Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, February 17, 2016

Waziri Jemedari: Mhandisi nguli wa umeme anayengoza kiwanda cha kutengeneza bia kwa ufanisi

 Mhandisi Waziri akiwa mitamboni



-Asema TBL Group ni tanuru la  kuendeleza vipaji

Ukifika mkoani Mbeya eneo la Iyunga kilipo kiwanda cha kutengeneza bia cha Tanzania Breweries Limited (TBL) tawi la Mbeya na kufanikiwa kuingia kiwandani hapo utajisikia uko eneo tofauti kutokana na mandhari utakayokutana nayo.

Mwonekano wake   kuanzia majengo ya kiwanda chenyewe,  wafanyakazi ambao wengi wao ni vijana, mazingira ndani ya kiwanda na yaliyokizunguka bila kusahau mitambo ya kisasa ya  uzalishaji iliyopo kiwandani hapo utakubaliana kwamba huo ndio uwekezaji unaotakiwa.

Kiwanda cha TBL ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza bia barani Afrika ambacho kinaongozwa na msomi wa kitanzania mwenye fani ya Uhandisi katika fani ya umeme wa viwandani, Mhandisi  Waziri Jemedari.

Katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni Mhandisi Jemedari anasema anaipenda kazi yake na anajisikia furaha kuongoza kiwanda kikubwa kama hicho ambacho ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza bia katika bara la Afrika kikiwa kimeajiri zaidi vijana wasomi wa kitanzania ambao wanamudu vyema kazi zao.

“Kiwanda hiki ni miongoni mwa viwanda bora vya kutengeneza bia barani Afrika na kina rekodi ya kushikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa kiwanda bora, hivyo unapokuwa kiongozi wa kiwanda kama hiki unatakiwa kuhakikisha viwango vyake katika sekta zote vinabaki kuwa juu, kazi ambayo naifanya kwa kushirikiana na timu ya wafanyakazi wenzangu wote kuhakikisha tunaendelea kuweka rekodi nzuri,”.Alisema

Anaongeza kusema Kutokana na historia hii ya ubora barani Afrika, kiwanda kimekuwa kikiendelea kufanya vizuri na kuvutia wageni kutoka   sehemu mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania ambao wamekuwa wakitembelea mara kwa mara  kujionea mafanikio na kujifunza.

Siri ya kiwanda hicho kuwa   bora,  Jemedar anasema kilipoanzishwa kilifungwa vifaa na mitambo ya kisasa ya uzalishaji vile vile kilianza kutumia kanuni bora za uendeshaji viwanda kwa njia ya kisasa za kampuni ya SABMiller ambayo ndiyo inamiliki kampuni mama ya  TBL Group.

Anasema kanuni hizi zinazojulikana kitaalamu kama The Manufacturing Way  zinaelekeza mfumo wa uzalishaji bora wenye viwango na wenye kuleta tija, na kugusa maeneo yote ya uendeshaji  viwanda kwa ufanisi wenye kuleta matokeo bora na zikifuatwa na kutekelezwa ipasavyo lazima matokeo yake yawe mazuri na mafanikio yapatikane.

“TBL Group  hivi sasa inatumia kanuni hizi katika viwanda vyake vyote na matokeo yake yanaonekana kuanzia kwenye uchangiaji wa pato la taifa kupitia kodi,kuwa mwajiri bora,kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii,kuwezesha wakulima wanaouzia kampuni  malighafi za kutengenezea vinywaji,kuzingatia kanuni za usalama kazini,kupunguza tatizo la ajira nchini na mengineyo mengi”.Alisema.

Pia anasema mfumo huu unaenda sambamba na kampuni kuajiri vijana wa kitanzania ambao wanapatiwa fursa ya kuonyesha vipaji vyao na wanaendelezwa kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ambapo wanafanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokea mazuri “TBL Group ni tanuru la kuendeleza vipaji na ina mfumo wa  kuajiri wafanyakazi waliobobea kwenye fani mbalimbali ambao wanaendana na viwango vya kampuni na mchango wao na ufanisi wao katika kazi kuongeza mafanikio.

Kuhusu  historia yake,  Jemedari  anasema  ni Mzaliwa wa mkoani Mara ambaye alipata  elimu ya msingi na sekondari na baadaye kujiunga na.Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisomea shahada ya kwanza ya Uhandisi wa umeme.

Mbali na shahada ya Uhandisi  akiwa mwajiriwa wa TBL  amehudhuria kozi mbalimbali nje ya nchi ambazo zimezidi kumpatia maarifa katika fani yake na kumfanya awe miongoni mwa wahandisi nguli wanaoaminika nchini katika fani ya umeme wa viwanda hususani vinavyozalisha vinywaji.

Baadhi ya kozi ambazo zimemnoa zaidi kitaalamu alisema kuwa alizipata katika  nchi za Afrika ya Kusini na  nchini Ujerumani bila kusahau mafunzo ya ndani anayoendelea kuyapata kiwandani hapo kwa sasa.

Kuhusu historia yake ya kazi anasema kuwa alijiunga na TBL mwaka  mwaka 1999 kama mhandisi wa umeme na  baada ya kutumikia kiwanda hicho kwa kipindi kirefu akiwa ameshikilia nafasi mbalimbali za uongozi kwenye idara yake. Alijiunga na kampuni ya Coca Cola Kwanza kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi ambako alifanya kazi kazi kwa muda mfupi na kurejea tena TBL ambako anaendelea kufanya kazi hadi leo akiwa Meneja wa Kiwanda.

Mafanikio aliyoyapata akiwa mfanyakazi wa TBL amesema kuwa ni mengi ikiwemo kuhudumia familia yake vizuri pia amejifunza mambo mengi yanayomsaidia kuendesha maisha na  yatakayomsaidia kimaisha hata baada ya kustaafu kazi.

Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake anasema ni za kawaida na anaamini kuwa hakuna kazi isiyokuwa na changamoto kinachotakiwa na kuangalia namna ya kukabiliana nazo.

Mbali na kazi yake ya utawala na uhandisi umeme baada ya saa za kazi anapendelea kusoma vitabu mbalimbali ikiwemo kujishughulisha na ufugaji “Napenda sana shughuli za ufugaji na mara nitakapostaafu  kazi nitakuwa mfugaji vilevile kujishughulisha na utoaji wa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na fani yangu ya umeme.

Jemedari anatoa wito kwa vijana wa kitanzania kutokimbia masomo ya hesabu na sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi kukomaa nayo kwa kuwa  katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila wataalamu wa kutosha katika nyanja mbalimbali itakuwa vigumu kwa taifa kupiga hatua ya maendeleo na pindi watakapoajiriwa au kujiajiri wafanye kazi kwa bidii.

Mwisho

No comments: