CHAMA cha Msalaba mwekundu nchini kimetakiwa kuelekeza nguvu zao zaidi katika kuwahamasisha Vijana kujiunga na Chama hicho ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini.
Wito huo ulitolewa na Kaimu Afisa Tarafa ya Sisimba, Fidel Mwaselela alipokuwa akifunga maadhimisho ya Siku ya Msalaba mwekundu duniani katika Sherehe zilizofanyika Kimkoa katika viwanja vya shule ya msingi RuandaNzovwe jijini Mbeya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyerembe Munasa.
Mwaselela alisema kwa mujibu wa kanuni za Chama cha Msalaba mwekundu shughuli zake nyingi ni kujitolea hivyo vijana wakihamasishwa kujiunga na Chama hicho tatizo la ajira litapungua sambamba na umaskini kwa sababu wengi watakuwa wanaelewa maana ya kujitolea.
Alisema vijana wakihamasishwa kujitolea na kujitoa kuweza kuwa wamoja katika mapambano dhidi ya ajira na umaskini unaoweza kuwanyemelea vijana katika maisha yao ya baadaye kunaweza kusaidia kupunguza wimbi la vijana kuandamana na kufanya fujo zisizokuwa za msingi.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi kufunga maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Mbeya, Ulimboka Mwakilili, alisema wananchi wengi wamezoea kufanya kazi kwa kulipwa jambo linalochangia kurudisha maendeleo nyuma.
Alisema wengi wao wanamtazamo hasi kuhusiana na Chama cha Msalaba mwekundu ambapo wakihamasisha wananchi kujiunga nacho hupeleka maslahi mbele kwanza kuliko jambo lingine na kusahau kama Chama hicho kinafanya kazi ya kupambana na majanga yanayomkumba binadamu wakati wowote.
Aliongeza kuwa hadi sasa Chama hicho Mkoa wa Mbeya kinawanachama 4000, idadi ambayo ni ndogo kulingana na matukio yanayotokea hivyo kuendelea kuhamasisha vijana kujiunga kwa gharama ya shilingi 1000, 3500 na Shilingi laki moja kwa taasisi au Kampuni.
Mwakilili aliongkuwa Chama cha Msalaba Mwekundu Duniani kinaendelea na Kampeni ya kuwaelimisha wanaotumia vibaya nembo ya Chama hicho tofauti na inavyotakiwa ambapo asilimia kubwa nembo hiyo inatumika kinyume katika Hospitali, Zahanati na vituo vya Afya pamoja na Maduka ya madawa.
Alisema pia wapo wengine wamekuwa wakizihusisha nembo za Chama na Imani za dini ili hali nembo hizo hazifanani na dini yoyote ambapo baadhi yao hudhani Msalaba huo upo kwa ajili ya wakristo na nembo ya mwezi Mchanga hufananishwa na dini ya kiislamu.
“Niwaambie ukweli Msalaba wetu uko sawa pande zote lakini ule wa dini ni mrefu kwa chini pia una rangi tofauti tofauti, na kuhusu nembo ya mwezi mchanga inayofananishwa na uislamu pia ni tofauti kwa maana Waislamu wanaweka na nyota sisi hatuna” Alisema Mwakilili.
Na Mbeya yetu
TANGAZO
TANGAZO MPYA KABISA: CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA (CBE) KAMPASI YA MBEYA. , NAFASI ZA MASOMO – SEPTEMBA 2015/2016 WAHI SASA
No comments:
Post a Comment