Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, March 31, 2016

KYELA YAJIPANGA KUDHIBITI KIPINDU PINDU


Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dk. Thea Ntara akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi katika operesheni ya kukagua usafi wa mazingira ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu


Afisa Afya Wilaya ya Kyela, Geophrey Baroshi akionesha aina ya pombe zilizopigwa marufuku kutumiwa na watu hapa nchini ambazo zilikutwa katika maduka zikiuzwa wilayani Kyela.

Mkuu wa Wilaya akisimamiazoezi la kukagua  aina ya vinywaji vilivyopigwa marufuku kutumiwa nchini

Baadhi ya Wananchi wakishiriki katika usafi wa mazingira

Baadhi ya vialabu vya pombe za kienyeji vikivunjwa kutokana na kutokudhi vigezo ikiwemo ukosefu wa vyoo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imeweka utaratibu kwa wananchi wake kuhakikisha wanaepukana na magonjwa ya kuambukiza hususani kipindupindu kwa kuwataka kila kaya kujenga vyoo.

Kutokana na agizo hilo Watu 17 wakazi wa Kijiji cha Lusungo Kata ya Lusungo  wamekamatwa kwa kutokuwa na vyoo na uchafu wa mazingira uliosababisha  kuzorotesha juhudi za kupambana na ugonjwa wa kipindupindu Wilayani humo.

Juhudi hizo zimekuja  baada ya ugonjwa huo kudumu kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo Kata ya Lusungo na Ndobo ndizo pekee ambazo bado zina wagonjwa wa kipindupindu hali iliyomfanya Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dk. Thea Ntara kupiga kambi Kata ya Lusungo ili kufanya ukaguzi wa vyoo na usafi wa mazingira.

Akizungumza na gazeti hili katika ukaguzi huo, Mkuu wa Wilaya, Dk. Ntara alisema anakwamishwa na Diwani wa Kata ya Lusungo Veronica Kanyanyila na Mwenyekiti wa Kijiji Zawadi Lugano Mwangojola ambao wamekuwa wakidai ugonjwa huo umesababishwa na imani za kishirikina na si uchafu au ukosefu wa vyoo.

Katika oparesheni hiyo maalumu iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya aliyeambatana na Maafisa wa Afya pia iliyakumba maeneo mbalimbali kama Kata ya Ikama na Kijiji cha Tenende ambapo alilazimika kuvunja Kilabu cha pombe Kata ya Ikama baada ya kuwakuta wakazi wa eneo hilo wakinywa pombe za kienyeji katika mazingira machafu.

Mbali ya ukaguzi huo pia Mkuu wa Wilaya alishuhudia baadhi ya wananchi wakinywa pombe ya moshi na pombe zilizopigwa marufuku kutoka nchi jirani na kulazimika kuwakamata wahusika ambao wamefikishwa kituo kikuu cha Polisi Wilaya ya Kyela ambapo pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Pia Mkuu huyo wa Wilaya  aliteketeza sindano zinazodhaniwa kutumika kwa ajili ya kujidunga na watumiaji wa  madawa ya kulevya katika Kata ya Ikama na ambapo alitoa agizo la kuwasaka wauzaji wa madawa hayo na wanaouza pombe zilizopigwa marufuku kutoka nchi jirani.

Kwa upande wake Afisa Afya Wilaya ya Kyela, Geophrey Baroshi alisema  zoezi hilo ni endelevu na watahakikisha kila kaya ina choo na kuwa na mazingira safi kwa muda wote ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huo Wilayani Kyela na kwamba waliokamatwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mtendaji wa Kijiji cha Lusungo Fadhili Sade alisema  wamefanya ukaguzi katika kaya 681 za kijiji hicho na zote hazina vyoo hali inayofanya mapambano ya kipindupindu kuwa magumu mno kwani wengi wao wamekuwa wakiamini ugonjwa huo unatokana na ushirikina.

Naye Mtendaji wa Kata ya Lusungo Stephen John alisema wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa Diwani wa Kata na Mwenyekiti wa kijiji kuwa aache kutangaza kuwa Kata hiyo inakabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu kwani ndiyo kunachochea kuongezeka kwa ugonjwa huo ambao unatokana na ushikina na si uchafu au ukosefu wa vyoo.


No comments: