CHAMA cha Walemavu(CHAWATA) Jiji la Mbeya kimesema kipo tayari kukiunga mkono Chama kipya cha ACT Wazalendo kutokana na kiongozi wake mkuu, Zitto Kabwe kutoka katika familia ya walemavu.
Hayo yalibainishwana Chama cha Walemavu Jiji la Mbeya katika mkutano wao uliofanyika katika ukumbi wa Coffee garden ambapo walisema wameona matumaini yao kama walemavu yanaweza kutetewa kupitia chama cha ACT Wazalendo.
Mwenyekiti wa CHAWATA Jiji la Mbeya, Damas Mwambeje alisema jamii ya walemavu imesahaulika kwa kiwango kikubwa licha ya viongozi mbali mbali kuwepo kwani hakuna kiongozi ambaye amewahi kuwatembelea ili kujua changamoto zinazowakabili.
Alisema kutokana na kutojaliwa na viongozi waliopita na waliopo wameona kwa sababu Zito Kabwe kiongozi wa Chama cha ACT ametokea katika familia ya walemavu wamuunge mkono katika jitihada zake za kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao ili aweze kuwatetea.
“Mheshimiwa Zitto Kabwe amezaliwa na kulelewa katika familia yenye ulemavu, kwani mama yake alikuwa ni mlemavu hivyo anaujua uchungu wa watu wenye ulemavu kwa sababu anajua alivyosoma hadi anafanikiwa huyu mtu tukimpa nguvu hatoweza kutusahau” alisema mwenyekiti huyo.
Naye Makamu Katibu wa Chawata, Mawazo Lupenza, alisema Walemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi vikiwemo vifaa kuuzwa bei kubwa bila kujali mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Alisema Serikali imeisahau jamii ya Walemavu kwa kuwapatia misaada licha ya kuandika maombi mbali mbali ya kutaka kutatuliwa shida zao lakini majibu yanakuwa hayafiki kwa wakati.
Wakati huo huo, Mchungaji wa makanisa ya WAM Jiji la Mbeya,Joshua Msigwa, ametangaza nia ya kugombea ubunge kupitia Chama cha ACT Wazalendo katika Jimbo la Mbeya mjini ambapo pia Chama cha Walemavu kimesema kitamuunga mkono.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mchungaji Msigwa alisema baada ya kuisoma Katiba ya ACT ameilewa Sera yake amegundua anaweza kutetea maslahi ya wakazi wa Jiji la Mbeya kupitia Chama hicho.
Alisema yuko tayari kusimamia shughuli za kiuchumi za Jiji la Mbeya ikiwa ni pamoja na kuhamasisha maendeleo akiwa jimboni hadi Bungeni pindi atakapokuwa amechaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Mbeya, Bahati Rongopa, alisema kujitokeza kwa Mchungaji kuonesha nia ya kugombea ubuge kunatia matumaini ya kukubalika kwa Chama mapema zaidi.
Alisema Jimbo la Mbeya mjini limekuwa na mkosi wa kupata kiongozi wa kuliwakilisha vizuri katika chaguzi zote zilizopita kwa wananchi wamekuwa wakichagua mtu kwa ushabiki bila kumpima na kumuona kama anaweza kuwawakilisha vizuri.
Aliongeza kwa kutoa wito kwa vyama vingine vya upinzani kukiunga Mkono chama cha ACT ili kukiondoa madarakani Chama tawala kwani hali ilivyo sasa Vyama vinavyounda Ukawa wamekuwa wakikituhumu Chama hicho kuwa pia kinawapinga wao.
Na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment