu, ni mwongo,jimbo la Singida mashariki sio lake,ni letu sote madiwani tulioko madarakani hadi 2015″.
Amesema Tundu hawatembelei wananchi ipasavyo kujua matatizo na kero zinazowakabili,kazi zote huwaachia madiwani wa kata ambao hana ushirikiano nao wa kukidhi haja.Natalias alisema Tundu amechafua hali ya hewa jimboni, kwani hata michango ya asilimia tano inayotakiwa na benki ya dunia ili wananchi waweze kuchimbiwa visima,wananchi wamegoma hawachangii.
Wanaoumia ni wananchi lakini mheshimiwa Tundu, yeye anaendelea kunywa maji safi na salama ya ndani ya chupa.
“Mpango wa Chakula Duniani (WPF) unaosaidia chakula kwenye shule zetu za msingi, wananchi wamepewa jukumu la kuchangia vitu vichache ili wanafunzi wapate chakula cha mchana bila matatizo,huko nako Tundu kawakataza wasichangie”,alisema Natalias kwa masikitiko makubwa.
Naye diwani wa kata mpya ya Msange,Elia Digha, alimwomba Tundu kufuta kauli yake hiyo kwa madai kwamba imejaa vitisho na kama hafuti,basi misaada yote yenye masharti ya kutaka wananchi nao wachangie sehemu ndogo,ihamishwe na kupelekwa mahali wananchi wako tayari kuchangia.
Mbunge wa jimbo la Kiteto mkoani Arusha,Christopher Ole Sedeka,ambaye alikuwa amefuatana na naibu waziri wa viwanda na masoko na ambaye ni mbunge wa jimbo la Singida kaskazini,Lazaro Nyalandu,alimwomba Tundu atafakari upya uamuzi wake huo wa kukataza mwananchi kuchangia maendeleo yao.
Sedeka aliliomba baraza hilo la madiwani,kuangalia uwezekano wa kuchagua baadhi ya madiwani ambao watakaa na Tundu Lissu wamwelimisha juu ya umuhimu wa wananchi kuchangia maendeleo yao.
“Ndugu zangu na majirani zangu,mahali kuna mafarakano,hapo tena maendeleo ya kweli yanakuwa ndoto,hakikisheni mnaondoa doa hilo,kaeni na Tundu ili mweze kufikia muafaka utakaowanufaisha wananchi wa halmashauri yote ya wilaya ya Singida vijijini”alisema mbunge huyo na kushangiliwa kwa nguvu na madiwani.
Baada ya mapigo hayo, Tundu alipewa nafasi ya kujibu na aliposimama alisema “Mimi sio kichaa, na hakuna mahali po pote palipoandikwa kwamba niliwahi kuugua kichaa,kwa hiyo ninayoyasema nimeyafanyia uchunguzi wa kina na kubaini kuwa michango yote inayochangishwa jimboni kwangu,haipo kisheria”.
Amesema mbaya zaidi ni kwamba tangu michango ianzwe kuchangishwa,hakuna hata mwaka moja wachangiaji wamesomewa mapato na matumizi.
“Nina ushahidi wa kimaandishi,kwamba katika kata ya Kinyeto,michango ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata,iliwahi kutumiwa kuchangia harusi ya mbunge Lazaro Nyalandu, na zingine walipewa wajumbe wa CCM kwa matumizi ya nauli ya kwenda kuhudhuria kikao Singida mjini.
Wakati mbunge Tundu Lissu,akiwakataza wananchi wake kuchangia maendeleo yao,tayari mwanachama moja wa CHADEMA jimboni kwake, hivi sasa anatumikia jela miezi sita kwa kosa la kuvunja geti linalotumiwa na halmashauri hiyo, kudhibiti ushuru wa mazao ya misitu.
Pia Diwani wa CHADEMA kata ya Mungaa na baadhi ya wananchama wa chama hicho,wanakabiliwa na kesi mahakamani kwa tuhuma ya kuvunja ‘geti’ la kudhiti ukwepaji wa ushuru wa mazao ya misitu, na kumpiga vibaya mlinzi wa geti hilo.Kesi hiyo iliyopo mbele ya mahakama ya mkoa,inasimamiwa na Tundu Lissu.
No comments:
Post a Comment