Mganga mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, mwenye shati la kitenge alipokuwa akichangia mada katika mafunzo yaliyotolewa na Redcross kwa Kamati ya Maafa na Majanga ya Mkoa wa Mbeya. |
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mikoa na Matawi Redcross makao makuu, Julius Kejo, akitoa mada kwa viongozi wa kamati ya maafa Mkoa wa Mbeya katika mafunzo yaliyotolewa na Chama cha Msalaba mwekundu |
Afisa Mahusiano wa Kamati ya kimataifa ya Redcross (ICRC) Nairobi Kenya, Viginia Njiru akiwasilisha mada kuhusu historia ya Redcross duniani pamoja na matumizi ya nembo zake. |
|
KAMATI ya Maafa na Majanga Mkoa wa Mbeya
imekishauri chama cha Msalaba mwekundu nchini(TRCS)kuanzisha ghala la kutunzia
vifaa vya uokoaji na misaada ya dharula mkoani Mbeya.
Rai hiyo ilitolewa na Mganga mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Dk. Seif Mhina, alipokuwa akichangia mada katika mafunzo yaliyotolewa na
Redcross kwa Kamati ya Maafa na Majanga ya Mkoa wa Mbeya.
Dk. Mhina alisema Mkoa wa Mbeya unamaeneo ambayo
yamekuwa yakikumbwa na maafa mara kwa mara lakini juhudi za haraka za kuwafikia
waathirika zinakwama kutokana na ukosefu wa msaada wa haraka.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo ni vema
Chama cha Msalaba mwekundu kikaweka utaratibu wa kuwa na ghala la kuhifadhia
vifaa vya uokoaji na misaada ya haraka mkoani Mbeya.
Alitolea mfano Wilaya ya Kyela kuwa imekuwa
ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara ambapo Kamati ya Maafa na majanga ya mkoa
inakuwa haina msaada wa haraka wa kuwasaidia waathirika na wakiwasiliana na
Redcross mkoa wa Mbeya wanasema msaada hadi utoke makao makuu jambo
linalochelewesha upatikanaji wa misaada hiyo.
Aidha alisema uwepo wa ghala hilo kwa Mkoa wa
Mbeya utasaidia pia kukabiliana na magonjwa ya milipuko inayoanzia nchi jirani
kutokana na Mkoa huo kuwa mpakani.
“Mfikirie kuanzisha ghala kwa sababu ya mkoa
wetu kuwa mpakani ili kuepukana na tishio la magonjwa kama ilivyokuwa Ebola, na
kama tatizo ni ghala Serikali inalo na inaweza ikashirikiana na Redcross
kuhifadhia bidhaa husika” alishauri Mganga Mkuu.
Akijibu Changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo
ya Matawi na Mikoa wa Redcross, Julius Kejo alipongeza kwa wazo na kujitolea
kwa Ghala hilo na kuongeza kuwa Redcross wanautaratibu wake wa kuweka ghala
mahali.
Alisema Redcross makao makuu wapo kwenye
mchakato wa kuangalia namna watakavyoiwezesha ofisi ya Redcross mkoa wa Mbeya
ili iweze kupatiwa ghala la kuhifadhia vifaa vya msaada wa dharula kwa
waathirika wa majanga na maafa.
Aliongeza kuwa mchakato huo hautachukua muda
mrefu kutokana na namna Chama cha Msalaba mwekundu Mkoa wa Mbeya kinavyoshiriki
shughuli za kijamii na kuonesha ukomavu wake chini ya Mwenyekiti wake Ulimboka
Mwakilili.
Aidha alitoa wito kwa Serikali kuipa mamlaka
kamati ya Maafa na majanga ya Mkoa ili kufanya shughuli zake bila kuingiliwa
kama ilivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na dawa(TFDA).
Alisema Kamati hiyo ikiwa na mamlaka kamili
itaweza kupanga mikakati namna ya kujiandaa na majanga kabla hayajatokea na kukabiliana
pindi yatakapojitokeza bila kuchelewa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment