Nianze kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,muweza wa yote kwa rehema
nyingi alizotushushia kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo.
Kwani hatukustahili
zaidi ya wengi waliotutangulia mbele za haki.Nawashukuru ninyi nyote mliofika
kuungana nami katika siku hii muhimu katika kukuza,kuimarisha na kuendeleza
demokrasia ndani ya Chama chetu,Chama Cha Mapinduzi.
Wazee wangu, Waheshimiwa Maaskofu, Viongozi wa Dini na
madhehebu mbalimbali,Waheshimiwa viongozi wa kimila,Waheshimiwa Machifu,akina
mama,vijana,WanaCCM wenzangu,Viongozi wa vyama vya siasa,Wananchi,Wana
Mbeya,Nawashukuru,Asanteni sana kwa uwepo wenu.
Ndugu zangu,
Kwa muda mrefu na kwa njia mbalimbali za mawasiliano mmekuwa
mkinidadisi Mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja nna kwambamliutaja mwaka tu,
lakini niliwaelewa.
Wengi mliushangaa ukimya wangu.Pamoja na na kwamba ukimya ni
sehemu ya haiba yangu na daima nimeupokea kama ni karama aliyonitunuku Mwenyezi
Mungu,Muweza wa yote,baadhi yenu niliwajibu " Ukimya una Kishindo"!
Kuhusu Sultan Qabus wa Oman,mwandishi mmoja maarufu aitwae Robert Kaplan
amemwelezea ifuatavyo: Ni mtu mkimya, mpole, hapendi kuzungumza na waandishi wa
habari mara kwa mara, hapendi habari zake ziandikwe kwenye magazeti mara kwa
mara,lakini ameibadilisha nchi ya Oman kutoka makundi hasimu ya makabila na
kuwa taifa linaloheshimika na linaloendelea kwa kasi sana na kuwa mfano wa
kuigwa...." Sijifananishi na Sultan Qabus, la hasha.Isipokuwa najaribu
kusisitiza kwamba mara nyingi ni bora katika maisha kuwa mjenga hoja na
mtendaji makini kuliko kuwa mpayukaji na
maamuzi ya papo kwa papo yenye matokeo hasi na yenye hasara kwa taifa. Nimeenda
nje kidogo ya mada yangu!
Kwa staili ya siku hizi wagombea watarajiwa huwa tunajitokeza
na kusema : tutatangaza nia siku hii au ile! Nadhani tunawashangaza na mtuwie
radhi.Kwani kwa kusema hivyo tunakua
tayari tumetangaza nia!Basi nami kwa staili hiyo hiyo naomba kutangaza
rasmi mbele ya kadamnasi hii kama mashahidi,kwamba kwa unyenyekevu mkubwa, nitaomba ridhaa ya
kuchaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Natarajia kuendeleza rasmi safari niliyoianza leo kwa kuchukua fomu za maombi
hayo pale Dodoma,Makao Makuu ya CCM, jumatano, tarehe 3 Juni,2015, saa 4
kamili,barabara.
Kipindi cha mpito kutoka awamu moja ya
uongozi kwenda awamu nyingine kingekuwa kigumu sana kwa nchi nyingi hasa nchi
zetu za kiafrika. Mifano iko wazi.Majirani zetu wamepata shida.Lakini waasisi
wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume wametujengea misingi
imara.
Tuna kila sababu ya kuwashukuru na tuna kila sababu ya kujivunia misingi
hiyo. CCM haijayumba na CCM haitayumba.
Baadhi ya wanachama inawezekana
wameyumba. Hebu tuzirudie Ahadi za mwana CCM: binadamu wote ni ndugu zangu na
AFrika ni moja, nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi
yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma, rushwa ni adui wa haki
sitapokea wala kutoa rushwa, cheo ni dhamana sitatumia cheo changu wala cha mtu
mwingine kwa faida yangu binafsi, nitajielimisha kadri ya uwezo wangu na kuitumia
elimu yangu kwa faida ya wote, nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi
yetu, nitakuwa mwanachama mwaminifu wa ccm na raia mwema wa Tanzania na Afrika
nzima.
Nitasema kweli daima fitna kwangu ni mwiko. Hii ndiyo CCM na atoaye
ahadi mbele za Mwenyezi Mungu ndiye Mwana CCM,na si vinginevyo.
Ahadi ya mwanaCCM ya kuondoa umaskini inanipa nafasi ya
kuelezea na kusisitiza kipaumbele muhimu sana cha serikali iliyodhamiria
kuwaondoa wananchi wake kutoka lindi la umasikini ni kukuza uchumi,uchumi wa
kisasa,uliojikita katika misingi ya sayansi na teknolojia na kutumia teknolojia
ya habari na mawasiliano kama kichocheo cha maendeleo hayo.
Kama sayansi na
teknolojia ndio msingi wa uchumi wa
kisasa basi naweza kusema,tena kwa unyenyekevu mkubwa kwamba aliye mbele yenu
ndiye pekee mwenye ujuzi,uelewa,na uzoefu wa masuala haya. Ninalotaka
kusisitiza hapa ni kwamba kukuza na kusimamia uchumi ndio utakuwa kipaumbele
namba moja.Jenga kwanza uchumi imara na mengine yatafuata.
Uchumi imara unajengwa hasa pale panapokuwa na lengo la
kitaifa.Lengo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Tanzania kufikia nchi yenye
kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Lengo hilo liliwekwa mwaka 2000. Tudhamiria
sasa kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe nchi za juu zenye kipato cha kati(High Middle
Income),na kwamba ifikapo 2050 Tanzania iwe nchi iliyoendelea.
Tunawezaje kuyafikia malengo hayo? Tunawezaje kukuza uchumi na
ukuaji huo uwe endelevu?Hili ndilo swali.
1.Kilimo cha kisasa na cha kisayansi kupitia matumizi zaidi na
bora ya mbolea; kuendeleza utafiti kwa kuboresha miundombinu,vifaa,na
kuendekeza rasilimali watu;kuboresha mifumo na aina ya mikopo kwa wakulima
wadogo;kuboresha barabara za vijijini; kuendeleza ujenzi wa maghala kwa ajili
ya kutunza nafaka;kuwa na migumo ya uhakika ya masoko ya mazao;na kuhakikisha
kiwanda cha kimkakati cha mbolea itokanayo na gesi asilia kinajengwa haraka
iwezekanavyo.
2.Kuanzisha na kuendeleza viwanda,kwa kuanzia viwanda
vinavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali asili
3.Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa
upatikanaji wa chakula.
4.Kuendelea kusimamia kutengemaa kwa uchumi mpana
5.Kuondoa vikwazo vinavyozuia uwekezaji wa ndani na kutoka nje
6.Kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ipasavyo kwa kufungua
fursa nyingi za utalii wa ndani na utalii katika sekta ya kusini.
7.Kuongeza tija katika utendaji wa kazi kwa kuthamini
kazi(kufanya kazi kwa bidii,kwa uadilifu,na kwa kujituma), kusimamia
kanuni,maadili na miiko ya utumishi wa umma na kuufanya utumishi wa umma usiwe
wa mazoea tu bali wa ushindani unaopimika katika kutoa huduma kwa wananchi.Hii
itakwenda sambamba na kulinda haki na kuboresha msilahi ya wafanyakazi.
8.Kuchukia,kuzuia na kupambana na ufisadi na rushwa. Kuondoa
vikwazo vinavyoonekana kuwepo kwa
matabaka mawili ya wananchi; wale wanaoshughulikiwa na takukuru moja kwa
moja,na wale ambao kibali kinahitajika kuwashtaki,kwa kuipa Takukuru uwezo wa
kisheria kufanya kazi bila kuingiliwa na chombo chochote,wakati huohuo
kuhakikisha haki za wananchi wema zinalindwa kupitia chombo cha kusimamia
malalamiko (ombudsman).
9.Kuendeleza na ikibidi kuimarisha uhuru wa Benki Kuu na uhuru wa vyombo vya udhibiti wa huduma za
kiuchumi,mifuko ya jamii,bima.
10.Serikali kuwa injini ya ukuaji wa uchumi lakini kuweka
mazingira mazuri kwa sekta binafsi,mtu mmoja,vikundi vya
wajasiriamali,saccos,na kampuni binafsi kuchochea ukuaji wa uchumi.
Uchumi unapokua,basi
serikali itakuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza vipaumbele katika maendeleo
ya jamii: Elimu,maji safi na salama,afya, na miundombinu.
Kuhusu elimu,lengo
litakuwa ni kuboresha mitaala ili iendane na matumizi ya sayansi na teknolojia
katika ngazi zote;kuhakikisha kila mtanzania ana nafasi sawa ya kujiendeleza
kielimu kuanzia ngazi ya awali mpaka elimu ya juu; kuendeleza elimu ya ufundi
na kilimo; kuandaa na kutekeleza mipango kwa hatua kuifanya elimu ya msingi
ifikie kidato cha pili, cha nne na hatimaye kidato cha sita;kuongeza wingi wa
udahili wa wasichana katika katika ngazi
ya elimu ya juu;kuboresha hali na ari ya utendaji wa kazi kwa walimu,ikiwa ni pamoja na ujenzi
nyumba za kuishi na kuongeza ujira.
Katika maeneo mengine ya huduma za kijamii,lengo la serikali
litakuwa ni kutekeleza sera zilizopo na kuhakikisha malengo yanatekelezwa na
yanapimika.Katika kuleta afya bora kwa wananchi lengo litakuwa ni kuweka
mizania katika kuzuia na kupambana na magonjwa.
Uchumi hauwezi kukua pasipokuwa na amani na utulivu. Amani
usalama na utulivu ni tunu.Waasisi wetu wametujengea msingi wa tunu hii.
Viashiria vya kupotea kwa amani vinaanza kuonekana kutoka ndani na nje.Hali
inahitaji kuimarisha vyombo vyetu vya usalama katika maeneo yote hususan
mafunzo,vitendea kazi,vifaa, miundombinu na silaha za kisasa.Hatimaye ulinzi wa
nchi unaanzia mwananchi mwenyewe.
Nafasi ya Zanzibar katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni
kubwa. Hii inatokana na asili na haiba ya nchi zenye visiwa,Zanzibar ikiwa
mojawapo. Historia ya Zanzibar inatukumbusha hili.Kwani katika karne ya kumi na
tisa Zanzibar iliongoza eneo lote la Afrika ya Mashariki kiuchumi na
maendeleo,ukuondoa biashara ya utumwa.
Ilisemekana Ikipigwa zumari Zanzibar
wanacheza ngoma maziwa makuu. Kila linalowezekana litafanywa kuondoa kabisa
hali inayoweza kuikwaza Zanzibar kufikia uwezo wake mkubwa kiuchumi.Muungano
utaimarika na uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi zaidi.
Nahitimisha na suala muhimu la uzalendo.Kwa tafsiri isiyo
rasmi,Uzalendo ni upendo kwa nchi.
Tumeanza kushuhudia kupungua kwa uzalendo. Upungufu huo unajionesha katika
kuenzi tamaduni za nje,kubeza juhudi za maendeleo yaliyopatikana, viongozi
kutoa matamshi yanayo kebehi nchi wakiwa nje ya nchi,kutojivunia historia yetu
iliyojikita katika michango ya mashujaa wetu.
Hawa ni pamoja na wale waliopambana na wakoloni,akina
Kinjeketile, Mkwawa ,Mirambo,Chaburuma
na wengineo ambao walitoa uhai wao kulinda na kutetea heshima ya mwafrika dhidi
ya ukoloni.Aidha waasisi wa TANU,Hayati Mwalimu Nyerere,Sykes,Mzee Kawawa, na
wenzao;Waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar,Hayati Abeid Amani Karume na
wenzake akina Mzee Thabit Kombo,Kanali Seif Bakari,Hais Darwesh,Edington
Kisasi,Yusuf Himid,Said Washoto na wengineo;ambao walionesha upendo na uzalendo
wa hali ya juu.Vilevile tuna mashujaa wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika akina
George Magombe na Hashim Mbita.Tutaendelea kuenzi, kuthamini,na kuiendeleza michango mikubwa ya Marais wetu wastaafu,Mzee
Aboud Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Idris Abdukwakil,Dr Salmin Amour,Dr
Amani Abeid Karume,na Mzee Benjamin William Mkapa. Kipekee napenda kuwashukuru
Marais wetu wa sasa; Mheshimiwa Dr Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,na Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein.ambao wamefanya kazi
kubwa ya kuimarisha uchumi na umoja wa nchi yetu. Daima nitaenzi mchango wao.
Tujivunie nvhi yetu na Kwa pamoja
tutaenga nchi tunayoitaka.
Picha na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment