CHUO cha muziki cha Triple J Sound &
Music college kilichopo Ivumwe jijini Mbeya kimefanya mahafali yake ya
kwanza tangu kuanzishwa kwake katika sherehe zilizofanyika chuoni hapo.
Aidha katika mahafali hayo jumla ya
wanafunzi wanne wamehitimu na kukabidhiwa vyeti katika fani za uinjinia wa
sauti na utengenezaji wa muziki na watatu katika fani ya upigaji wa
vyombo(piano).
Mkurugenzi wa Chuo cha muziki cha Triple
j sound & music college, Dk. Leonard Maboko, akizungumza katika mahafali
hayo alisema watu wanajishughulisha na sanaa ya muziki ni vema kufanya
kazi hiyo baada ya kupata taaluma kutoka vyuoni ili kuboresha tasnia sambamba
na kupambana na ushindani wa soko.
Dk. Maboko alisema wasanii wengi wa
muziki wanashindwa kuendana na ushindani wa soko kutokana na kukosa elimu
ambayo itamsaidia kujua kutumia vifaa, kuandika na kuimba jambo linalosababisha
kukosa nyimbo zenye ujumbe kwa jamii.
Alisema kwaya nyingi na vikundi vingi
vya uimbaji havina wapigaji wazuri wenye vipaji na taaluma ya muziki pamoja na
ujuzi wa uimbaji jambo linalochangia muziki kutokuwa na ubora unaoweza kuleta
ushindani na ladha kwa wasikilizaji(hadhira).
Alizitaja kozi zinazotolewa chuoni hapo
kuwa ni mafunzo ya kupiga vyombo vya muziki, uinjinia wa sauti na utengenezaji
wa muziki, kuimba na kuandika muziki, kozi maalumu ya Software ya muziki
iitwayo Pro- tools, utengenezaji wa video, mafunzo ya msingi kwa elektronikia
na mafunzo ya awali ya Kompyuta.
Aliongeza kuwa lengo la Chuo hicho ni
kuzalisha wanafunzi wenye vipaji na ubunifu watakaoweza kuhimili ushindani na
kuinua tasnia ya muziki wa Tanzania hata kufikia ngazi ya kimataifa.
Kwa upande wake Wahitimu katika risala
yao kwa mgeni rasmi walisema ni vema viongozi wa vikundi vya muziki, wachungaji
na wazazi kuwapeleka watoto wao kujifunza masuala mbali mbali ya muziki ili
kuwafanya vijana kuwa wataalamu wa muziki waliobobea.
Naye Mgeni rasmi katika mahafali hayo,
Mchungaji Sunday Matondo, ambaye pia ni Mchungaji kiongozi wa Rehoboth
International Christian centre, mbali na kupongeza jitihada za Mkurugenzi kwa
kuanzisha chuo hicho pia alisema kitasaidia kuongeza ajira kwa vijana.
Alisema hivi sasa kunatatizo la watu
wengi kushindwa kufunga vifaa vya muziki katika mikutano jambo linalosababisha
kuunguza vifaa hivyo kutokana na uwepo wa Chuo tatizo hilo litaondoka na
kuwafanya vijana waliojifunza kuwa keki na kuajiriwa.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment