Na Anna Nkinda – Putrajaya, Malaysia
21/6/2011 WATOTO wenye vipaji maalum kama watalelewa na kutunzwa katika mazingira mazuri nchi itazalisha wataalamu wengi wenye ujuzi wa kutosha na hivyo kuondokana na tatizo la kutegemea wataalamu kutoka nje na nchi.
Hao yamesemwa jana na Mke wa Waziri Mkuu wa Malaysia Mama Datin Paduka Seri Rosmah Mansor wakati akiongea na wake wa viongozi kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Zambia walipotembelea shule ya Sekondari ya watoto wenye vipaji maalum ya Pusat PERMAT – Apintar iliyoko mjini Putrajaya.
Mama Datin ambaye ni mlezi wa shule hiyo alisema kuwa alipata wazo la kuanzisha shule hiyo baada ya kuona kuwa vipaji vingi vya watoto vinapotea bila ya kufanyiwa kazi jambo ambalo linasababisha taifa kukosa wataalamu wa ndani hivyo basi akaamua kuamua kulea vipaji hivyo.
“Watoto wengi wenye vipaji maalum ambao wanatoka katika familia maskini wanapata tabu ya kwenda shule na hata wengine hawasomi kabisa kwa kukosa ada jambo ambalo linawafanya wapoteze vipaji vyao.
Kutokana na tatizo hilo niliamua kuanzisha shule hii ili tuweze kuvilea na kuvitunza vipaji vya watoto wetu ambao hapo baadaye watakuwa wataalamu wazuri na hivyo kuongeza nguvu kazi ya taifa,”alisema.
Kwa upande wake Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alisema kuwa kufika kwao katika shule hiyo wamejifunza mengi na kutambua kuwa vipaji vya watoto vinatakiwa kutunzwa tangu wakiwa wadogo la sivyo vinaweza kupotea .
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa nchini Tanzania kuna shule za Sekondari za watoto wenye vipaji maalum lakini tatizo lililopo ni ukosefu wa walimu na vifaa vya kufundishia.
“Tofauti iliyopo ni kuwa nyie mnavitambua, kuvitunza na kuvilea vipaji vya watoto tangu wakiwa na umri mdogo wa miaka tisa hadi 16 ila sisi tunavitambua na kuvilea kuanzia umri wa miaka 13 pale ambapo mtoto atakuwa amemaliza elimu ya msingi na kufaulu kwa kiwango cha juu mitihani ya Taifa hapo ndipo mtoto huyu atajiunga na shule ya sekondari ya vipaji maalum,”alisema Mama Kikwete.
Naye Mkurugenzi wa shule hiyo ambayo inaandaa wataalamu mbalimbali Prof. Dk. Noriah Mohd Mohd Ishak alisema kuwa ili kuwalea watoto hao ni lazima uwe na saikolojisti aliyesomea mambo ya vipaji ambaye atakuwa mshauri kwani watoto wenye vipaji maalum wanamazingira yao ya kuwatunza na kuishi.
Aliendelea kusema kuwa masomo yanayofundishwa katika shule hiyo ni ya sayansi na hivi sasa kuna jumla ya wanafunzi 116 kila darasa lina wanafunzi 16 hadi 17 na uwiano wa kufundisha uliopo ni kuwa kila mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi nane na muda wa mwanafunzi kukaa darasani ni masaa tisa na nusu.
Dk. Noriah alisema, “Huwa kuna program maalum ya kuwasaidia watoto wakati wa kipindi cha likizo (summer) ambapo watoto kutoka ndani na nje ya Malaysia wanafanya mitihani ya kujiunga na shule hii kama mtoto akiwa amefaulu anakuja kusoma ili aweze kukuza kipaji alichonacho na baada ya kumaliza kupata mafunzo hayo anafanya tena mitihani ili kuona kama ameimarika na program hiyo au la”.
Nchi hiyo yenye watoto wenye umri wa mwaka 1 hadi 15 milioni 8.9 kwa kutumia wataalamu wa vipaji walitambua kuwa kati ya watoto laki moja kuna mtoto mmoja mwenye kipaji maalum na baada ya watoto hao kumaliza elimu ya sekondari wanajiunga na elimu ya juu ili waweze kuandaliwa zaidi kwa kuwa wataalamu wa fani mbalimbali ikiwemo udaktari na uinjinia.
No comments:
Post a Comment