Mkuu wa Wilaya akipewa zawadi
MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Munasa
ametoa wito kwa wanafunzi nchini kupendelea masomo ya Sayansi kutokana na taifa
kwenda kwenye mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Munasa alitoa wito huo katika sherehe za
maadhimisho ya kutimiza miaka kumi kwa Shule ya St. Marys International tangu
kuanzishwa kwake Mkoani Mbeya ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Alisema Taifa linakoelekea ni kwenye matumizi ya
teknolojia mbali mbali hivyo linahitaji wasomi ili waweze kuendana na kasi hiyo
hivyo jambo la msingi ni kwa wanafunzi kukazania masomo ya sayansi ili yaweze
kuwasaidia baadaye katika kukabiliana na tatizo la ajira.
“Tunataka taifa la wanaosoma sayansi, na karne
hii ni sayansi hivyo pendeni masomo ya sayansi, hivi sasa kunamatumizi makubwa
ya mitandao ya kijamii pia tumieni hiyo kupata vitu vitakavyowasaidia kimasomo”
alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake Afisa Tawala wa Shule hiyo,
Anuciatha Ngonyani, alisema shule hiyo licha ya kupata mafanikio makubwa katika
kipindi cha miaka kumi tangu ianzishwe tawi mkoani Mbeya bado inakabiliwa na
changamoto nyingi.
Ngonyani alisema shule hiyo iliyofunguliwa
Januari 20, 2005, inakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu, upungufu wa usafiri
kwa wanafunzi wa kutwa na kusababisha kukodi magari kwa gharama kubwa, upungufu
wa viwanja bya michezo kama mpira wa kikapu na mpira wa mikono.
Aliongeza kuwa bado changamoto kwa Serikali
kuzirundikia kodi nyingi shule binafsi pia inapelekea kushindwa kuwalipa Walimu
na watumishi wengine mishahara mizuri licha ya kupunguza tatizo la ajira kwa
kuwa na watumishi ambao ni walimu na wasio walimu zaidi ya 120.
Alisema Kodi ambazo Serikali inapaswa
kuzipunguza katika shule binafsi ni pamoja na Kodi ya ardhi, kodi ya majengo,
kodi ya zimamoto na uokoaji, kodi ya Afya za wafanyakazi(OSHA), kodi ya leseni
ya biashara, kodi ya uzoaji taka na kodi ya mapato.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment