-Asema
TBL Group ni tanuru la kuendeleza vipaji
Ukifika mkoani Mbeya eneo la Iyunga kilipo
kiwanda cha kutengeneza bia cha Tanzania Breweries Limited (TBL) tawi la Mbeya
na kufanikiwa kuingia kiwandani hapo utajisikia uko eneo tofauti kutokana na
mandhari utakayokutana nayo.
Mwonekano wake kuanzia majengo ya
kiwanda chenyewe, wafanyakazi ambao wengi wao ni vijana, mazingira ndani
ya kiwanda na yaliyokizunguka bila kusahau mitambo ya kisasa ya
uzalishaji iliyopo kiwandani hapo utakubaliana kwamba huo ndio uwekezaji
unaotakiwa.
Kiwanda cha TBL ni miongoni mwa viwanda bora
vya kutengeneza bia barani Afrika ambacho kinaongozwa na msomi wa kitanzania
mwenye fani ya Uhandisi katika fani ya umeme wa viwandani, Mhandisi
Waziri Jemedari.
Katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni
Mhandisi Jemedari anasema anaipenda kazi yake na anajisikia furaha kuongoza
kiwanda kikubwa kama hicho ambacho ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza
bia katika bara la Afrika kikiwa kimeajiri zaidi vijana wasomi wa kitanzania
ambao wanamudu vyema kazi zao.
“Kiwanda hiki ni miongoni mwa viwanda bora vya
kutengeneza bia barani Afrika na kina rekodi ya kushikilia nafasi ya kwanza kwa
kuwa kiwanda bora, hivyo unapokuwa kiongozi wa kiwanda kama hiki unatakiwa
kuhakikisha viwango vyake katika sekta zote vinabaki kuwa juu, kazi ambayo
naifanya kwa kushirikiana na timu ya wafanyakazi wenzangu wote kuhakikisha
tunaendelea kuweka rekodi nzuri,”.Alisema
Anaongeza kusema Kutokana na historia hii ya
ubora barani Afrika, kiwanda kimekuwa kikiendelea kufanya vizuri na kuvutia
wageni kutoka sehemu mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania ambao
wamekuwa wakitembelea mara kwa mara kujionea mafanikio na kujifunza.
Siri ya kiwanda hicho kuwa bora,
Jemedar anasema kilipoanzishwa kilifungwa vifaa na mitambo ya kisasa ya
uzalishaji vile vile kilianza kutumia kanuni bora za uendeshaji viwanda kwa
njia ya kisasa za kampuni ya SABMiller ambayo ndiyo inamiliki kampuni mama
ya TBL Group.
Anasema kanuni hizi zinazojulikana kitaalamu
kama The Manufacturing Way zinaelekeza mfumo wa uzalishaji bora
wenye viwango na wenye kuleta tija, na kugusa maeneo yote ya uendeshaji
viwanda kwa ufanisi wenye kuleta matokeo bora na zikifuatwa na kutekelezwa
ipasavyo lazima matokeo yake yawe mazuri na mafanikio yapatikane.
“TBL Group hivi sasa inatumia kanuni hizi
katika viwanda vyake vyote na matokeo yake yanaonekana kuanzia kwenye uchangiaji
wa pato la taifa kupitia kodi,kuwa mwajiri bora,kusaidia masuala mbalimbali ya
kijamii,kuwezesha wakulima wanaouzia kampuni malighafi za kutengenezea
vinywaji,kuzingatia kanuni za usalama kazini,kupunguza tatizo la ajira nchini
na mengineyo mengi”.Alisema.
Pia anasema mfumo huu unaenda sambamba na
kampuni kuajiri vijana wa kitanzania ambao wanapatiwa fursa ya kuonyesha vipaji
vyao na wanaendelezwa kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ambapo wanafanya kazi kwa
ufanisi na kuleta matokea mazuri “TBL Group ni tanuru la kuendeleza vipaji na
ina mfumo wa kuajiri wafanyakazi waliobobea kwenye fani mbalimbali ambao
wanaendana na viwango vya kampuni na mchango wao na ufanisi wao katika kazi
kuongeza mafanikio.
Kuhusu historia yake, Jemedari
anasema ni Mzaliwa wa mkoani Mara ambaye alipata elimu ya
msingi na sekondari na baadaye kujiunga na.Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako
alisomea shahada ya kwanza ya Uhandisi wa umeme.
Mbali na shahada ya Uhandisi akiwa
mwajiriwa wa TBL amehudhuria kozi mbalimbali nje ya nchi ambazo zimezidi
kumpatia maarifa katika fani yake na kumfanya awe miongoni mwa wahandisi nguli
wanaoaminika nchini katika fani ya umeme wa viwanda hususani vinavyozalisha
vinywaji.
Baadhi ya kozi ambazo zimemnoa zaidi kitaalamu
alisema kuwa alizipata katika nchi za Afrika ya Kusini na nchini
Ujerumani bila kusahau mafunzo ya ndani anayoendelea kuyapata kiwandani hapo
kwa sasa.
Kuhusu historia yake ya kazi anasema kuwa
alijiunga na TBL mwaka mwaka 1999 kama mhandisi wa umeme na baada
ya kutumikia kiwanda hicho kwa kipindi kirefu akiwa ameshikilia nafasi
mbalimbali za uongozi kwenye idara yake. Alijiunga na kampuni ya Coca Cola
Kwanza kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi ambako alifanya kazi kazi kwa muda mfupi
na kurejea tena TBL ambako anaendelea kufanya kazi hadi leo akiwa Meneja wa
Kiwanda.
Mafanikio aliyoyapata akiwa mfanyakazi wa TBL
amesema kuwa ni mengi ikiwemo kuhudumia familia yake vizuri pia amejifunza
mambo mengi yanayomsaidia kuendesha maisha na yatakayomsaidia kimaisha
hata baada ya kustaafu kazi.
Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika
kazi yake anasema ni za kawaida na anaamini kuwa hakuna kazi isiyokuwa na
changamoto kinachotakiwa na kuangalia namna ya kukabiliana nazo.
Mbali na kazi yake ya utawala na uhandisi umeme
baada ya saa za kazi anapendelea kusoma vitabu mbalimbali ikiwemo
kujishughulisha na ufugaji “Napenda sana shughuli za ufugaji na mara
nitakapostaafu kazi nitakuwa mfugaji vilevile kujishughulisha na utoaji
wa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na fani yangu ya umeme.
Jemedari anatoa wito kwa vijana wa kitanzania
kutokimbia masomo ya hesabu na sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi
kukomaa nayo kwa kuwa katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila
wataalamu wa kutosha katika nyanja mbalimbali itakuwa vigumu kwa taifa kupiga
hatua ya maendeleo na pindi watakapoajiriwa au kujiajiri wafanye kazi kwa
bidii.
Mwisho
|
No comments:
Post a Comment