Waziri Mkuchika akihutubia wananchi wa Kata mpya ya Igombwe Singida vijijini.
Mkuchika akiweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Kata mpya ya Igombwe Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Waziri Mkuchika akikabidhiwa kibuyu na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Joram Alute kama ishara ya kukaribishwa kwenye Kata mpya ya Igombwe singida vijijini wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani Singida.
Mmoja wa wanakikundi cha ngoma cha kijiji cha Igombwe akiruka sarakasi wakati wa sherehe hizo.
Hii ni ngoma ya kisukuma ikisakatwa na wanakikundi cha ngoma.
Waziri wa TAMISEMI George Mkuchika akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya tamko la serikali la kuwataka wasiambatane na kamati mbalimbali za maendeleo mkoani Singida .
******************************
Na Hillary Shoo,
Singida.
SERIKALI imesema waandishi wa habari hawaruhusiwi kuambatana na wajumbe wa Kamati mbalimbali za halmashauri za Wilaya, Manispaa na Miji wakati wa kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI,George Mkuchika aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Singida wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili.
Waziri Mkuchika amesema vikao vya Kamati hizo ni shughuli za faragha hivyo si ruhusa kwa mtu yeyote asiyekuwa mjumbe wa kamati hizo kuhudhuria vikao hivyo ama kuambatana kwenye kukagua miradi ya maendeleo.
Amesema waandishi wa habari na wananchi wengine wa kawaida watapata taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo kwenye kikao cha Baraza la madiwani ambacho ni kikao cha wazi kwa mtu yeyote kuhudhuria.
Hata hivyo baadhi ya waandishi wa habari wamesema kuwa licha ya kukosa picha za miradi husika kwa ajili ya magazeti na Runinga kitendo hicho kinawanyima fursa ya kufahamu kwa undani mapungufu mbalimbali yanayojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia kuwa wao ndiyo jicho na kioo cha jamii.
Wakati kamati za halmashuri zikizuiliwa, kwa upande wa Kamati mbalimbali za Bunge ambazo pia hufanya vikao vya faragha, zimekuwa zikiruhusu kuambatana na Waandishi wa habari wakati wa kukagua miradi ya maendeleo.
Habari kwa hisani ya Mo Blog
No comments:
Post a Comment