Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, March 17, 2015

MAHAKIMU NA MAAFISA PROBESHENI WA MKOA WA MBEYA WAPEWA MAFUNZO KUHUSU UTEKELEZAJI WA SHERIA ZA ADHABU MBADALA.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa mbeya, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, alipokuwa akifungua  mafunzo ya Mahakimu na Maafisa Probesheni wa Mkoa wa Mbeya kuhusu utekelezaji wa sheria za adhabu mbadala,yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa, jijini Mbeya.

Mkurugenzi Idara ya Probesheni na huduma kwa jamii Wizara ya mambo ya ndani ya Nchi, Fidelis Mboya akimkaribisha mgeni rasmi

Mratibu, Mradi wa Kuboresha Mafunzo ya Urekebishaji wa Wahalifu,  Bw. Charles Nsanze


Mahakimu na Maafisa Probesheni wa Mkoa wa Mbeya wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mkoa wa Mbeya Mhe. Michael Mteite akimshukuru mgeni rasmi mara baada ya kufungua mafunzo kuhusu utekelezaji wa sheria za adhabu mbadala


Picha ya pamoja

WATEKELEZAJI wa Sheria nchini wametakiwa  kupatiwa orodha ya aina mbalimbali za adhabu ili wazitumie katika kuhukumu kulingana na mahitaji ya kila mkosaji ili hatimaye malengo ya adhabu hiyo yatimie.
                                          


Maagizo hayo yalitolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa mbeya, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, alipokuwa akifungua  mafunzo ya Mahakimu na Maafisa Probesheni wa Mkoa wa Mbeya kuhusu utekelezaji wa sheria za adhabu mbadala,yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa, jijini Mbeya.


Dk. Nchimbi alisema Msongamano wa wafungwa magerezani ulisababisha mambo matatu makuu,  ambayo  ni Gharama kubwa za uendeshaji wa magereza kuwa mzigo mkubwa kwa serikali na hivyo kusababisha hali duni ya maisha ya wafungwa kwa  huduma za chakula na afya jambo ambalo ni uvunjifu wa Haki za Binadamu kwa wafungwa.


Alisema jambo la pili ni  Kuzorota kwa utekelezaji wa jukumu la msingi la magereza la kuwarekebisha wakosaji na hivyo kupelekea kuongezeka kwa viwango vya urudiaji wa uhalifu miongoni mwa wale wanaomaliza kutumikia adhabu zao za jinai.


Aliongeza kuwa jambo la tatu Wahalifu wa makosa madogo madogo kupelekwa magerezani kuchanganyika na wahalifu sugu na hivyo kujifunza uhalifu mkubwa zaidi.

Alisema kutokana na hali hiyo kujitokeza, dunia katika ngazi ya Umoja wa Mataifa iliandaa Sheria na Miongozo mbalimbali ambavyo kwa ujumla wake vinasisitiza Adhabu Mbadala wa Kifungo Gerezani zitumike pale inapostahili ili kuepukana na utegemezi uliokithiri wa Adhabu ya Kifungo Gerezani.


Alizitaja adhabu hizo mbadala ni pamoja na Faini, Onyo, Probesheni, Parole, Kifungo cha Nje, Huduma kwa Jamii, Kuachiliwa kwa Masharti, Kuchapwa Viboko na nyinginezo nyingi tu ambazo zinatumika katika nchi mbalimbali duniani.Aliongeza kuwa  malengo makuu ya kuwapa adhabu wakosaji ni kuonya, kurekebisha, kutoa haki na kukinga au kulinda jamii dhidi ya kosa au makosa yaliyotendwa. 


Alisema  ni jambo la muhimu  kwa watekelezaji wa Sheria kupatiwa orodha ya aina mbalimbali za adhabu ili wazitumie katika kuhukumu kulingana na mahitaji ya kila mkosaji ili hatimaye malengo ya adhabu hiyo yatimie.


“ Ni dhahiri kwamba kila mkosaji anapaswa kuadhibiwa kulingana na tabia na mwenendo wake katika jamiii, mazingira ya kosa lake, uzoefu wake wa makosa na hata umri na sababu za utendaji wake wa kosa” alisema Dk Nchimbi.


Awali akimkaribisha Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Idara ya Probesheni na huduma kwa jamii Wizara ya mambo ya ndani ya Nchi, Fidelis Mboya, alisema mafunzo hayo yamelenga kwa Mahakimu wote wa Mkoa wa Mbeya, Njombe na Iringa, ambao wako katika ngazi za Hakimu Mkazi Mfawidhi, Hakimu Mkazi, Hakimu wa mahakama ya Wilaya,Hakimu wa Mahakama za Mwanzo pamoja na Maprobesheni.

Alisema Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi mkubwa unaoendeshwa katika nchi tatu za Afrika mashariki zikiwemo Tanzania, Uganda na Kenya ili kuboresha adhabu mbadala kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza.

Alisema kutokana na ufinyu wa fedha kila nchi ilitakiwa kuchagua Mkoa mmoja ambao mradi huo utatekelezwa ambapo kwa Tanzania Mkoa wa Mbeya ndiyo ulipendekezwa na kuanza kutekelezwa kwa kutoa mafunzo mbali mbali kwa wadau.

Aliongeza kuwa mradi huo ni wa miaka miwili 2015 na 2016 ambapo tayari mafunzo yalishafanyika kwa waandishi wa habari na kufuatiwa na Mahakimu kisha kumalizia na wasimamizi wa vyombo vinavyosimamia wahalifu wanaotumikia adhabu mbadala.

Mwisho.

Na Mbeya yetu

No comments: