Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, February 5, 2015

KAMPUNI YA SIMU YA TTCL YAZINDUA MNARA WA MAWASILIANO, WAISHIO VIJIJINI KUNUFAIKA ZAIDI

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Chunya, Sosthenes Mayoka akikata utepe kuashiria ufunguzi wa sherehe za kuzindua mnara wa simu ya kampauni ya TTCL katika kijiji cha Shoga wilayani Chunya.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Chunya(DAS), Sosthenes Mayoka akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mnara wa mawasiliano ya simu ya kampuni ya TTCL.

Mwenyekiti wa kijiji cha Sangambi, Lusekelo Lwesha, akifungua sherehe za uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa kampuni ya TTCL.

 Mkurugenzi wa Kanda wa kampuni ya simu ya TTCL, Juvenal Utafu akitoa taarifa za mradi wa ujenzi wa mnara wa mawasiliano uliojengwa katika kijiji cha Shoga wilayani Chunya.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Chunya ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Chunya, Sosthenes Mayoka akitoa hotuba yake kwa wakazi wa vijiji vya Shoga na Sangambi.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, Lames Mlaguzi akimkabidhi simu ya mezani Katibu tawala Wilaya ya Chunya.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, Lames Mlaguzi akimkabidhi simu ya mezani Afisa mtendaji wa kijiji cha Shoga, Simon Mwabubite kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya Kijiji.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, Lames Mlaguzi akimkabidhi simu ya mezani Afisa mtendaji wa kijiji cha Sangambi, Emanuel Evance kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya Kijiji.

Mwakilishi wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC) Hoseah Cheyo akichukua maoni kwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha Sangambi kuhusu kupokea mnara wa simu wa kampuni ya TTCL.

Mkurugenzi wa Kanda ya TTCL      akiungana na kikundi cha sanaa kucheza ngoma ya asili ya wakazi wa kijiji cha Shoga katika sherehe za uzinduzi wa mnara wa mawasiliano.


Baadhi ya watumishi wa kampuni ya simu ya TTCL na Walinzi wa mnara wa mawasiliano uliopo kijiji cha Shoga wakiwa katika picha ya pamoja.


Watumishi wa Kampuni ya TTCL wakikagua mnara wa mawasiliano kabla ya kuzindua rasmi.

Wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa kampuni ya simu ya TTCL katika kijiji cha Sangambi wakifuatilia kwa makini matukio yanayoendelea.

WAKAZI zaidi ya 7000 wa Kijiji cha Shoga kata ya Chalangwa Wilaya ya Chunya mkoani hapa wanatarajia kunufaika na huduma za simu kutoka kampuni ya TTCL baada ya kuzindua mnara wa mawasiliano.

Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa mnara huo, Mkurugenzi wa Kanda ya Mbeya wa TTCL, Juvenal Utafu, alisema mradi huo umejengwa kupitia mfuko wa huduma ya mawasiliano kwa wote(UCSAF) uliotolewa na Serikali.

Utafu alisema Serikali kupitia mfuko huo umelenga kuleta ushiriki kwa watoa huduma za mawasiliano katika kukuza na kusukuma maendeleo ya kijamii kwa kutumia TEHAMA hususani katika maeneo ya vijijini.

Alisema Serikali ilitoa tenda kwa kampuni ya simu ta TTCL katika awamu ya kwanza iliyoanza kutekelezwa mwaka 2014 kwenye mikoa 10 ikilenga Kata 20 zenye vijiji 98 vyenye wakazin  160818  ambapo gharama yake ni shilingi Bilioni 3.6.

Alisema katika awamu hiyo Mkoa wa Mbeya umetekeleza mradi huo wilayani Chunya katika Kata ya Chalangwa kijiji cha Shoga ambako umejengwa mnara unaotumia teknolojia ya CDMA ambapo mradi huo umegharimu shilingi 98,515,000 na kuwanufaisha wakazi 7343.

Alisema TTCL imejipanga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kirahisi ikiwa ni pamoja na Vocha , simu na vifaa vyake, Internet na Fax na kuongeza kuwa huduma zaidi zitaendelea kuongezeka.

Baadhi wa Wananchi waliozungumza na gazeti hili waliipongeza Kampuni ya TTCL kwa kuwajengea mnara wa mawasiliano na kwamba umewapunguzia gharama kubwa walizokuwa wakizipata awali kabla ya kuwepo kwa mnara huo.

Nathaniel Nakamia na Lusekelo Lwesha wakazi wa Kiji cha Shoga walisema kabla ya kujengwa kwa mnara huo na kuanza kutumika walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilomita 6 kufuata vichuguu ili wapate mawasiliano.

Walisema mbali na kusafiri umbali huo pia walilazimika kupanda pikipiki kwa gharama ya shilingi 3000 ili kufikia maeneo ambayo yalikuwa yanamawasiliano ya simu ili kuweza kuwasiliana na ndugu zao kutoka pande zingine.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika sherehe hizo, Katibu tawala wa Wilaya ya Chunya, Sosthenes Mayoka, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Deodatus Kinawiro, mbali na kuipongeza kampuni hiyo pia alisema kutokana na kuwepo kwa mawasiliano kijijini hapo kutasaidia kurahisisha shughuli za maendeleo na suala la ulinzi.

Alisema hivi sasa wananchi waweza kupiga simu moja kwa moja wilayani endapo kutatokea tatizo lolote hivyo kuifanya kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya kuchukua hatua za haraka.

Aidha alitoa wito kwa Wananchi kuutunza mnara huo kwani Kampuni hiyo imeonesha mfano wa kuigwa kwani makampuni mengine yameshindwa kupeleka huduma za mawasiliano vijijini wakihofia kupata hasara lakini wakasahau kuwa vijiji hivyo vinarasilimali za madini na mifugo ambapo wanauwezo wa kununua huduma za simu.

Hata hivyo Kampuni hiyo ilitoa simu mbili za mezani kwa Serikali za Vijiji vya Shoga na Sangambi ili zisaidie katika kurahisisha shughuli za maendeleo pamoja na mawasiliano kati ya viongozi na wananchi wao.

Mwisho. 
Na Mbeya yetu

No comments: