WAKAZI wa Jiji la Mbeya
wametakiwa kuacha kutupa taka katika mifereji ya maji na kwenye mito jambo
linaloweza kusababisha uharibifu wa miundombinu na na magonjwa ya miripuko.
Wito huo ulitolewa jana
na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Samwel Lazaro,
alipokuwa akizungumza na Mtandao huu kuhusiana na kukithiri kwa taka katika
mitaa ya Halmashauri hiyo iliyosababishwa na utaratibu mpya wa uzoaji wa taka
ulioanzishwa.
Dk. Lazaro alilazimika
kutoa kauli hiyo kufuatia kuharibika kwa magari ya kuzoa taka ya Halmashauri ya
Jiji na kusababisha takataka kukaa muda mrefu mitaani bila kuzolewa ambapo
wananchi hulazimika kuvizia mvua zinaponyesha na kasha kutupa taka katika
mitaro ya maji na mifereji.
Katika utaratibu mpya
ulioanzishwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk. Lazaro alisema udhibiti wa
taka umerudishwa mikononi mwa jamii husika ambapo sheria inamtaka kila
anayezalisha takataka inakuwa ni mali yake mwenyewe.
Hivi sasa Halmashauri ya
Jiji la Mbeya limeondoa utaratibu wa wananchi kukusanya takataka na kulunduka
katika maghuba na badala yake wanatakiwa kukusanyia majumbani mwao na kasha kusubiri
usafiri wa kuzipeleka kwenye dampo.
Aidha tangu utaratibu
huo uanze wananchi wamekuwa na malalamiko mengi kutokana na magari hayo
kushindwa kupita kwa wakati licha ya kulundika taka kwa muda mrefu jambo
linaloleta usumbufu kwa watumiaji wa maeneo yanayotumika kukusanyia taka hizo.
Akizungumzia malalamiko
hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk. Lazaro alisema changamoto kubwa imetokana
na kuharibika kwa magari pindi yanapokuwa yanatakiwa kwenda kusomba taka
majumbani lakini hivi sasa Jiji liko kwenye mpango wa kuondokana na adha hiyo
baada ya TAMISEMI kuridhia Jiji kununua magari mapya ya taka.
Alisema hivi sasa
Halmashauri ina magari 7 ambayo kati yake magari manne ni ya kupakia kwa mkono
na magari mawili yanabeba makontena lakini matarajio ni kuongeza magari mengine
7 ifikapo Mwezi Julai mwaka huu.
Aliyataja aina ya magari
mapya yanayotarajiwa kuja kupunguza adha ya takataka katika jiji la Mbeya kuwa
ni magari matatu ya kupakiwa kwa mkono na magari manne yatakayokuwa yanabeba
makontena.
Aliongeza kuwa
Halmashauri iko kwenye utaratibu wa kuziachia Kata kuunda vikundi kwa ajili ya
kukusanya taka katika maeneo yao ambavyo vitajiendesha kupitia ushuru wa taka
utakaochangiwa na wananchi wenyewe.
Alisema kwa mujibu wa
sheria kila Kaya inapaswa kuchangia shilingi 1000 kwa mwezi kwa ajili ya taka
lakini Halmashauri imepunguza na kufanya kila nyumba kuchangia shilingi 500 kwa
mwezi.
Dk. Lazaro aliongeza
kuwa Halmashauri haizuu baadhi ya kata kama wanakubaliana kuongeza kiwango cha
kuchangia kama wameona shilingi 1000 au 500 haiwatoshi kwa ajili ya kuondoa
taka katika maeneo yao.
Alizitaja baadhi ya Kata
ambazo tayari zimeanza kutekeleza mpango huo kwa kuunda vikundi vya kukusanya
taka ambazo ni Kata ya Forest na Kata ya Mwakibete huku utaratibu ni kuendelea
kuzihamasisha kata zingine.
No comments:
Post a Comment