Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, February 20, 2015

Nini Wanafunzi wafanye Baada ya Matokeo Ya Kidato cha Nne


Huzuni ikipitiliza humpelekea mtu kukata tamaa na kutoona thamani ya maisha na hata kufikia hatua ya kunywa sumu au kujiua wakati furaha ikizidi humfanya mtu akasahau majukumu mengine mazito yaliyo mbele yake.

Matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni yamewaacha wanafunzi na wazazi wengi kwenye majonzi huku wengine wakiwa na furaha. Hii ni kutokana na idadi ya wanafunzi waliomaliza kuwa na matokeo ya wastani katika mitihani yao.

Pamoja na hilo, kubwa ni kuangalia namna bora ya kusonga mbele kwa wale ambao hawakufanya vema wakijipanga upya kuangalia ni yepi ya kufanya ili kuweza kusonga mbele baada ya jitihada zao zilizotangulia kutofanikiwa wakati wale waliofaulu vizuri wakiweka mipango na mikakati madhubuti itakayowawezesha kuendelea zaidi.  

Jambo la kwanza analopaswa kulitambua mwanafunzi ni kukubali matokeo aliyoyapata. Kuukana ukweli huu hakutakuwa na msaada kwake. Ni wazi zinaweza kuwapo kasoro za hapa na pale katika masuala ya usahihishaji lakini mchango wake katika matokeo ya jumla unaweza usiwe mkubwa sana.

Kwa muhtasari, matokeo ya kidato cha nne unaweza kuyagawa katika makundi yaliyopangwa katika Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) ambayo ni daraja la ‘A’ kundi la fauli Uliojipambanua (Distinction) litakuwa na alama kati ya 3.6-5.0, ‘B’ Kundi la Kundi la ufaulu mzuri (Merit) litakuwa na alama kati ya 2.6.3.5, ‘C’ kundi la ufaulu wa wastani (Credit) litakuwa na alama kati ya 1.6-2.5, ‘D’ Kundi ufaulu hafifu (Pass) 0.3-1.5 na ‘F’ Kundi la ufaulu usioridhisha (Fail) 0.0-0.2.

Aidha unaweza kuyagawa katika makundi manne ya walio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi; wasio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi lakini wana fursa za kuendelea na vyuo vingine; na waliofeli kabisa amabo wanakosa sifa za kuendelea na masomo kwa vigezo vya ufaulu wa kidato cha nne.

Kujiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi
Awali ya yote ifahamike kuwa wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya serikali ni wale wanaotoka shuleni (school candidates) na si watahiniwa wa kujitegemea (private candidates).

Kadhalika wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja katika vyuo vya ufundi mfano Dar es Salaam Institute of Technology (DIT), Arusha Institute of Technology (AIT) na kama hivyo, huwa na sifa sawa na wale wanaochaguliwa kuijunga na kidato cha tano katika michepuo ya sayansi. Idadi ya wanafunzi hawa huwa si kubwa sana.

Mwanafunzi aliyefaulu kwa Distiction na Merits ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano au chuo cha ufundi katika shule na vyuo vya serikali. Aidha hata waliopata Credit na Pass wana nafasi ya kuchaguliwa. Si tukio la kawaida mwanafunzi aliyepata divisheni F kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano au chuo cha ufundi.

Mara nyingi changamoto wanayokuwa nayo wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu ni aina ya michepuo na shule za kuendelea nazo. Ni jambo la kawaida kukuta kijana akifaulu masomo mengi na kisha kusoma mchepuo ambao hana mapenzi nao sana. Hili husababishwa na mazingira ya ujazaji fomu za michepuo ya kuendelea nayo baada ya kuhitimu masomo. Hutokea kuwa mchepuo anaoupenda sana ana shaka ya kufanya vizuri na hivyo kuchaguwa michepuo mingine. Ama kwa upande wa shule, hutegemeana na nafasi, ufaulu wa wanafunzi na idadi ya wanafunzi walioomba katika Shule husika. 

Baadhi ya wanafunzi wanapokosa michepuo au shule walizoomba huhangaika na kutumia muda mwingi wakitaka kubadilisha. Uzoefu unaonyesha kwamba ni sehemu ndogo za sana ya wanafunzi hao ambao hufanikiwa. Ushauri wetu ni kwamba endapo kijana atachaguliwa katika shule asiyoipenda na hakuna sababu za kiafya za kumfanya asiende katika shule hiyo pengine kutokana na hali ya hewa, au kachaguliwa mchepuo asioupenda na familiya yake haina uwezo wa kumsomesha shule binafsi, basi atulizane katika hicho alichopata na ajikite zaidi katika masomo kwani anaweza pia kufanikiwa katika fursa hiyo aliyoipata.

Changamoto nyingine ambayo huwakuta vijana wa kundi hili ni kuanza kusoma tuisheni za masomo ya kidato cha tano kabla ya uchaguzi kufanyika. Utata wa jambo hili ni kama tulioueleza hapo juu wa mwanafunzi kuchaguliwa mchepuo tofauti kabisa na masomo anayosoma. Kwa mfano kuna kijana tunayemfahamu akisoma masomo ya mchepuo wa Economic, Geography na Mathematics (EGM) lakini akachaguliwa mchepuo wa History, Kiswahili na Language (HKL). Tofauti iliyoje! Katika hilo inashauriwa kuwa kama mwanafunzi hana hakika ya kusoma katika shule binafsi, asianze masomo hayo mpaka baada ya uchaguzi wa kidato cha tano kufanyika. Na ikibidi kujisomea asome vitu vya jumla kama masomo ya lugha, kompyuta nk. 

Kwa wale waliokwisha amua au lazima wasome katika shule binafsi, ni muhimu kufanya utafiti juu ya ubora wa shule hizo kitaaluma, maadili na stadi nyingine za maisha. Aidha ni muhimu kufuatilia juu ya kiwango cha ada, muda wa kuchukuwa na kurejesha fomu za maombi, tarehe ya usaili na ya kufungua shule. Hutokea mwanafunzi akapoteza muda na hatimaye kuhangaika kutafuta shule wakati shule nyingi zimeshasimamisha kupokea wanafunzi. 

Kuna wanafunzi waliopata Pass na Credit ambao hawatapata nafasi ya kujiunga na kidato cha tano. Hata hivyo vijana waliopata Pass na sehemu ndogo ya waliopata Credit huwa wanapata sifa na wanaweza kujiunga na kidato cha tano katika shule binafsi endapo uwezo wa familiya unaruhusu. Hii ni kutokana na kanuni za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zinamruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo ya kidato cha tano endapo amefaulu katika kiwango cha angalau alama C kwa masomo matatu au zaidi hata kama masomo aliyofaulu hayatengenezi mchepuo wowote mfano Civics, Biology na English huku akiwa amepata alama D au chini yake katika masomo mengine. Endapo familiya itamudu kumsomesha kidato cha tano kati shule binfasi, ni vema kijana akapata ushauri wa wazazi, walimu na wazoefu wengine juu ya mchepuo stahiki inayomfaa. Mara nyingi wanafunzi wa aina hii huwa wanashindwa kutofautisha baina matashi ya nafsi na uwezo binafsi wa kimasomo. Kwamba kijana tuliyemtaja hapo juu asome CBG au HGL ni suala linalohitaji tafakuri pamoja na mhusika.

Kujiunga na vyuo vya Ualimu
Kuna wanafunzi waliopata Pass na hata Credit ambao hawatachaguliwa kujiunga na kidato cha tano lakini watachaguliwa kujiunga na vyuo vya ngazi ya Diploma mfano vyuo vya Ualimu. Kwa mujibu wa kanuni zilizopo sasa, kiwango cha ufaulu cha mwisho kuchukuliwa ni Credit. Pamoja na kujaza nafasi za masomo ya Ualimu, mwanafunzi atapaswa kuomba rasmi nafasi hizo kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi au katika vyuo binafsi baada ya matokeo kutoka na nafasi kutangazwa rasmi. Aidha kutokana na uchache wa nafasi katika vyuo huwa si wote walio na sifa wanaoweza kuchaguliwa serikalini lakini nafasi ni nyingi sana katika vyuo binafsi.
Kujiunga na Vyuo Vingine

Wapo vijana ambao licha ya kuwa na sifa za kuchaguliwa katika vyuo vya ualimu, huwa hawachagui au hawaendi hata baada ya kuchaguliwa kwasababu zao binfasi. Kama uwezo wa familia unaruhusu na mnaona kusoma ualimu si kipaumbele chenu haina tatizo. Hata hivyo, ni vema kuangalia fursa zilizopo na uwezo wa familia kiuchumi. kijana anapaswa kufahamu kufahamishwa kuwa si busara kwa familia yenye uwezo duni wa kiuchumi, kama zilivyo familia nyingi za kitanzania, kumsomesha kijana katika ngazi hii kwa gharama kubwa wakati kuna wengi wanahitaji kuendelezwa kitaaluma katika familia.

Wale wote waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi, vyuo vya kawaida au vyuo ualimu, fursa pekee waliyonayo ni kujiunga na vyuo vingine vinavyotoa kozi mbalimbali kama, biashara, utawala, ufundi, nk. Vyuo kama College of Business Education (CBE), Tanzania Institute of Accountancy (TIA), Institute of Social Work (ISW), Institute of Information Technology (IIT) ni mifano michache katika ya vyuo vingi vilivyopo. Changamoto kubwa katika vyuo hivi ni uwezo wa kuzimudu gharama zake za mafunzo hayo. 

Mwanafunzi aliyefeli kabisa na kupata Sifuri (0), hana fursa yoyote katika zote zilizotajwa hapo juu. Hata hivyo anakuwa amepata cheti cha kuhudhuria masomo (leaving certificate) ambacho huwa na msaada fulani katika maisha kwa kuna wakati huhitajika vijana waliomaliza kidato cha nne bila kujali ufaulu wake. 

Pia kuna fursa zinazohitaji vijana waliomaliza shule ya msingi ambazo bado zinaweza kutumiwa na vijana hawa. Kwa mfano kuna fani mbalimbali zinazotolewa na vyuo vya VETA kama ufundi, udereva, usafi,utunzaji bustani, upishi nk ambazo zinaweza kutumiwa vema na vijana ambao hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne.
Ni muhimu kutaja hapa kwamba si waliofeli tuwanaoweza kuzitumia fursa za mafunzo ya VETA bali hata wale waliopata divisheni Pass na hata Credit ambao ama hawakupata fursa za kuchaguliwa kidato cha tano au familiya zao hazimudu kuwasomesha katika shule au vyuo vya kujilipia.

Kurudia Mitihani
Wanafunzi wengi wanaofanya vibaya katika mitihani yao, jambo la haraka linalowajia vichwani ni kurudia mitihani. Ndio maana siku hizi vituo vinavyotoa mafunzo kwa wanaorudia mitihani vimekuwa vikiongezeka kila kukicha. Ni kwakuwa soko linakuwa na wateja wameongezeka.
Pamoja na kuunga mkono na kuheshimu juhudi za wanaotoa mafunzo hayo, tungependa tutanabahishe kwamba ni ili kuepusha upotevu mwingi wa muda na pesa, ni vema mwanafunzi akawa akijiandaa kurudia mitihani huku akijufunza ujuzi mwingine. Uzoefu unaonyesha kuna wanafunzi wanaorudia mitihani na matokeo yao kuwa mabaya kuliko ya mwaka uliotangulia. Aidha kuna wanafunzi waliorudia mitihani zaidi ya mara moja na bado hawakufanikiwa kupata alama C au zaidi (credits) tatu walizohitaji ili wajiunge na kidato cha tano.
Endapo mwanafunzi atajiandaa kurudia mitihani huku anapata ujuzi mwingine mfano udereva, ufundi,nk anakuwa katika nafasi nzuri ya ajira hata asipofaulu mitihani yake anayorudia. Ni uzuri ulioje endapo atapata vyote - credits na huku ana cheti cha ujuzi wake. 

Jambo hili linawezekana endapo kijana ataugawa vizuri muda wake chini ya muongozo wa familia kwa mfano asubuhi akienda chuoni kupata ujuzi na jioni akienda tuisheni kwa ajili ya kurudia mitihani. Aidha endapo mwanafunzi hatofanikiwa kupata credits, anaweza kuanza kazi huku ajiandaa taratibu kurudia mitihani yake. Wengi wamefanikiwa kwa utaratibu huu.
Kukata rufaa juu ya matokeo
Wapo wanafunzi ambao wanakuwa hawakuwa hawakuridhika na matokeo waliyopata wakiamini hawakutendewa haki katika usahihishaji pengine kwa kuzingatia rekodi za matokeo yao katika mitihani ya shuleni au kwa jinsi walivyofanya mitihani.
Kwamba hatupingi jambo hili ndivyo pia tungependa kusisitiza kuwa wakati ukikusudia hilo ni vema ukaendelea na mipango mingine ya kujiendeleza kama tulivyoitaja hapo juu. Hii ni kwasababu ni wanafunzi wachache sana ambao matokeo yao hubadilika baada ya mitihani yao kusahihishwa upya. Aidha unaweza kupoteza muda mwingi ukisubiri hatma ya rufaa yako na kisha majibu kuja usivyotarajia. 

Ufadhili wa Masomo
Hutokea wanafunzi waliopata nafasi za masomo katika shule binafsi au vyuo vinavyohitaji kujilipia wakawa hawana uwezo wa kujisomesha na hivyo kuhangaika huku na kule kutafuta ufadhili. Ukweli ni kuwa ni wachache sana ambao hufanikiwa. Hii ni kutokana na kutokuwa na taasisi rasmi zinazotoa ufadhili katika viwango hivi ya elimu nchini.
Pamoja na kutokatishana na tamaa,  ni vema mtu unapokuwa katika hali hiyo kutafuta shughuli itakayokuwezesha kujenga nguvu za kiuchumi na kisha kuweka akiba kwa ajili ya kujisomesha. Unaweza kuweka malengo ya kusoma huku ukifanya kazi. Endapo shughuli zako hazikupi fursa ya kusoma huku ukifanya kazi, unaweza kuahirisha kusoma hadi kipindi fulani baada ya kujiimarisha kiuchumi. Endapo hilo litakuwa gumu kulitekeleza, familia iangalie uwezekano wa kuuza sehemu ya rasilimali endapo inazo na ambazo hazitaithiri familia nzima endapo zitauzwa.

Tuhitimishe kwa kusema, matokeo vyovyote yawavyo hayawezi kuwa ndio mwisho wa maisha. Siku zote wanaofanikiwa ni wale wanaotazama mbele huku wakijifunza kwa yaliyowatokea. Walofaulu washukuru huku wakijipanga; waliofanya vibaya wasubiri huku wakijifuza. Tumia vizuri kila fursa unayoipata bila kujali udogo wake. Jifunze kwa wengine, uliza, pata miongozo kwa waliokutangulia, na amini kuwa ipo siku ufanikiwa. Washindi hawaachi, na wenye kuacha hawashindi.
KUVUNJIKA KWA KOLEO SI MWISHO WA UHUNZI

Kwa Msaada zaidi wa ushauri na namna bora ya kusoma tafadhali wasiliana nasi kwa namba 255 767 488856
au barua pepe marshk86@hotmail.com


1 comment:

Anonymous said...

naitwa miraji nimepata credit 1.6 je kuna uwezekano wa mm kupangiwa shule na combi haijabalance?